Jinsi kuthibitisha habari kwa kutumia takwimu
- Ni lazima katika kuthibitisha takwimu ufahamu chanzo cha takwimu hizo.
- Lazima kuuliza maswali ya msingi kuhusu takwimu hizo.
- Takwimu zinazopotosha huleta madhara ya kijamii hata ya kiuchumi
Dar es Salaam. Licha ya takwimu kutumika kwa ajili ya kufanya maamuzi kwa manufaa ya taasisi au wananchi lakini katika siku za hivi karibuni pia watu wasio na nia njema wemekuwa wanatumia takwimu kusambaza habari za uzushi mtandaoni.
Takwimu hizo zinazopotosha zimekua zikitumika hasa katika majanga makubwa yanayoikumba dunia kama Corona ili kuzua taharuki na kujipatia faida isivyo halali.
Lakini hakuna lisilowezekana, takwimu kutoka vyanzo vya uhakika, pia ni nyenzo muhimu ya kupambana na habari za uzushi
Jinsi ya kutumia takwimu kupambana na habari za uzushi
Chanzo cha takwimu (Source) ni jambo la kwanza la msingi katika kuthibitisha habari za uzushi zinazotumia takwimu. Pale unapokutana na takwimu zozote ama katika mitandao ya kijamii au vyombo vya habari ni lazima muhusika eleze chanzo cha takwimu hizo amezitoa wapi na unapaswa kufahamu kama zimetoka katika vyanzo sahihi.
Kuna wakati wanaozalisha habari za uzushi kwa kutumia takwimu wanataja vyanzo vya takwimu hivyo na wakati mwingine hawavitaji jambo la msingi linalotakiwa ni wewe kama mwanahabari au msomaji kufahamu chanzo za takwimu hizo kama ni za kweli.
Zinazohusiana:
Kujiuliza maswali magumu au ya msingi kuhusu takwimu hizo. Kwa kila takwimu inayotajwa hasa unayotilia mashaka, ipime kama ina ukweli kabla ya kusambaza kwa watu.
Mfano, katika siku za nyuma zilisambazwa taarifa mtandaoni zinazosema jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na mabikira wengi Tanzania. Kwa hali ya kawaida takwimu hizi zinazua maswali mengi hasa njia iliyotumika kukusanya data na kutoa matokeo. Njia hizo zinatumika maeneo mengine duniani?
Jambo lingine la msingi katika kuangalia takwimu ni lazima ufahamu takwimu hizo zinachapishwaje au zinatolewa kwa muda gani. Mfano takwimu za Sensa ya Watu na Makazi huchapishwa kila baada ya miaka 12 na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2012.
Wakati unajaribu kuzithitisha takwimu husika jambo la msingi ni kufahamu pia uzalishaji wa hizo takwimu huwa kwa kipindi cha muda gani. Hii itakusaidia kuepuka uzushi
Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kabla ya kusambaza habari yoyote katika mitandao ya kijamii ikiwemo wakati huu wa janga la ugonjwa wa COVID-19 ambayo takwimu zake unazitilia mashaka, jipe muda kwanza wa kuhakiki kama ni ya kweli au imetengenezwa kwa ajili ya kupotosha.
Latest