Fahamu sababu za wanafunzi kuandika matusi katika mitihani

November 11, 2024 5:05 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na wanafunzi kuwa na maandalizi hafifu pamoja na ukosefu wa maadili.

Arusha. Kila mwaka wanafunzi wa ngazi mbalimbali nchini ikiwemo darasa la nne, kidato cha pili, kidato cha nne na cha sita hufanya mitihani ya upimaji wa kitaifa inayowawezesha kuendelea na ngazi nyingine za kielimu.

Licha ya umuhimu wa mitihani hiyo, baadhi ya wanafunzi hujikuta wakifutiwa matokeo kutokana na vitendo vya kuandika matusi katika karatasi za kujibia mitihani badala majibu ya maswali waliyoulizwa.

Mathalani, Oktoba 2024, wanafunzi 61 waliofutiwa matokeo ya kuhitimu elimu ya shule ya msingi na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kwa udanganyifu na kuandika matusi.

Wakati mitihani ya kidato ya nne iliyoanza leo Novemba 11, 2024 ikiendelea wadau wa elimu wameeleza sababu za wanafunzi kuandika matusi katika mitihani ya ngazi mbalimbali za elimu mmomomnyoko wa maadili na maandalizi finyu.

Hali hiyo inayojitokeza kila mwaka imekuwa ikikemewa vikali na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) huku ikitoa adhabu hiyo ya kuwafutia matokeo wanafunzi hao kwa mujibu wa sheria za baraza hilo.

Hata hivyo, adhabu hiyo siyo muarobaini wa tatizo hilo ambapo kila mwaka idadi ya wanaoandika matusi hupanda na kushuka kulingana na ngazi ya elimu.

Mathalani\ katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa Oktoba 29 mwaka huu Necta ilifuta matokeo ya wanafunzi 16 kwa kuandika matusi katika karatasi za kujibia mtihani.

Kwa upande wa  matokeo ya kitaifa ya upimaji wa darasa la nne mwaka 2023 Necta iliwafutia matokeo wanafunzi watatu, huku wengine wa 14 wa kidato cha pili na 14 kidato cha pili wakiingia kwenye orodha hiyo.

Sababu za kuandika matusi zatajwa

Shabani Omary Mwalimu wa Shule ya Sekondari  ya Kiislamu Arusha ameiambia Nukta habari kuwa tatizo la wanafunzi kuandika matusi hujitokeza pia hata katika mitihani ya ndani ambapo husababishwa na wanafunzi hao kuwa na maandalizi finyu.

“Hakuna mwanafunzi ambaye amejipanga kufaulu akaandika matusi kwenye mtihani hao wanaoandika matusi unakuta hawana maandalizi wengine hata maudhurio yao huwa ni hafifu,” amesema mwalimu Omary.

Mwalimu Omary ameogeza kuwa wanafunzi wengine wenye tabia za kuandika matusi huwa hawapendi shule na hulazimishwa na wazazi kufanya mitihani hiyo huku pia mmomonyoko wa maadili unaosababisha wanafunzi kujifunza lugha za matusi kuwa chanzo.

“Hawa watoto hususani wanaosoma shule za kutwa wanachanganyika sana na jamii na huko wanajifunza matusi na lugha za mtaani mwanafunzi akiingia kwenye mtihani kichwa chake kimejaa tu mambo hayo yasiyo na maadili,”ameongeza Mwalimu Omary.

Ili kumaliza tatizo hilo Mwalimu Omary ameshauri wazazi kutokuwalazimisha watoto masomo, badala yake wakae nao na kuwaeleza umuhimu wa safari hiyo ya elimu ambayo wanaendelea nayo.

“Wazazi pamoja na walimu wanajukumu la kuwaambia watoto kwanini wapo shule tangu wakiwa shule ya msingi darasa la kwanza ili kuwasaidia wazingatie masomo na kufaulu vizuri,”amesema Mwalimu Shabani.

Naye Richard Mabala, Mwandishi wa vitabu na mchambuzi wa masuala ya elimu amesema idadi ya wanaoandika matusi katika mitihani ni ndogo na inaweza kushughulikiwa kwa kuimarisha miundombinu ya elimu.

“Kwa mawazo yangu hao wanaoandika matusi ni chini ya asilimia moja na huwezi kujua sababu ni nini…naona tuwe na  walimu wa kutosha, vitabu vya kutosha pia tubadilishe lugha ya kufundishia ili wanafunzi waingie uwanjani kwa pamoja washindane kwa usawa,”amesema Mabala.

January 25, 2024 Necta pia ilianika mbinu za kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaoandika matusi ikiwemo utolewaji wa elimu katika shule na vituo vya mitihani ambapo watahiniwa hao wanatokea.

“Suala hili ni la kimaadili, kwanza tunaziandikia barua shule kwa ajili ya kuwaonya na kutoa elimu kwa wanafunzi wanaokuja katika madarasa yanayokuja nyuma kujua kwamba suala hili ni kinyume na sheria,” amesema Dk. Mohamed.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks