Udanganyifu, matusi vyawaponza watahiniwa 107 wa kidato cha nne 2023

January 25, 2024 1:16 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo iliyotangazwa mwaka huu imepungua kwa asilimia 68.
  • Katibu Mtendaji wa Necta asema udanganyifu huo ni wa wanafunzi wenyewe.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 107 wa kidato cha nne mwaka 2023 kwa makosa ya udanganyifu na kuandika matusi katika karatasi za majibu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 25, 2024, jijini Dar es Salaam amesema kati ya watahiniwa  waliofutiwa matokeo 102 walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi.

“Kuhusu udanganyifu watahiniwa 102 wa mwaka huu wote ni udanganyifu wa watahiniwa wenyewe kwa wenyewe ndio maana katika press ya leo  hujasikia tumefungia kituo cha mtihani,” amesema Dk.Mohamed.

Dk.Mohamed amebainisha kuwa watahiniwa hao waliofutiwa matokeo walifanya makosa mbalimbali ya udanganyifu ikiwemo kuingia na simu, ‘notes’ pamoja na kusaidiana majibu katika chumba cha mtihani jambo ambalo ni kinyume na sheria za baraza hilo.


Soma zaidi:Matokeo kidato cha nne 2023 haya hapa


Kwa mujibu wa kifungu cha  tano kipengele cha pili I na J cha Sheria za Necta namba 107 pamoja na kifungu cha 30 kipengele cha pili cha kanuni za mitihani za mwaka 2006 ni kosa kwa mtahiniwa kufanya udanganyifu wowote akiwa ndani ya chumba cha mtihani.

Idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo iliyotangazwa mwaka huu imepungua kwa asilimia 68 kulinganisha na watahiniwa 337 waliofutiwa matokeo mwaka 2022  kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya udanganyifu.

Ili kuendelea kudhibiti ongezeko la watahiniwa wanaofutiwa matokeo hayo hususan wanaoandika matusi Dk.Mohamed amesema Necta hutoa elimu katika shule na vituo vya mitihani ambapo watahiniwa hao wanatokea.

“Suala hili ni la kimaadili, kwanza tunaziandikia barua shule kwa ajili ya kuwaonya na kutoa elimu kwa wanafunzi wanaokuja katika madarasa yanayokuja nyuma kujua kwamba suala hili ni kinyume na sheria,” amesema Dk.Mohamed.

Huenda baraza hilo likawatazama kwa jicho la pili watahiniwa hao waliofutiwa  matokeo ili kuwapa nafasi ya kukamilisha hatua ya kuhitimu ngazi hiyo ya muhimu katika safari ya elimu nchini.

Itakumbukwa kuwa April 2023, Necta ilitoa fursa kwa wanafunzi 337 waliofutiwa matokeo katika mtihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2022 kurudia mtihani katiya Mei 2 hadi 15 mwaka 2023.

Aidha, Necta imesema mbali na kuwafutia matokeo wanafunzi hao itawachukulia hatua wengine wote watakaothibitika kujihusisha na udanganyifu huo ikiwemo walimu wakuu pamoja na wamiliki wa shule.

Enable Notifications OK No thanks