Simulizi ya wanawake wajasiriamali katika kujikwamua na Corona Tanzania
- Baadhi yao wasema bado maumivu ya ugonjwa huo yanawatesa.
- Waiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la tatu.
- Serikali, wadau watoa ushauri kuziimarisha biashara zao.
Arusha. Akiwa amezungukwa na bidhaa za utamaduni na sanaa zikiwemo zilizotengenezwa na shanga katika duka lake, mfanyabiashara huyu anaendelea kukipendezesha kikapu kwa urembo wa shanga huku akitabasamu akiwa na matumaini ya kuwavutia zaidi wateja.
Duka lake ni miongoni mwa maduka takriban 200 yaliyopo katika soko la Maasai linalouza bidhaa hizo katikati ya jiji la Arusha, kaskazini mwa Tanzania.
Hata hivyo, tabasamu alilonalo mfanyabiashara huyo siyo kwa sababu biashara yake inamwendea vizuri bali amerejea katika biashara yake baada ya kufungwa kwa muda kutokana na janga la Corona (Uviko-19).
“Siku za nyuma tulikuwa tunafikiria Watanzania ni wateja wetu tukagundua siyo wateja…lilipotokea tatizo la Corona tulifunga kabisa biashara kwa sababu tulikosa kabisa wateja ndipo tukagundua wateja wetu kwa asilimia 95 ni watalii,” anasema Priskila Roine, mfanyabiashara wa bidhaa za utamaduni na sanaa katika soko la Maasai.
Licha ya kurejea katika biashara yake ambayo anahusika na kushona shanga katika bidhaa mbalimbali ikiwemo vikapu na viatu, bado haijamarika kwa sababu idadi ya watalii wanaotembelea sokoni hapo siyo kubwa ikilinganishwa kabla ya Uviko-19.
Utalii ni miongoni mwa sekta ambazo ziliathiriwa sana na janga hilo ambapo watu wengi walipoteza ajira na wengine kutumbukia katika umaskini uliokithiri.
Hata hivyo, sekta hiyo inatarajia kuimarika tena baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo utoaji wa chanjo na kuanza upya kwa safari za kimataifa zinazohusisha watalii na wafanyabiashara.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) limeeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa ilipungua kwa asilimia 73 kwa mwaka 2020, huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.
Hata hivyo, UNWTO inasema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022, huku Afrika, sekta hiyo ikitarajiwa kuimarika kwa asilimia 73.

‘Mambo bado’
Priskila anasema kwa sasa mambo bado siyo mazuri, wakati mwingine hukaa hata siku tatu bila kuuza chochote kwa sababu wateja siyo wengi kama zamani licha ya shughuli za utalii kurejea jijini humo.
“Wageni wanakuja ila sasa na wao wamepitiwa na hili tatizo ndiyo maana hata wakija hawafanyi shopping (manunuzi) hata wakifanya wanafanya kidogo sana kwa sababu ya hii Corona, walikaa muda mrefu bila kufanya kazi kwa hiyo hawana hela za kutosha,” anasema.
Mama huyo, ambaye mtoto wake alisimama masomo ya chuo kikuu mwaka jana kwa kukosa ada, anasema wakati akisubiri sekta ya utalii iimarike analazimika kutumia soko la ndani ambalo ni dogo kwa kutuma bidhaa kwa wateja wake waliopo katika mikoa mbalimbali nchini.
“Hali ni mbaya sana kwa sababu ni zaidi ya mwaka mpaka sasa hivi bado hatujaweza kuziba mapengo yaliyotokea wakati ule,” anasema.
Ripoti ya utafiti kuhusu usawa wa kijinsia wakati wa janga la Corona ulifanywa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) umeeleza kuwa wanawake wachache kati ya wengi waliopoteza ajira kutokana na athari za janga hilo wataweza kupata kazi nyingine ikilinganishwa na wanaume.
Ripoti inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani sawa na kupoteza ajira milioni 54, wakati wanaume waliathirika kwa asilimia 3 tu au ajira milioni 60. Ikumbukwe kuwa wanaume ni wengi zaidi kuliko wanawake kwenye mfumo wa ajira.
Wanawake wamekuwa waathirika wakubwa katika ajira na kukosa kipato kwa sababu maeneo wanayofanyia kazi ikiwemo sekta ya malazi, chakula, biashara na uzalishaji yameathirika zaidi na janga la Corona.
Selina Francis, mfanyabiashara sokoni hapa anasimulia kipato anachopata kwa sasa kiko chini kwa sababu mwenendo wa biashara siyo wa kuridhisha.
Zinazohusiana:
- Kutana na Aneth David mwanasayansi anayechipukia Tanzania
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
- Esther Mndeme: Muongozaji aliyewashangaza wengi tuzo za filamu 2019
Kutokana na hali ilivyo sasa, amelazimika kumuondoa mtoto wake katika shule ya msingi binafsi na kumpeleka shule ya Serikali ili kupunguza gharama za maisha.
“Kwa sasa tumepanda kidogo (kibiashara) hadi asilimia 30, hapa unaweza kuja wiki nzima hujauza unakuja unafanya usafi unaondoka. Siku nyingine unauza Sh15,000,” anasema Selina ambaye wakati mwingine huuza mifuko mbadala na barakoa ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha.
Wakati wafanyabiashara wa bidhaa za utamaduni na sanaa wakiendelea kuugulia maumivu ya Uviko-19, wenzao katika sekta nyingine hali imeimarika.
Sarah Mollel, mmiliki wa kampuni ya Kabinti Products iliyopo Ilboru jijini hapa anasema kwa sasa biashara yake imesimama na amerejea katika hali ya kawaida kwa sababu bidhaa anazouza zinahitajika kwa wingi na wateja.
Mfumo wa dijitali waokoa wengine
Binti huyo, muhitimu wa shahada ya kwanza kutoka Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) anayeuza bidhaa za lishe ukiwemo unga, mchele na asali, anasema ana uhakika wa kupata kipato na kuwalipa wafanyakazi wake kwa sababu bidhaa zina soko ikilinganishwa na mwaka jana ambapo Corona ilikuwa juu.
Kutokana na athari alizopata wakati wa janga hilo, amelazimika kubadili mfumo wa mauzo na kutumia mifumo ya kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wake ili kuhimili soko la ushindani.
“Kwa sasa kuna ahueni, wateja wanakuja na wengine tunawatumia katika maeneo yao baada ya kuweka oda mtandaoni, hii inanipa ujasiri kuwa nitasimama tena katika biashara yangu ambayo ilitikiswa na Corona,” anasema Sarah.
Kodi bado kitendawili
Selina na Priskila wana matumaini makubwa ya biashara zao kusimama tena kwa sababu wateja wameanza kurejea katika biashara zao lakini wanaiomba Serikali iwapunguzie na kuwarefushia muda wa kulipa kodi kwa sababu hawapati mapato ya uhakika.
Sisi wafanyabiashara wadogo wa utalii ndiyo tumeathirika kuliko watu wote, kwa hiyo tunaiomba Serikali watusimamishie kodi, kwa mfano kama hapa tunadaiwa kodi za maduka, watuondolee kodi ya maliasili, leseni hata miaka miwili mbele tuweze kujipanga kabisa,” anasema Selina akiwa mbele ya duka lake lililosheni vinyago.
Suluhu kwa wanawake wajasiriamali
Wakati huu ambao bado baadhi ya wajasirimali hawajasimama vizuri katika biashara zao, ILO inapendekeza Serikali na mashirika ya kusaidia wanawake kuunda programu maalum ili kuwapatia mitaji na ushauri wa kuendesha biashara wakati wa majanga kama Uviko-19.
Meneja wa kituo atamizi cha Obuntu cha jijini Arusha, John Mushi anasema katika kipindi hiki cha Uviko-19 wamekuwa wakiwasaidia wajasiriamali wadogo namna ya kutumia fedha, kuwa na mipango endelevu ya kuendesha biashara ili waendelee kuwepo katika soko la ushindani.
“Tunatoa mafunzo ya kuwasaidia namna ya kuendesha biashara zao, kubuni mbinu mpya za kujiingizia kipato na kupata mitaji itakayowasaidia kuziimarisha biashara ambazo zimepata changamoto,” anasema Mushi.
Anatoa wito kwa wajasiriamali kuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha kujiingizia kipato ili kuweza kukabiliana na dharura kama ya Corona.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro Oktoba 17 mwaka ilisema wizara yake kwa sasa inatumia Sh90.2 bilioni za mgao wa mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) katika maeneo makuu matano ikiwemo kukarabati na kujenga miundombinu ya utalii ili kukabiliana athari za janga la Corona (Uviko-19) katika sekta hiyo na kuongeza watalii wanaotembelea Tanzania.
Pia inaongeza wigo wa matangazo na kujenga uwezo wa taasisi zake katika kusimamia shughuli zake ili sekta ya utalii iimarike tena na kuanza kuwanufaisha Watanzania waliajiriwa na kujiajiri katika sekta hiyo.
Huenda mikakati hiyo ikawasaidia wajasiriamali wa bidhaa za utamaduni na sanaa ambao bado hawajapona vidonda vya Uviko-19 kurejea tena katika biashara zao.
Latest