Bajeti Kuu ya Serikali: Wapendekeza msamaha wa kodi kwa wenye kipato cha chini

February 2, 2022 6:03 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mjumbe wa Chama cha watoa Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) kutoka Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, Hilda Bujiku, akichangia hoja wakati wa Mkutano kati yao na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba (hayupo pichani), jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.


  • Wadau wa mawasiliano waiomba Serikali itoze kodi kampuni kubwa.
  • Washauri Serikali iongeze wigo wa kodi kwenye huduma kidijitali.
  • Serikali yasema itayafanyia kazi mapendekezo hayo.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya bajeti kuu ya mwaka 2022/23, Chama cha Watoa Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) kimewasilisha maoni yake kuhusu sera za kodi ili kuiwezesha Serikali kuongeza mapato na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

TAMNOA imesema kuwa mapendekezo waliyoyatoa yakifanyiwa kazi na kuanza utekelezaji wake mapato ya Serikali yataongezeka kutoka asilimia 61 hadi asilimia 64.9.

Miongoni mwa maoni yaliyotolewa ni kutoza kodi maeneo yenye kipato kikubwa na kutoa msamaha wa kodi kwa wale wenye kipato kidogo ili kupunguza pengo la walio nacho na wasio nacho.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa Februari 1, 2022 jijini Dodoma wakati ujumbe wa TAMNOA ulipokutana na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Lameck Nchemba ambaye amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara yatakayoiwezesha sekta binafsi kukua na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Sekta binafsi ikinawiri na Serikali inanawiri! Kwa sababu sekta binafsi ndiyo injini ya kuwezesha ukuaji wa uchumi wetu, kwa hiyo niwashukuru kwa maoni mliyotoa”, alisema Dk Nchemba.

Amesema wizara imepokea maoni hayo na itasimamia utekelezaji wake ili kuangalia mianya mipya ya kutoza kodi hususani kampuni kubwa duniani zinazofanya biashara kwa njia ya kidijitali kwa kuweka sheria ili kodi hizo ziweze kutumika kutoa huduma kwa wananchi.


Soma zaidi: 


Aidha, Dk Nchemba amewaelekeza wataalamu wa wizara hiyo kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia mapendekezo yaliyotolewa na wadau hao ili kuona namna bora ya kuyatumia ili yalete tija.

Wadau wengine ikiwemo sekta binafsi wameombwa kuwasilisha mapendekezo na maoni yao mapema kuelekea maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 ili kuwa na sera za kikodi rafiki kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya nchi.

Mapendekezo kutoka sekta binafsi ni muhimu katika kusaidia maboresho ya sera za kiuchumi na sera za kikodi ili kujenga mazingira rafiki kwa sekta binafsi nchini.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema kuwa mawazo yaliyotolewa na wadau ni mazuri na kuwa Serikali imeyachukua na yatafanyiwa kazi na kuiomba Wizara ya Fedha kuchambua maoni hayo mapema na kuwashirikisha wadau kuhusu maamuzi yatakayofikiwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Jamal Kassim Ali amesema kuwa suala la kuangalia namna ya kuzitoza kodi kampuni kubwa duniani zinazofanya biashara kwa njia ya mtandao ni muhimu kwa kuwa yanakusanya fedha nyingi kutoka kwa wananchi lakini haziachi chochote kwa ajili ya maendeleo yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW