NECTA yapiga marufuku kuchapisha matokeo kwa majina ya wanafunzi bila idhini
- Ni kwa lengo la kulinda faragha na taarifa binafsi za kielimu za wahitimu na watahiniwa wote waliowahi kufanya mitihani.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limepiga marufuku vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, blogu na majukwaa ya habari kuchapisha au kusambaza matokeo ya mitihani kwa kutumia majina ya wanafunzi bila idhini yao, likieleza kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Uhusiano wa Necta, John Nchimbi, hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda faragha na taarifa binafsi za kielimu za wahitimu na watahiniwa wote waliowahi kufanya mitihani yake, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 ya mwaka 2023.
“Baraza la Mitihani linatambua umuhimu wa kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya kielimu ya wanafunzi na watahiniwa kwa kuzingatia misingi ya sheria, maadili na heshima kwa kulinda faragha zao,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Necta imeeleza kuwa inaendela kuboresha mifumo yake ya Tehama kwa kuondoa utaratibu wa kuonesha majina ya wanafunzi au watahiniwa katika tovuti yake rasmi ya www.necta.go.tz, ili kuhakikisha usalama wa taarifa binafsi.
Hata hivyo, agizo la Necta limekuja mara baada ya hivi karibuni vyombo vya habari na watu binafsi kuchapisha wasifu wa watu mbalimbali ikiwemo viongozi. Uchapishaji huo wa wasifu ulizua mijadala katika majukwaa ya mitandao ya kijamii huku kila mmoja akitoa mtazamo tofauti kulingana na wasifu wa elimu wa mtu husika.
Necta imesisitiza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote au taasisi kuhifadhi, kuchapisha, kusambaza au kuonesha hadharani matokeo ya mtahiniwa kwa kutumia jina lake au taarifa nyingine zinazoweza kumtambua bila idhini yake na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.