72 wafutiwa matokeo mtihani kidato cha nne 2024

January 23, 2025 4:25 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • 67 wafanya udanganyifu, 5 waandika matusi.
  • 459 washindwa kumaliza mitihani kutokana na matatizo ya kiafya.

Dar es salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefuta matokeo yote ya watahiniwa 72 wa kidato cha nne mwaka 2024 kwa kufanya vitendo vya udanganyifu na kuandika matusi kinyume na sheria za mitihani.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 23, 2025, jijini Dar es Salaam amesema kati ya waliofutiwa matokeo 67 walibainika kufanya udanganyifu huku watano wakifutiwa matokeo kwa kuandika matusi.

“Baraza limefuta matokeo yote ya wanafunzi 67 waliofanya udanganyifu na wanafunzi watano walio andika matusi,” amesema Dk Mohamed.

Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) (j) cha Sheria ya Necta sura ya 107 pamoja na kifungu cha 30(2) (b) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 ambayo inaeleza kuwa ni kosa kwa mtahiniwa kufanya udanganyifu wowote akiwa ndani ya chumba cha mtihani.

Sheria ya mitihani inaeleza kuwa ni kosa kwa mtahiniwa kufanya udanganyifu wowote akiwa ndani ya chumba cha mtihani. Picha | Kelvin Makwinya, Nukta

Hata hivyo, idadi hiyo ya watahiniwa waliofutiwa matokeo imepungua kutoka 107 ya mwaka 2023 ambapo kati yao 102 walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi.

Kutokana na muendeleo wa watahainiwa kuandika matusi katika mitihani ya kitaifa Dk Mohamed amewarai wazazi pamoja na walezi kuwekeza katika maadili ya watoto wao kwa kuwa matusi hayakubaliki katika misingi ya maadili ya jamii yoyote ile.

“Matusi ni suala linaloendana na maadili, matusi sio suala linaloendana na mitihani tu, kwenye chumba cha mtihani matusi hayakubaliki, matusi hayakubaliki popote… kama jamii tuendelee kukemea, lakini kanuni za mitihani ziko wazi ukiandika matusi unafutiwa matokeo” amesisitiza Dk Mohamed.

Aidha, Necta imekifungia kituo cha mitihani cha watahiniwa wa kujitegemea chenye namba za usajili P6384 BSL Open School kilichopo mkoani Mwanza kwa kuratibu mipango ya udanganyifu ambapo tayari baraza limeshawafungulia kesi ya jinai mahakamani.

Kwa upande mwingine Necta imezuia matokeo ya watahiniwa 459 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

Hata hivyo, Dk Mohamed amesema watahiniwa hao watapata nafasi ya kufanya mitihani hiyo mwaka 2025 kwa masomo ambayo hawakufanya kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks