Mwanamke shujaa anayekabiliana na Corona mpakani Tunduma

October 25, 2021 11:33 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Esta Mwampashi, mfanyabiashara wa vinywaji mkoani Songwe.
  • Biashara yake imeyumbishwa na athari za Uviko-19.
  • Amegeukia kilimo, Vicoba kupunguza athari katika biashara yake.

Songwe. Shughuli za kawaida na hekaheka za hapa na pale zikiwa zinaendelea katika mji wa kibiashara, Tunduma ambao ni mpaka wa Tanzania na Zambia zinaashiria namna mji huo ulivyo “bize”

Unapofika tu eneo hili ni kawaida kuona wanawake kwa wanaume wakiwakaribisha watu kwenye biashara zao; nyingi kati ya hizo ni biashara za vinywaji, chakula, kubadilisha fedha na sukari.

Watu wa mpaka huu uliopo mkoani Songwe, hufanya shughuli hizo mchana na usiku kutokana na kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu wanaotoka mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya na hata nchi jirani ya Zambia.

Licha ya pilika pilika za mpakani hapa, Esta Mwampashi (34), mfanyabiashara katika eneo hilo bado anaugulia maumivu ya athari za janga la Corona (Uviko-19) lililoathiri biashara yake tangu Machi 2020.

Licha ya biashara yake kwenda kinyume na matarajio yake, mwanamke huyo anayefanya biashara ya kuuza bidhaa za nyumbani ikiwemo vinywaji baridi, mafuta na sukari, amebaki imara na Uviko-19 umemfungulia fursa nyingine za kuingiza kipato.

“Kwa sasa hali ni mbaya usishangae nikikumbia mpaka jioni hii mauzo hata 10,000 haifiki tofauti na hapo nyuma nilikuwa naweza kuuza mpaka 100,000 kwa siku ila sasa hali ni mbaya,”  anasema Esta ambaye ni mkazi wa mji mdogo wa Tunduma.

Kuyumba kwa biashara kulitokana na kufungwa kwa mpaka huo na nchi jirani ya Zambia na kuwaweka raia wake katika vuzuizi vya nyumbani (lockdown) ili kuwakinga na ugonjwa huo.

Hata baada ya kufunguliwa kwa mpaka huo na kuanza kutolewa kwa chanjo ya Uviko-19, bado shughuli za kibiashara katika eneo hilo hazijachanganya kama ilivyokuwa awali. 

Esta mwenye watoto watatu anasema wateja wakubwa walikuwa wanatokea Zambia na sasa wamepungua kwa sababu ya kuimarishwa kwa masharti ya udhibiti wa Uviko-19 kwa pande zote mbili.

Esta Mwampashi akiwa katika biashara yake katika mpaka wa Tunduma. Picha| Isakwisa Mbyale.

Anasema uwezo wake wa kuhudumia familia umepungua kutokana na kupungua kwa kipato kilichoathiriwa na uviko 19 katika eneo hilo la mpakani.

“Hii biashara nimekuwa nikiifanya kwa miaka mitatu sasa, wanangu wanaitegemea biashara hii ili kula, kuvaa na mahitaji mengine ya shuleni,” anasema Esta ambaye ametengana na mume wake. 

Ripoti ya utafiti wa ajira uliofanywa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) ya mwaka 2021 imeeleza kuwa wanawake wamepoteza  ajira na kukosa kipato kwa sababu maeneo wanayofanyia kazi ikiwemo sekta ya malazi, chakula na utengenezaji bidhaa yameathirika zaidi na janga la Corona.

Utafiti unaonyesha kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani sawa na kupoteza ajira milioni 54, wakati wanaume waliathirika kwa asilimia 3 au ajira milioni 60. 

Akiwa amevalia gauni la maua ya kijani pamoja na mzula mwekundu, Esta anaonekana mwenye ucheshi kwa sababu kushuka kwa mapato katika biashara yake kumemfikirisha zaidi kutafuta mbinu nyingine zinazomsaidia kutunza familia na kuendesha maisha yake.


Mbinu anazotumia kushinda athari za Uviko-19

Baada ya kuona biashara ya vinywaji haimletei tija ameamua kuanzisha kilimo cha mahindi na maharage ambacho kwa sasa kimemletea ahueni ya maisha.

“Mwaka huu nilijikita zaidi kwenye kilimo maana mwaka jana nilipitia wakati mgumu wa uchumi kutokana na biashara kutonipa faida, hivi sasa tayari nimevuna mazao yangu naweza kuhudumia familia na nimepunguza ukali wa maisha,” anasema Esta.

Mazao hayo pia huyatumia kwa ajili chakula nyumbani na biashara yake ili kupata kipato na maisha yasonge mbele. 


TANGAZO:


Pia amelazimika kuondoka katika baadhi ya vikundi vya kuweka na kukopa kutokana na kushuka kwa mauzo hivyo kusalia na kikundi kimoja ambacho ataweza kushiriki kikamilifu.

“Wanawake sisi tunacheza tumichango hivyo sasa hivi imenilazimu kuacha vikundi vingine na kubaki na kikundi kimoja pekee,” anasema mwanamke huyo.

Katika kikundi ambacho ni mwanachama kina wanawake 50, kila wiki huchanga Sh5,000 hivyo kutoa nafasi ya kupata mkopo nafuu unaowasaidia katika kuendeleza mitaji ya biashara zao pamoja na kuhudumia famia.

Akipokea fedha za kikundi huziweka katika biashara yake ya vinywaji ili isife kabisa ingawa bado ina mwendo wa ‘konokono’.

“Utakuta mkishavunja kale kamchango kako unakaingiza kwenye biashara wakati mwingine unakopa na maisha yanaenda,” amebainisha Esta.

Esta anasema katika kipindi hiki, wanawake wanaweza kuwa na shughuli zaidi ya moja ya kuwaingizia kipato ili yanapotokea majanga kama Uviko-19 wasiyumbe kimaisha.

Wafanyabiashara katika mpaka wa Tunduma wakiendelea na shughuli zao. Picha| Isakwisa Mbyale.

Nini kifanyike kuwainua wanawake?

Nchi ambazo wanawake wameathirika zaidi na janga hilo wanaweza kutumia mbinu zilizotumiwa na baadhi ya nchi duniani kulikwamua kundi hilo.

Kwa mujibu wa ILO, zipo baadhi ya nchi ikiwemo Chile na Colombia ambapo ruzuku ya mshahara ilitolewa huku kiwango cha juu ya ruzuku wakipewa wanawake. Colombia na Senegal zilikuwa miongoni mwa nchi zilizotengeneza au kuimarisha usaidizi kwa wanawake wajasiriamali. 

Wakati huo huo, Mexico na Kenya waliweka upendeleo maalum katika kuhakikisha wanawake wananufaika na ajira kwenye miradi ya umma.

Mbinu zingine ambazo ripoti ya ILO imependekeza ni kuhakikisha kunakuwa na usawa katika malipo ya kazi, kutengeneza programu za kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fedha za mitaji na kuwapatia ajira ili wapate kipato.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV