Tamasha la ‘Urithi Festival’ kufanyika mikoani kila mwaka

Rodgers George 0527Hrs   Agosti 27, 2018 Habari
  • Tamasha la mwaka huu kufungua milango zaidi kwa watalii kuja nchini.
  • Serikali iko mbioni kulipeleka tamasha hilo mikoa yote kila mwaka.
  • Urithi na utamaduni wa mtanzania kutangazwa kimataifa.

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika kwa tamasha la ‘Urithi Festival’ Jijini Dodoma, Serikali inakusudia kufanya tamasha hilo kila mwaka katika mikoa yote siku zijazo ili kukuza  shughuli za utalii nchini.

Tamasha hilo litazinduliwa na Rais John Magufuli  Septemba mosi mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Square ambapo linalenga kuenzi na kutangaza utamaduni wa kitanzania duniani. 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devotha Mdachi amesema Serikali iko kwenye mipango kuhakikisha tamasha la ‘Urithi Festival’ linafanyika katika mikoa yote kila mwaka ili kuchochea shughuli za utalii na kukuza Pato la Taifa. 

“Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu lakini litakua linafanyika kila mwaka. Hatukuweza kuanza na mikoa yote kwa sababu ya gharama na inahitaji muda kujipanga. Nia yetu baadaye maadhimisho haya yawe yanafanyika mikoa yote” amesema Mdachi.

Amebainisha kuwa kwa mwaka huu wa 2018 mikoa minne ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na visiwa vya Zanzibar vimepata fursa ya kuendesha tamasha hilo chini ya TTB ambapo litafungua fursa kwa makampuni ya utalii ya ndani na nje kunufaika na fursa zitakazojitokeza katika kipindi chote cha tamasha hilo.   

Ufanisi wa tamasha la mwaka huu, utatoa tathmini na mipango ya kulipeleka katika mikoa yote nchini ili kuibua vivutio vya kitamaduni vinavypatikana na katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Utalii wa Tanzania sio tu wanyama kuna vitu vingi moja vitu hivyo ambavyo tulikua hatutangazi kwa ukubwa ni suala la utamaduni kwahiyo tamasha hilo litatumika kama jukwaa la kutangaza utalii wa tanzania na kuvutia watalii,” amesema Mdachi.  

Mavazi ya asili ni kivutio kikubwa kwa watalii wa kimataifa kuja Tanzania. Picha| Tanzania Expiditions

Uzinduzi rasmi utafanyika jijini Dodoma kwasababu ndiyo makao makuu ya nchi ambapo litafungwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan  katika Jiji la Arusha Septemba misi mwaka huu ambako ndiyo kitovu cha shughuli za utalii nchini. 

Katika jiji la Dodoma litafanyika kwa siku nane (Septemba 1 hadi 8) kisha litapelekwa Zanzibar na Dar es Salaam (Septemba 9-16). Septema 17 hadi 23 litafanyika Jijini Mwanza kabla ya kufikia kilele chake katika Jiji la Arusha kati ya Septemba 24 na 25. 

Shughuli zitakazofanyika katika tamasha hilo ni ngoma na muziki wa asili, mapishi ya vyakula vya kitanzania, maonyesho ya zana za utamaduni na vivutio vingine vya utalii.

Katika hatua nyingine, Mdachi amesema TTB imeanzisha kitengo maalum cha utalii wa mikutano ambapo kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arsha (AICC) wataendesha utalii huo ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa. 

“Kazi yetu ni kwenda kwenye hiyo mikutano na maonyesho ya utalii wa mikutano na kushindana nan chi nyingine kuweza kuwavutia hao waandaaji wan chi nyingine” amesema Mdachi. 


Related Post