Namna ya kuwanusuru wafanyakazi wa ndani na madhara ya Corona
- Baadhi yao wafukuzwa kazi na kunyimwa mishahara yao.
- Janga la Uviko-19 lachangia madhira wanayopitia.
- Wadau waungana kuwapigania.
Iringa. Ilikuwa jumamosi majira ya saa 10 jioni, alipofukuzwa kazi na bosi wake kwa sababu tu alihoji mshahara wake ambao hakulipwa kwa miezi minne mfululizo.
Ester* (si jina lake halisi) mkazi wa Manispaa ya Iringa katika Mkoa wa Iringa alikuwa mfanyakazi wa ndani aliyepoteza kazi yake Oktoba 2020 baada ya kushindwa kuelewana na bosi wake kutokana na kucheleweshwa malipo yake.
Binti huyo, aliyekuwa analipwa Sh40,000, alikuwa akifanya kazi katika moja ya nyumba yenye familia ya watu wanne katika moja ya mtaa katika manispaa hii.
“Aliniambia hana pesa kwa sababu shughuli zake hazijamwendea vizuri (kwa sababu ya Uviko) na alinikitaka niondoke nyumbani kwake,” anasema Ester akiongeza kuwa biashara ya bosi wake ilikuwa imeathiriwa vibaya ugonjwa wa virusi vya Uviko-19.
Kutolipwa mshahara kulianza baada ya shughuli za bosi wake za kutoa huduma ya chakula kwenye sherehe hasa za harusi kuyumba kutokana na Serikali ya Tanzania kupiga marufuku shughuli za mikusanyiko ya watu kuwakinga raia wake na Uviko-19.
“Pale nyumbani mambo yalibadilika hata hela ya matumizi nayo ilipungua,” anaelezea Ester hali ya nyumbani kwa bosi wake mara baada ya Uviko-19 kuingia nchi Machi 2020.
Jitihada za kumpata bosi wa Ester kuelezea madhira hayo na madai ya aliyekuwa mfanyakazi wake hazijazaa matunda mpaka sasa.
Ester ambaye kwa sasa yuko nyumbani bila kazi yoyote ni miongoni mwa maelfu ya wafanyakazi wa ndani ambao wamepoteza kazi zao duniani kutokana na athari za kiuchumi za Uviko-19.
Elimu na msaada wa kisheria ukitolewa kwa wafanyakazi wa ndani utawasaidia kuzijua haki zao na hivyo kuboresha maisha yao. Picha| Shutterstock.
Ripoti iliyoangazia haki za wanawake kazini iliyotolewa Julai 2021 na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) imeeleza kuwa wanawake wachache kati ya wengi waliopoteza ajira kutokana na Uviko-19 wataweza kupata kazi nyingine ikilinganishwa na wanaume.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani sawa na kupoteza ajira milioni 54 kwa mwaka.
Kadhia hiyo iliyompata Ester pia ilimpata Edna James ambaye aliondolewa kazi ghafla na bosi wake mara tu baada ya Uviko-19 kuingia Tanzania na hivyo kupoteza haki zake za msingi ikiwemo mshahara.
Tofauti na Ester, Edna aliondolewa kazini kwa sababu bosi wake alitaka kupunguza idadi ya watu nyumbani kwake ili kujikinga na Uviko-19.
Anaeleza kuwa aliambiwa na bosi wake kuwa atarudishwa kazini mara baada ya janga la Uviko-19 kuisha lakini mpaka sasa hajapata majibu yoyote.
Hata hivyo, Edna alifikisha malalamiko yake kwa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU) ambapo kesi yake inaendelea kushughulikiwa.
Wakati mabosi wengine wakiwaondoa kazini wafanyakazi wa ndani, wengine wameendelea kuishi nao huku wakichukua tahadhari zote za kujikinga dhidi ya Uviko-19 na kuwapa stahiki zao.

Mabosi wengine wawajali wafanyakazi wa ndani
Mkazi wa kata ya Frelimo katika Manispaa ya Iringa, Zaituni Mkwawa anasema yeye hakuona sababu ya kumuondoa mfanyakazi wake kwa sababu ni sehemu ya familia licha kuwepo kwa changamoto za Uviko-19.
“Corona haijaleta changamoto katika familia yangu, dada wa kazi analipwa kama kawaida lakini tumejiwekea utaratibu mzuri kujilinda ili tusipate huo ugonjwa,” anasema Mkwawa ambaye katika mlango wa kuingilia nyumbani kwake kuna ndoo ya kunawia mikono.
Mama huyo, mwenye watoto watatu, anaeleza kuwa pia familia yake inatumia barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya.
Kwa mujibu wa ILO, kada ya wafanyakazi wa ndani nchini Tanzania imeajiri zaidi ya watu milioni 1.1 sawa na asilimia 5 ya wafanyakazi wote nchini.
Kwa upande wa dunia, kada hiyo imeajiri zaidi ya watu milioni 75.6 sawa na asilimia 4.5 ya wafanyakazi wote duniani na wanawake ni zaidi ya asilimia 70 wa wafanyakazi hao.
Wafanyakazi wa ndani ni sawa na wafanyakazi wengine ambao wanastahili heshima na kutunza ili kuboresha maisha yao. Picha| Shutterstock.
Namna ya kuwanusuru wafanyakazi wa ndani
Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu) ambacho kinasimamia maslahi ya wafanyakazi hao kinaeleza kuwa wanatoa elimu majumbani namna ya kujikinga na Uviko-19 ili waendelee kufaidika na kazi zao.
“Huwa tunapita majumbani tukishirikiana na wadau wengine kuelimisha umma na kuhimiza kuchukua tahadhari ikiwemo wafanyakazi hawa kupewa vifaa vya kujikinga na matibabu wakipata ugonjwa huo,” anasema Daudi Mapuga, Katibu wa Chodawu Mkoa wa Iringa.
Kupunguza athari za kufurushwa bila malipo, chama hicho kuwa kinawajengea uwezo wafanyakazi wa ndani kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya kazi ambayo inaweza kuwalinda hata wakifukuzwa au kunyimwa haki zao na waajiri wao.
Kwa mujibu wa Mapuga, changamoto kubwa zinazowakabili wafanya kazi wa ndani hasa wakati huu wa Uviko-19 ni kutolipwa mishahara kwa wakati, kufanya kazi muda mrefu, kutengwa na kunyimwa chakula, jambo ambalo wao wanapambana nalo kuliondoa.
“Kwa wale ambao tayari wamefukuzwa kazi au wamedhulumiwa haki zao, tunafungua mashauri hapa ofisini na waajiri wao wanaitwa ili kusuruhisha hizo kesi,” anasema Mapuga ambaye ofisi yake hupokea kesi sita mpaka 10 za wafanyakazi wa ndani.
Dhana hasi kuwa wafanyakazi wa ndani wanaweza kuchangia kueneza Uviko-19 hazina mashiko kwa kuwa kila mtu anawezwa kupatwa na maradhi hayo hivyo tahadhari inapaswa kuchukuliwa bila kujali vyeo au nafasi katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Mohamed Moyo anawahimiza wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono.
“Tuhimizane kila mmoja ndani ya familia huu ugonjwa upo na kila kundi lipewe kipaumbele ili wote tuwe salama,” anasema Moyo.
Makala haya ni sehemu ya mfululizo ya ripoti maalum zinazoangazia namna ya kukabiliana na Uviko-19 nchini zinazofadhiliwa na Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
