Mbinu zitakozokusaidia kubaini tovuti feki
- Mara nyingi hutumia vikioa tofauti na tovuti za kweli.
- Hazina maelezo ya kutosha kuhusu taasisi au shirika linalomiliki tovuti.
- Pia huiga muonekano wa tovuti maarufu duniani ili kuwapotosha watu kwa haraka.
Dar es Salaam.Tovuti (website) zimekuwa ni nyenzo muhimu za kidijitali za kupashana habari miongoni mwa watu duniani kwa sababu hazifungwi na mipaka ya jiografia.
Mtu yoyote anayetumia mtandao wa intaneti kwenye simu, tableti au kompyuta naweza kuperuzi na kuvinjari kwenye tovuti za watu, taasisi au mashirika mbalimbali ili kujipatia habari zitakazomsaidia kufanya maamuzi.
Hata hivyo, tovuti imekua ni njia mojawapo inayotumika na watu wasio na nia njema kutoa habari za uzushi kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa virusi vya Corona ili kuibua taharuki kwenye jamii.
Habari za uzushi husambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuleta madhara mbalimbali ya kijamii, kiafya, kiuchumi na hata kisiasa.
Wapotoshaji hao hutumia tovuti halisi na wakati mwingine hutengeneza tovuti feki ambazo hufanana karibu kila kitu na zile za kweli. Unawezaje kuitambua tovuti feki ili kuepuka uzushi hasa kipindi hiki cha janga la Corona?
Vitu vitakavyokusaidia kubaini tovuti feki
Kikoa (domain) ni njia moja wapo ya kugundua tovuti feki kwa urahisi kwa kuwa ndicho ambacho hutumika zaidi katika kutengeneza tovuti za uongo.
Mara nyingi wanaotengeza tovuti feki hufanya badiliko ya kikoa cha tovuti halisi na ikiwa mtu akikosa umakini anaweza kuiamini tovuti na kutumia maudhui yaliyowekwa.
Mfano tovuti ya Nukta Habari (www.nukta.co.tz) inaweza ikachezewa na ikapatikana tovuti nyingine ambayo inafanana na tovuti hiyo kwa kuibadilishia kikoa, mfano ikaitwa nukta.co.com au nukta.co.
Kwa sababu Nukta imekua ikichapisha habari za COVID-19, ni rahisi kwa watu kuamini na hivyo kupata madhara. Ili kuepuka mtego huo, ni vema ukafanya ilinganifu wa vikoa ili kujiridhisha kama ni sahihi.
Zinazohusiana:
Sehemu nyingine ya kubaini kama tovuti ni feki ama la ni kwenye sehemu ya taarifa za msingi za kampuni au taasisi (About Us) . Kama tovuti ni ya kweli, utakutana na taarifa zilizojitoshereza za taasisi husika ikiwemo uanzishwaji wake, umiliki na hata inafanya jambo gani.
Lakini tovuti feki mara nyingi huwa hazina maelezo hayo au maelezo yake yanakuwa hayajitoshelezi. Kama ukipata mashaka na kipengele cha ‘About us’, basi inaweza kuwa kiashiria cha kuwa tovuti unayofuatilia ni feki.
Chapa au nembo (logo) ya tovuti ni jambo lingine ambalo mtu anatakiwa kuwa nalo makini kwa kuwa ni kitu kinachotumika pia katika kutengeza tovuti feki.
Wanaotengeza tovuti feki kuna wakati wanatumia mbinu hii kwa kuweka logo maarufu ya tovuti kama ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kwenye tovuti nyingine kabisa ambayo wanaitumia kusambaza habari za uzushi.
Wanafanya hivyo ili kuwaminisha watu kwa haraka kutokana na ukweli kuwa BBC ni miongoni mwa vyombo vya habari vinavyoheshimika duniani.
Kabla ya kutumia au kusambaza habari za COVID-19 ambayo tovuti yake unaitilia mashaka, jipe muda kwanza wa kuhakiki kama ni ya kweli au imetengenezwa kwa ajili ya kupotosha.
Latest
