Mikutano ilivyowazimisha viongozi wa ‘wasusa, twala’ Tanga

May 17, 2022 12:47 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Mikutano ya kijiji sasa yachochea maendeleo katika vijiji vingi vya wilaya ya Pangani.
  • Pamoja na hamasa, ushiriki wa vijana kwenye mikutano ya kijiji bado tatizo.
  • Wanawake waongoza kwenye mikutano wanaume wakiburuza mkia.

Pangani, Tanga. Baada ya kumalizika Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 uhusiano baadhi ya wananchi na viongozi haukuwa vyema. 

Viongozi wapya waliochaguliwa katika kijiji cha Msaraza wilayani Pangani walijikuta wakikosa ushirikiano ipasavyo kutoka kwa wakazi wa maeneo yao ambao baadhi walikuwa wakisononekea matokeo ya uchaguzi. 

Baadhi waliona waliochaguliwa walishinda kihalali na wengine waliona hawakushinda kihalali huku kauli za baadhi za viongozi zikiichefua sehemu ya wanakijiji.

“Hapa kijijini kwetu kulikuwa na uhusiano mbovu kati ya wananchi na wanakijiji uliofanya wananchi wasusie mikutano na wasusie shughuli mbalimbali za kimaendeleo,” anasema Bibie Mohammed mkazi wa Kijiji cha Msaraza.

‘Mwasusa, sisi twala’

 “Viongozi nao wakawaambia kama mwasusa, sisi twala,” anaongeza.

Ili kurudisha imani ya wananchi katika kushiriki mikutano ya kijiji iliwalazimu baadhi ya wakazi kujitoa na kuwaelimisha wengine juu ya umuhimu wa mikusanyiko hiyo katika ukuzaji wa uwazi na uwajibikaji. 

Tofauti na maeneo mengine Tanzania, Kijiji hiki cha Msaraza kina kamati ya wananchi ambayo ni tofauti na zile kamati rasmi za Serikali za mitaa. 

Kamati hii ya wananchi iliundwa baada ya kuwepo baadhi ya wananchi vinara waliopewa mafunzo juu ya kuibua na kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii husika ambayo huitwa uraghbishi. 

Baada ya mgogoro mrefu, kamati ya wananchi inayomhusisha Bibie ilimwomba mwenyekiti wa kijiji chao kuitisha mkutano na wajumbe wa halmashauri ya kijiji ili wazungumze kwa pamoja na kutatua tofauti zao.

Kwa mujibu wa Bibie, mwenyekiti wao alikiri kuwa hakuwa na lugha nzuri zilizozorotesha uhusiano na wananchi wake na baada ya maafikiano alilizimika kuitisha mkutano wa kijiji kwa ajili ya kuomba radhi. 

“Baada ya mwenyekiti kuitisha mkutano wa kijiji ambapo kamati ya wananchi iliomba radhi kwa niaba ya viongozi wa vijiji na yeye mwenyekiti kuomba radhi. 

“Tulianza kuona mabadiliko, wananchi walikuwa na utayari wa kushiriki mikutano ya hadhara…awali walikuwa wananchi 40 au 50 lakini baada ya hapo tulifikia103 katika mikutano ya kijiji,” anasema Bibie. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msaraza hakupatikana kwa haraka kuzungumzia undani wa mgogoro huo. 

Tatizo la maeneo mengi

Hali hiyo haikuwa Msaraza pekee bali sehemu nyingi za vijiji vya wilaya hii iliyopo kando kando mwa Bahari ya Hindi. 

Ally Hamis, mkazi wa Kijiji cha Pangani Mashariki anasema yeye ni miongoni mwa watu ambao awali walikuwa hawashiriki mikutano ya kijiji baada ya uchaguzi kwa kuwa hakuridhika na waliochaguliwa. 

“Mimi mwenyewe nilikuwa sishiriki mikutano na nilikuwa mwaribifu hasa…tulikuwa tunapitiana na kuelezana kuwa tusiende kwenye mikutano, tuwaache wenyewe wafanye,” anasema Hamis. 

Baadhi ya wananchi wa Pangani mkoani Tanga wakishiriki moja ya mkutano wa kijiji ili kujadili mipango ya maendeleo. Picha| Benezeth Kahwa.

Hamis anasema alipata hamasa ya kuanza kushiriki mikutano ya kijiji baada ya mkuu wa wilaya ya Pangani kuitisha mkutano wa vyama vyote vya siasa, kujadiliana na wananchi na kutatua jambo hilo. 

“Napenda sana mikutano kwa sababu ninawiwa na mambo ya maendeleo ya kijiji, kata mpaka wilaya kwa sababu nina maono yangu yakichujwa na kufanyiwa kazi vizuri yanaweza kuleta tija,” anasema Hamis huku akibainisha kuwa mikutano inamsaidia sana kufahamu yanayoendelea na kutatua matatizo kwenye vijiji vyao. 

