Barakoa zilizotumika zinavyowaweka mtegoni wazoa taka, watoto

August 26, 2021 4:42 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni barakoa zinazozagaa mtaani na kutokohifadhiwa vizuri kwenye vyombo vya taka.
  • Wazoa taka wasiotumia vifaa vya kujikinga wako hatarini kupata Uviko-19
  • Serikali mbioni kutoa mwongozo wa kukusanya na kuteketeza taka za barakoa.

Dar es salaam. Ni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika dampo la Mpiji, shughuli ya kushusha mizigo ya taka zilizokusanywa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo inaendelea.

Taka hizo zinashushwa na kuwekwa katika maeneo salama kwa ajili ya kuchomwa katika bonde hilo lilipo katika Mto Mpiji unaotenganisha jiji hili na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. 

Dampo hilo hujumuisha taka za aina nyingi hasa zile zinazozalishwa majumbani na mitaani ikiwemo plastiki, vyakula vilivyotumika, vifaa vya kielektroniki na hata barakoa ambazo hutumika kujikinga na Corona (Uviko-19).

Salum Hassan ni miongoni mwa wafanyakazi wanaosafisha mazingira yanayozunguka dampo hilo huku akiwa hajavaa mavazi maalum ya kukinga afya yake ikiwemo barakoa, ‘gloves’ wala kofia maalum.

“Mi naamini kila mtu hapa anajielewa, Sivai ‘gloves’ wala barakoa naona uzito sana nikivaa wakati nafanya kazi”, anasema Hassan huku akishika taka na kuweka mahali zinapotakiwa. 

Asichokijua Salum kuwa kwa kutochukua tahadhari anajiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Uviko-19 kutokana na kushika taka kwa mikono yake na harufu kali iliyopenya puani. 

Wataalam wa afya kikiwemo Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) wanaeleza kuwa virusi vya Uviko-19 vinaweza kukaa kwenye vitu zikiwemo barakoa zilizotumika kwa siku tatu (saa 72) vikiwa hai.

Ikiwa mtu atashika maeneo au kugusa barakoa yenye virusi anaweza kuambukizwa ugonjwa huo. 

“Mfano mimi nimevaa barakoa nikatupa kiholela, naweza kusababisha madhara mfano akaokota mtoto akavaa au mtu mzima akashika anaweza kuchukua bakteria ambao wanaweza kuwa hatarishi kwa afya ya aliyeokota,” anasema Dk Ambilikile Malango kutoka hospitali ya Sarib Healthcare ya jijini hapa.

Takataka zikiwemo barakoa zilizotumika katika dampo la Mpiji lililopo jijini Dar es Salaam ambako baadhi ya wazoa taka hawachukui tahadhari kujikinga na uviko-19. Picha | Clifford Sangai

Hata wakati Sulum  akionesha kutokujali, wafanyakazi wenzake wapatao saba kwenye dampo hilo wamevaa mavazi ya kuwakinga na magonjwa wakati wakitimiza majukumu yao.

Mfanyakazi wa dampo hilo, Asha Said (34) anasema kutokana na shughuli anazofanya uwezekano wa kupata maambukizi ya Uviko-19 ni mkubwa kwa sababu muda mwingi anashughulika na taka hivyo kuchukua tahadhari kwake siyo jambo la hiari.

“Pamoja na kazi yangu hii, naogopa hili janga. Japo siwezi kuvaa barakoa kutokana na kutumia nguvu nyingi, ila tahadhari zote nachukua kama kawaida,” anasema Asha.

                               

‘Hatari zaidi’

Pia siyo tu wazoa taka wa jijini hapa wako katika hatari ya kupata Uviko-19 kutokana na barakoa zilizotumika, pia watoto wanaocheza katika mitaa ambako barakoa za kutumika mara moja (disposal mask) hutupwa kiholela. 

Esther Daniel, mfanyabiashara katika soko la Mwananyamala jijini hapa anasema anajitahidi sana kumchunga mtoto wake asicheze mbali na mazingira aliyopo ili kuepusha madhara yatokanayo na kuokota takataka zikiwemo barakoa zilizotumika.

“Huyu mtoto ni mdogo nikizubaa tu ameshanitoroka, najitahidi sana kumchunga maana hili janga sasa hivi nasikia halichagui umri,” anasema Esther akiwa na mtoto wake wa miaka mitatu huku akiendelea kukaanga mihogo. 

Wafanyakazi wakikusanya na kuteketeza taka katika dampo la Mpiji kwa Mgosha. Picha | Clifford Sangai.

Kukabiliana na hatari hiyo, baadhi ya wafanyabiashara wameshauri watu kutumia barakoa za vitambaa ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja, jambo litakalosaidia kupunguza kuzagaa kwa barakoa mitaani na maeneo ya umma. 

“Tunauza za kitambaa 1,000 kwa sababu unaweza kufua, ikakauka ukapiga pasi vizuri na kutumia tena kwa mara nyingine tofauti na hizi za kawaida unazokaa nazo masaa machache na kutupa ambazo ndiyo tunaona zinazagaa kila mahali mtaani,” anasema Neema Shirima, muuza barakoa katika stendi ya daladala ya Makumbusho.

Pia Barakoa ni miongoni mwa taka ngumu zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira kama uchafu mitaani hata kuziba njia za kupitisha maji  iwapo hazitahifadhiwa vizuri.

Nini kifanyike kuhifadhi barakoa zilizotumika?

Kwa mujibu wa mwongozo wa utumiaji wa barakoa uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), utupaji holela wa barakoa zilizotumika unaweza kusababisha maambukizi ya virusi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Hivyo ni muhimu kuzihifadhi sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa maambukizi.

“Barakoa ya aina yoyote inahitaji uhifadhi mzuri ili kuepuka uwezekano wa kusambaza maambukizi ya Corona,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo.

Dk Malango anasema barakoa ikishatumika inatakiwa iwekwe sehemu maalum ya kutupia taka na ambayo siyo rahisi kufikiwa na watu hasa watoto wadogo. 

“Ni vyema mtu baada ya kuvua barakoa yake aikunje vizuri na kuiweka katika chombo au mfuko utakaopelekwa katika eneo stahiki la kuhifadhia taka baada ya kutupa ili kuepuka kuzagaa kunakoweza kusababisha maambukizi,” anasema mtaalam huyo wa afya.

                         

Barakoa zilizotumika zikihifadhiwa vizuri, uwezekano wa kupata maambukizi unakuwa mdogo kuliko zikitupwa maeneo yanayoweza kufikiwa na watu kwa urahisi.

“Jambo la msingi ambalo liko wazi, inashauriwa barakoa ikishatumika itupwe kwenye eneo husika la kuhifadhia taka ambapo hazitaguswa na yule anaefanya kazi ya kukusanya zile taka ili naye asije akaathrika,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Mhandisi Samuel Gwamaka.

Ili kutunza mazingira, Mhandisi Gwamaka anashauri wananchi kuwa na utaratibu mzuri wa kutenganisha na kuhifadhi taka kulingana na aina zake ili kupunguza athari kwa mazingira hasa pale zinapotua ardhini.

“Sisi kama Baraza tunaendelea kuwasihi wananchi waweze kutofautisha namna wanavyotupa hizi taka pale zinapozalishwa hasa katika taasisi, mashule hata makazi ya watu. Inapaswa kuwa na mapipa/madebe yenye rangi tofauti ambayo taka zitaweza kutengwa,” anasisitiza mkurugenzi huyo.

Anasema NEMC kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanatengeneza mwongozo utakaotumika kuelekeza namna taka kama barakoa zinavyopaswa kukusanywa na kuteketezwa.

Makala hii imeandaliwa kwa ushirika na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).  

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW