Watahiniwa zaidi ya milioni 1 darasa la saba 2025 kikaangoni kesho

September 9, 2025 3:24 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kufanya mitihani yao kwa siku mbili Septemba 11-12, 2025.
  • Watahiniwa waonywa kujiepusha na udanganyifu.

Dar es Salaam. Watahiniwa milioni 1.1 wa darasa la saba Tanzania Bara wanatarajia kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ikiwa lengo ni kupima maarifa na umahiri walioupata wanafunzi katika kipindi chote cha elimu hiyo.

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi (Primary School Leaving Examination PSLE) itafanyika kwa siku mbili kati ya Septemba 11 na 12, 2024.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta Prof Said Ally Mohamed aliyekuwa akitangaza kuanza kwa mitihani hiyo leo Septemba 9, 2025, jijini Dar es Salaam, wanafunzi watakaofanya mtihani huo wanatoka katika jumla ya shule 19,441.

“Watahiniwa waliosajiliwa 1,172,279, ambapo kati yao wavulana ni 535,388  sawa na asilimia 46 na wasichana ni 637,141  sawa na asilimia 54,” amesema Prof Mohamed.

Katika mitihani hiyo watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosajiliwa ni 4,679, sawa na asilimia 0.4 ya jumla ya watahiniwa wote wanaotarajiwa kufanya mtihani.

“Kati yao watahiniwa 92 ni wasioona, 1,551 wenye uoni hafifu, 1,079 wenye uziwi, 448 wenye ulemavu wa akili pamoja na 1,509 wenye ulemavu wa wa viungo,” amebainisha Dk Mohamed.

Watahiniwa hao watafanya mtihani huo katika masomo sita ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia (Science and Technology), Hisabati (Mathematics), Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi (Social Studies and Vocational Skills) pamoja na Uraia na Maadili (Civics).

Prof Mohamed ameongeza kuwa Maandalizi yote ya mtihani yamekamilika, ikiwemo usambazaji wa karatasi, semina kwa wasimamizi na maandalizi ya vituo. 

Weledi uzingatiwe

Aidha, Necta imewataka wasimamizi kufanya kazi kwa umakini, uadilifu na kwa kuzingatia kanuni za mitihani, huku likiwataka walimu na wakuu wa shule kuepuka kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani.

“Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wote wanafanya mtihani katika muda uliopangwa, na katika hali ya utulivu. Aidha, wahakikishe watahiniwa wenye mahitaji maalum wanafanya mitihani yao ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi…

… Haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu,” amesisitiza Prof. Mohamed.

Aidha, Necta imewataka wasimamizi kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kwa watahiniwa wenye mahitaji maalum.

Wakati huo huo, Necta imeitaka jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mitihani inafanyika kwa amani na utulivu ikionua vitendo vyovyote vya udanganyifu.

Mwaka 2024 watahiniwa 61 wa shule ya msingi walifutiwa matokeo yao huku watahiniwa 45, sawa na asilimia 0.03 ya waliofanya mtihani huo waliobainika kufanya udanganyifu na wengine 16 wakiandika matusi katika karatasi za kujibia mtihani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW