Namna ya kubaini tovuti za habari za uzushi kwa kutumia ‘Wayback machine’

November 23, 2020 1:52 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Kupitia teknolojia unaweza kupata habari za zamani ambazo tovuti ilifutwa. 
  • Kumbuka kujiridhisha na ukweli wa habari kabla ya kuisambaza mtandaoni.

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa dijitali, watu wengi wamepata fursa ya kuchapisha habari mtandaoni kiasi cha kuwafikia watu wengi zaidi ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, baadhi ya wanaochapisha habari hizo iwe kwenye mitandao ya kijamii au tovuti huchapisha habari za uzushi. Habari hizo zisizo za kweli kwa sehemu kubwa huandaliwa na watu kwa makusudi kwa lengo mahususi la kuwadanganya au kuwavuruga watu mtandaoni.

Kwa kawaida habari za uzushi nyingi huvutia kiasi cha hata baadhi ya wanahabari dhaifu na vyombo vyao hushawishika kuzichapisha. Miongoni mwa habari za uzushi ambazo huenda zikaaminika zaidi ni zile zinazochapishwa kutoka kwenye tovuti ambazo huiga muundo, rangi na hata majina ya tovuti za vyombo vya habari mashuhuri duniani.

Si watu wote ulimwenguni hususan hapa Tanzania wana elimu ya kukumbuka kila kitu cha vyombo vya habari vinavyoaminika hususan mashirika ya kimataifa. Ili kuepuka kunaswa na tovuti za habari za uzushi kuna mbinu kadhaa za kufanya zikiwemo zifuatazo:-

1.   Jiridhishe na jina la chombo cha habari husika

Iwapo umepokea habari kutoka katika tovuti ya habari, kabla hujaisambaza jiridhishe na jina la chombo husika. Je, hili ni jina jipya? Jina hili linahusiana na chombo chochote kikubwa cha kitaifa ama kimataifa? Iwapo vina uhusiano, je chombo hicho kina kiunganishi au kiliwahi sema chochote kuhusu tovuti hiyo?

2.     Fuatilia historia ya tovuti kwa kuangalia habari zinazoonekana ukurasa wa mbele kwa wakati huo. Je, habari zilizochapishwa zinaonyesha shaka yeyote kuhusu ukweli wake kama takwimu zilizotiwa chumvi kupitiliza? Kukosewa kosewa kwa taarifa za wazi au majina ya watu na miji?

3.      Je, tovuti hiyo ina umri gani tangu ianzishwe? Hapa unaweza kuiperuzi tovuti yote kwa kufungua ukurasa mmoja mmoja na iwapo utashindwa basi yakupasa kutumia maktaba ya mtandaoni inayofahamika kama ‘Wayback machine’.

Maktaba hii www.archive.org inamuwezesha mtumiaji kuona muonekano na habari za miaka ya nyuma hata kama tovuti hizo zilishafutwa.  

Maktaba hii www.archive.org inamuwezesha mtumiaji kuona muonekano na habari za miaka ya nyuma hata kama tovuti hizo zilishafutwa. Picha| BetaNews. 

 

Namna ya kutumia Wayback machine

A)     Ingia kwenye kitafutio (browser) cha simu au kompyuta yako kisha andika www.archive.org au andika wayback machine kwenye Google utaletewa kiunganishi cha maktaba hiyo ya mtandaoni.

B)    Baada ya kufungua tovuti hiyo ya Wayback machine, andika tovuti unayotaka kuhakikisha au kutafuta habari zake za nyuma. Mfano, andika www.nukta.co.tz na kisha bonyeza kitufe cha “Browse history”.

C)    Ukishabonyesha kitufe cha maneno, tovuti hiyo itafungua kalenda maalum inayoihusu. Kwa mfano huo wa tovuti ya Nukta, itafungua kielezo cha miaka ya nyuma huku miaka ambayo tovuti hiyo imekuwa ikiwa na rangi nyeusi wakati mwaka wa wakati huo ukiwa umeainishwa kwa rangi ya njano.

D)     Chini ya kielezo chenye miaka utaona kalenda yenye miezi kuanzia Januari hadi Desemba ikiwa na viduara kwenye baadhi ya siku. Kiduara hicho kinawakilisha siku ambayo sura ya tovuti hiyo iliifadhiwa mtandaoni. Gusa au bonyeza mara mbili kwenye kiduara hicho utapata muda iliporekodiwa na baadaye kiguse au bonyeza mara mbili na tovuti hiyo itafunguka kabisa. Tovuti na habari utakazoletewa ni zile zilizochapisha siku ya tarehe uliichagua.


Soma zaidi:


E)    Kupitia matokeo uliyoyapata kwenye Wayback machine unaweza kuchunguza historia ya uchapishaji wa habari wa tovuti husika ikiwemo kama huwa inachapisha habari za uzushi mara kwa mara.

Ujuzi huu unaweza kukusaidia kung’amua tovuti zinazochapisha habari mbalimbali za uzushi zikiwemo za ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) ambazo zimeendelea kusambaa kwa kasi ulimwenguni.  

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa baadhi ya habari za uzushi huchapishwa na vyombo vya habari vinavyoaminika baada ya kushindwa kuzithibitisha au uharaka wa kuwa wa kwanza mtandaoni.

Wakati wote unapopata shaka kuhusu habari zilizochapishwa kwenye tovuti kuhusu ugonjwa kama Covid-19 jaribu kutafuta taarifa hizo kwenye tovuti za mamlaka kama wizara ya afya nchini Tanzania au Shirika la Afya Duniani (WHO).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW