Mwelekeo mpya sekta ya utalii Tanzania
- Kuimarisha uhifadhi na vivutio vya utalii.
- Serikali kuongeza kasi ya kuwahudumia wawekezaji.
Dar es Salaam. Huenda sekta ya utalii Tanzania ikapata msukumo mpya kutoka katika athari za janga la Corona (Uviko-19) mwaka mmoja uliopita baada ya Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa vibali na leseni za uwekezaji.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa sekta ya utalii pamoja na kuendelea kuboresha huduma za kitalii ikiwemo upatikanaji wa leseni ya shughuli za utalii kwa haraka pamoja na mifumo ya malazi.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoa fursa katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi.
“Sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii, falsafa yetu ni moja tu, mteja ni mfalme. Ndiyo maana mimi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, tuko tayari kukutana na mwekezaji wa aina yoyote yule, muda wowote ule kujadili changamoto zozote zile, milango iko wazi,” amesema.
Dk Ndumbaro amesema hayo leo Machi 31, 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akikabidhi vyeti kwa wawekezaji waliokidhi vigezo na kufanikiwa kupata maeneo ya uwekezaji mahiri katika maeneo ya wanyamapori (SWICA), yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambao ni kampuni mbili za Grumet Services Ltd pamoja na Mwiba Holding ltd.
Amewasisitiza wawekezaji wazawa pamoja na wa kigeni kulinda na kutangaza utalii na maeneo ya uhifadhi na vivutio hapa nchini, katika maeneo waliyopewa kuwekeza kwa kushirikiana na Serikali.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Majaliwa aanika faida za chaneli mpya ya safari Tanzania
Pia Waziri Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini, akiitaja Tanzania kuwa ni salama yenye amani na demokrasia na kwamba wizara anayoiongoza imefungua milango kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vyeti hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Grumeti Reserves Ltd, Graham Ledger amesema kampuni ya Grumeti inashukuru kupata cheti cha umiliki wa vitalu viwili kwa sasa na inaahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kulinda na kuendeleza shughuli za uhifadhi nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwiba Holding ltd., Mark Ghaui ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinaleta tija kwa Taifa kwa kuhakikisha unaimarika kwa kuleta faida ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi kwa kupitia uwekezaji huo wa muda mrefu.
Latest