Vijana wapo nyuma kama mkia wa kondoo

Pamoja na wananchi wengi kuhamasishwa kwenda kwenye mikutano, bado kundi la vijana halijitokezi vema ikilinganishwa na idadi yao katika maeneo mengi ya vijiji vya wilaya ya Pangani. 

Asia Clement (23), Mraghbishi wa Kijiji cha Msaraza anasema kuwa awali mwitikio wa vijana ulikuwa chini zaidi jambo lililowafanya kupita mitaani na kwenye vijiwe mara kwa mara kutoa elimu ya umuhimu wa kushiriki kwenye mikutano. 

“Kwa sasa kidogo hali inaridhisha tofauti na mwanzo. Tangu tulivyoanza kutoa elimu saa hivi vijana wanafika kwenye mikutano,” anasema Asia huku akieleza kuwa asili ya shughuli nyingi za vijana kama bodaboda zinawafanya wasipatikane mara kwa mara. 

Asia, ambaye amekuwa akifanya kazi ya uraghbishi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, anasema ni wakati kwa vijana kushiriki kikamilifu katika mikutano kwa sababu kutoshiriki kunafanya wasifahamu masuala mengi ya maendeleo. 


Soma zaidi: 


Nuru yaanza kuonekana

Mwitiko wa wananchi hawa kwenye mikutano angalau kunawatia moyo wadau wa maendeleo ikilinganishwa na awali ikiwemo mikutano ya dharura. 

“Mkutano wa leo ulikuwa wa dharura na ulilenga kuweka majina ya barabara na mitaa na namba za kwenye nyumba, mbiu ilipigwa jana na watu wengi wamejitokeza sana zamani usingewaona hawa,” Grace Francis, mkazi wa Kijiji cha Bushiri na mhamasishaji masuala ya kijamii.  

Grace, ambaye tulikutana naye wakati akitoka kwenye mkutano uliokuwa unafanyika katika kijiji chao, anasema wanaendelea kuwahamasisha wakazi wenzao kushiriki zaidi kwenye mikutano ikiwemo kuweka faini kwa wasiofika mara kwa mara. 

 “Mwanzo walikuwa hawahudhurii mkutano walikuwa wanakaa na vitu moyoni lakini sasa wakienda kwenye mikutano wanaibua kero kama migogoro ya mashamba,” anasema Grace huku akibainisha kuwa “wananchi hawawaogopi wanatoa kero zao.” 

                     

Mikutano yatatua kero sugu

Katika mikutano mingi inayofanyika katika vijiji hivi wanawake hujitokeza zaidi kuliko wanaume jambo ambalo baadhi wanasema linatokana na asili ya shughuli za kiuchumi za wanaume hao.  

Grace anasema wanaume wachache huudhuria mikutano kwa sababu kero nyingi kwenye jamii zinahusisha zaidi wanawake na wanaume wengine hawana uelewa wa umuhimu wa kushiriki mikutano hiyo. 

Mikutano ya vijiji imesaidia maendeleo makubwa katika wilaya hii iliyopo mkoani Tanga. 

Katika Kijiji cha Mwera, Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwera, Omari Shehe anasema imesaidia kupunguza utoro baada ya wazazi kufanya mkutano na kuwadhibiti wazazi wenye watoto watoro ikiwemo kuwawekea faini. 

Mbali na kudhibiti utoro, mikutano hiyo ilichochea mijadala mbalimbali ikiwemo wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya kuwawezesha watoto kupata chakula shuleni katika baadhi ya vijiji kama Mwera na Bushiri.  


Tangazo:


Ushiriki wa wananchi si michango

Mwinyimkuu Sultan, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bushiri anasema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuleta maendeleo nchini na watu wanapaswa kufahamu ushiriki si lazima ihusishe michango bali hata mawazo yao yanahitajika.

Sultan, anayekiri kuwa katika baadhi ya vijiji kulikuwa na uhusiano mbovu na wananchi, anasema wananchi huibua shughuli za maendeleo na namna ya kuweza kufikia malengo yao.

“Waliopo nyumbani huwa wanaendelea kulalamika kwa sababu hawajui kinachoendelea…ili tusifikie huko wafike kwenye mikutano, inawezekana wao waliopo nyumbani wana mawazo mazuri kuliko yetu, waje tupate mawazo yao, tupange pamoja, tufanye maamuzi pamoja,” anasema Sultan. 

Sultan anasema hufanya kazi na kamati za wananchi vizuri jambo wapo baadhi ya viongozi wanashindwa kufanya nazo kazi kwa sababu zinahamasisha uwajibikaji kwa kufuatilia jambo mara kwa mara. 

Uongozi wa halmashauri ya Pangani unasema kuwa uwepo wa wananchi wanaohamasisha wenzao kushiriki katika mikutano unasaidia kuchochea maendeleo nchini. 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Pangani, Hassan Nyange aliwaeleza wakazi wa mji huo wawe na utaratibu wa mazungumzo ya mara kwa mara na viongozi wao wakiwemo wenyeviti wa vijiji, watendaji na madiwani kutatua matatizo yanayowakabili. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Nukta TV

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV