Ahueni kwa bodaboda Tanga baada ya utalii kuanza kuimarika
Ramani inayoonyesha umbali uliopo kutoka msitu wa Magoroto na kituo cha mabasi cha Muheza mkoani Tanga.
- Ni wale wanaosafirisha watalii ambao waliathiriwa na Uviko-19.
- Waanza tena kutoa huduma na kupata kipato katika vituo vya utalii japo si kama awali.
- Serikali yahamasisha watu kutembelea vivuto vya utalii huku wakijikinga na Uviko-19.
Tanga. Alikuwa mmoja ya madereva wa bodaboda walionikimbilia na kuomba kutoa huduma ya usafiri baada ya kushuka katika stendi kuu ya mabasi iliyopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Kati ya bodaboda wanne walionisogelea, Ramadhani Kirua alikuwa wa kwanza kiasi cha kunivutia kumchagua kutokana na kasi yake ya kutaka kutoa huduma kwa haraka.
Kirua husafirisha wageni wanaotembelea vivutio vilivyomo Muheza ukiwemo msitu wa Magoroto na milima ya Usambara.
Usafiri wa bodaboda ni maarufu kwa watalii wanaotembelea wilaya hiyo kwa sababu huwafikisha kirahisi katika vituo vya utalii ambako magari hayafiki hasa sehemu za milimani ambazo hazina barabara za lami.
“Dada unakwenda wapi?” aliuza kwa haraka. Nikamjibu “Magoroto”. Ghafla uso wake ukajawa na tabasamu kuashiria kuwa siku yake itaenda vema kwa sababu ana uhakika wa kupata fedha.
“Mungu mkubwa tunarudi kwenye reli,” anasema Kirua huku akisema nitakutoza Sh25,000 tu kwa safari ya leo.
Furaha ya Kirua haikua bure kwa sababu ameanza kuona ahueni baada ya kuingia kwa ugonjwa wa Corona nchini Tanzania Machi 2020 na kuathiri shughuli za utalii na hivyo kuwakosesha mapato waliyokuwa wanayapata awali.

Ramadhani Kirua anayejishugulisha na shughuli ya kusafirisha watalii Wilayani Muheza. Picha | Gift Mijoe
Wakati tukiwa njiani kuelekea katika msitu wa Magoroto ambapo ni mwendo wa nusu saa katika barabara ya vumbi inayokatiza katika safu ya milima, Kirua anasema janga la Uviko-19 limeathiri sana biashara zao kwa sababu watalii wamepungua.
“Zamani mtu ulikuwa unaweza kupanda (Magoroto) huku mara tatu mpaka mara nne kwa siku, baada ya janga la Corona kupukutisha watalii vipato vyetu vilishuka sana mpaka kupanda mara moja kwa wiki au wiki mbili,” anasema dereva huyo mwenye mke na watoto wawili.
Kabla ya Uviko-19, kijana huyo na madereva wengine wa bodaboda walikuwa na uhakika wa kupata Sh40,000 hadi Sh50,000 kwa siku lakini baada ya janga hilo anaweza kupata safari moja au mbili kwa wiki na kuambulia Sh25,000 tu.
Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zilizoathirika kwa kiwango kikubwa na janga la Corona kwa sababu ya safari za kimataifa zilizuiliwa.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) linaeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa ilipungua kwa asilimia 73 mwaka 2020 huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.
Mwaka 2020 Tanzania ilipokea watalii 620,867 ikiwa ni pungufu mara mbili ikilinganishwa na watalii milioni 1.5 wa mwaka 2019, kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kushuka kwa mapato ya Kirua, kumeathiri hadi familia yake kwa sababu shughuli hiyo ndiyo humpatia kipato cha kutunza na kusomesha watoto wake.
Waangazia fursa nyingine kuendesha maisha
Mbali na kazi ya kusafirisha watalii, baadhi ya madereva hawakukubali kulala njaa, badala yake wamegeukia shughuli nyingine za kibiashara ili kuendelea kupata kipato.
Dereva wa bodaboda wilayani humo, Mohamed Mnyone anasema baada ya hali ya uchumi kuyumba alifungua genge la bidhaa za nyumbani ili apate chochote cha kujikimu kimaisha.
Hadi sasa Mnyone anaendelea kuifanya biashara hiyo ya genge huku akisubiri hali ya utalii iimarike licha ya kuwa anapata wateja wachache ambao wameanza kwenda katika msitu wa Magoroto.
“Nilipigiwa simu na wateja wangu nikiwa kwenye shughuli zangu zingine. Sasa naweza kupata ujasiri wa kuweka mafuta nianze tena kusaka wateja,” anasema Mnyone.
Baada ya hatua mbalimbali ikiwemo utoaji wa chanjo ya Uviko-19, shughuli za utalii duniani na Tanzania zimeanza kurejea, hivyo kuwapata matumaini madereva hao kuwa huenda kipato chao kikazidi kuongezeka siku zijazo.
Mandhari ya Msitu wa Magoroto ambao hutumika kwa shughuli za utalii mkoani Tanga. Picha| Gift Mijoe.
Hatua zinazochukuliwa kuimarisha utalii
Kutokana na kulegezwa kwa masharti ya Uviko-19 ikiwemo safari za kimataifa, wadau wa utalii ukiwemo uongozi wa Magoroto unaendelea kutangaza vivutio vyake ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Magoroto ni kivutio cha watalii wanaopenda kupanda milima, kutazama mimea adimu, kuona au kununua bidhaa za utamaduni na asili, kutembelea mashamba ya zamani ya mawese na kuogelea katika ziwa lililopo katika eneo hilo.
“Tuna imani kuwa janga hili litaisha. Kwa kasi hii ya utoaji chanjo, watu wameanza tena kutalii na kusafiri, tuna matumaini makubwa kwamba mwenendo huu wa utoaji chanjo ukiendelea, tutarudi kwenye mstari,” anasema Meneja wa Msitu wa Magoroto, Jeremiah Mchechu.
Bodaboda ni miongoni mwa watoa huduma wakuu wa usafiri kuelekea Magoroto, msitu uliopata umashuhuri miaka ya hivi karibuni.
Serikali inasema inaendela kuhamasisha wananchi kujihusisha na shuguli za utalii wa ndani ili kufungua milango ya ajira wakiwemo bodaboda na kuinua mapato ya Serikali yanayoweza kuleta maendeleo.
“Tusipopata tozo kutoka kwa vivutio vya utalii kama Magoroto, kasi ya kupeleka huduma kwa wananchi inapungua. Hivyo kama Watanzania ni jukumu letu kujiinua kiuchumi kupitia utalii wa ndani,” anasema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Nassib Mmbagga.
Ripoti ya masuala ya kiuchumi ya Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa mwaka 2021 inasema kukuza utalii wa vijijini na mijini itakuwa moja ya njia zitakazosaidia kuimarisha sekta ya utalii kupitia ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya Serikali.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
