Corona: Wajasiriamali walia kupungua matumizi ya barakoa
- Wafanyabiashara walalamika kushuka kwa biashara ya barakoa.
- Idadi ya wanaovaa nayo yapungua.
- Serikali yasema itaendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi.
Mwanza. Alikuwa miongoni mwa wajasiriamali wa Tanzania waliofadika na janga la Corona (Uviko-19) tangu lililopoingia nchini Machi 2020.
Alitumia fursa ya kutengeneza barakoa za vitambaa kwa wingi na kuuza kwa watu ili wajikinge na ugonjwa huo unaotikisa dunia.
Hata hivyo, hakufikiria kuwa kuna siku atashindwa kabisa kuuza hata barakoa moja kwa sababu aliamini uvaaji wa barakoa ni sehemu ya maisha ya watu wakati huu wa janga hili la Uviko-19.
Ni fundi cherehani katika kata ya Buhunda, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Maulid Fundi ambaye wateja wake wakuu walikuwa wananchi wa kawaida na wachimbaji wadogo wa madini katika migodi miwili ya Busolwa na Chitongo wilayani humo.
Wakati huo, Fundi ambaye anajihusisha na ushonaji wa nguo alikuwa na uwezo kutengeneza na kuuza barakoa zisizopungua 10 kwa siku na hivyo kuwa una uhakika kujipatia Sh10,000 kila siku.
Kiasi hicho cha fedha alichokuwa anapata kilikuwa nje ya mapato yake anayopata kwa kushina nguo za wateja wake zikiwemo suti za wanaume.
Mwanaume huyo mwenye miaka 47 anasema kwa sasa inaweza kupita hata mwezi hajapata mteja wa barakoa na akipata ni wale ambao wanaweka oda ambao nao wananunua chache.
“Unaposema kuwa ugonjwa wa corona umekuwa fursa kwa wajasiriamali wadogo hususan mafundi cherehani, hilo kwangu nakataa tena kwa awamu hii ya wimbi la tatu… Kwangu sijashona hata barakoa 10 na unazoziona hizi tatu ndio oda niliyopokea na ninaziuza buku kwa kila moja, sasa hapo fursa imetokea wapi?” amehoji fundi huyo.
Kupungua kwa matumizi ya barakoa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa husasan wilayani Misungwi kunatokana na imani waliyojingea watu kuwa ugonjwa huo ni kama magonjwa mengine na hivyo hawana sababu ya kuchukua tahadhari.
Fundi cherehani katika kata ya Buhunda, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Maulid Fundi ni miongoni mwa watu waliowekeza katika utengenezaji wa barakoa za kitambaa lakini sasa biashara hiyo imepungua. Picha| Mariam John.
Jambo hilo limewafanya kuacha kuvaa barakoa na hata wanaovaa huzivaa wakati wakienda kupata huduma katika ofisi bila kuvaa kifaa hicho cha kujikinga na Uviko-19 huwezi kuhudumiwa.
Fundi cherehani katika kata ya Buhunda, Wilayani hapa, Ratifa Mashauri anakiri kuwa katika maeneo hayo hakuna fursa tena zinazotokana na ushonaji wa barakoa kwa sababu uvaaji umepungua.
“Eti kusema kwamba tumeshona barakoa nyingi sana zilizotusaidia kukuza uchumi hapana!, ni mara moja moja tena kwa oda labda mtu anayetaka kwenda hospitali,” anasema Ratifa na kubainisha kuwa bei ya barakoa imechuka hadi Sh500.
Elimu kuendelea kutolewa
Viongozi wa eneo hilo akiwemo diwani wa kata ya Buhunda, Luzambya Simuda anasema wanaendelea kutoa elimu huku wakikumbana na changamoto ya uelewa mdogo kwa wakazi wa eneo hilo kuhusu tahadhari dhidi ya Uviko-19.
Simuda anasema bado watu hawaamini kama kuna ugonjwa wa Uviko-19 na kuwa tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo hazichukuliwi kama wataalam wa afya wanavyoelekeza.
“Tunaendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, tunahamasisha watu kunawa mikono na kupaka vitakasa mikono, ” anasema Simuda.
Maulid Fundi akionyesha barakoa ambazo amezishona baada ya kupata oda. Hata hivyo, idadi ya wanaozitumia iko chini katika Wilaya ya Misungwi. Picha| Mariam John.
Licha ya kutoa elimu ya kujikinga, viongozi wa Wilaya ya Misungwi wameendelea kuhamasisha watu kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 ili kujihakikishia usalama wao wakati huu wa wimbi la tatu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Buhunda, Sospeter Balele anasema wananchi wako tayari kupokea chanjo lakini vituo vinavyotoa chanjo hiyo vingesogezwa karibu na wananchi.
“Wapo wananchi walio tayari kupata chanjo lakini kutokana na vituo kuwa mbali wengi wanashindwa kwenda hivyo Serikali ingeona umuhimu wa kusogeza vituo hivyo hususan kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini,” anasema Balele.
Katika wilaya hiyo ya Misungwi jumla ya vituo vitatu vimetengwa kwa ajili ya kutolea chanjo ambapo ni Hospital ya Wilaya ya Misungwi, Kituo cha afya Bukumbi na kituo cha afya Misasi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Dk Clement Morabu amesema wilaya hiyo ilipokea dozi 4,600 za chanjo ambazo zinatolewa katika vituo vitatu na elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi kuchanja na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).