Necta yawafutia watahiniwa 31 matokeo kwa udanganyifu
- Shule mbili zafungiwa, nne zapewa onyo.
- Ni kwa mujibu wa sheria za Necta Sura ya 107.
- Zitakuwa chini ya uangalizi maalumu wa Necta kwa muda usiojulikana.
Dar es Salaam. Wakati mamilioni ya wazazi, walezi na wanafunzi wanasheherekea matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa leo Novemba 23. 2023, hali ni tofauti kwa watahiniwa 31 ambao matokeo yao yamefutwa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Dk. Said Mohamed aliyekuwa akizungumza na wanahabari wakati wa kutangaza matokeo, amebainisha kuwa wanafunzi hao wamefutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya udanganyifu.
“Necta imefuta matokeo yote ya watahiniwa 31 sawa na asilimia 0.002 ya watahiniwa 1,356,392 waliofanya mtihani ambao wamebainika kufanya udanganyifu,” amesema Dk. Mohamed.
Bofya hapa kutizama matokeo ya darasa la saba 2023
Aidha, Dk. Mohamed ameongeza kuwa adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kifungu 30(2)b cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 kikisomwa pamoja na kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha sheria za Necta sura ya 107.
Hata hivyo, idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka 2023, imepungua kutoka ile ya Mwaka 2022, ambapo Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 2,194 waliobainika kufanya vitendo vya udanganyifu.
Shule mbili zafungiwa, nne zapewa onyo
Pamoja na kufuta matokeo ya watahiniwa hao Necta pia imezifungia shule mbili za Twibokhi na Graiyaki za mkoani Mara, kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Soma zaidi : Ufaulu matokeo ya darasa la saba waongezeka kiduchu
Itakumbukwa kuwa mwaka 2022, zaidi ya wanafunzi 60 walifutiwa matokeo yao ya kidato cha nne na Necta kutokana na kuhusika na vitendo vya udanganyifu.
Sambamba na hilo Necta imeziandikia barua za onyo shule nne za St. Mary’s Mbezi Beach, na Mother of Mercy za Dar es Salaam, Charm Moderm ya Arusha pamoja na Morotonga ya Mara, baada ya kujaribu kujihusisha na vitendo vya udanganyifu ambavyo ni kinyume cha sheria.
“Vituo hivyo vitakuwa chini ya uangalizi wa Necta mpaka hapo baraza litakapojiridhisha kuwa ni vituo salama kwa uemdeshaji wa mitihani ya Taifa,” amesema Dk.Mohamed.
Latest