Asia Clement: Mbegu ya mabadiliko inayohamasisha uwajibikaji vijijini Tanzania

May 18, 2022 10:51 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Binti amekuwa akijitolea kuwahamasisha wanakijiji wenzie kuibua, kuchambua na kutatua changamoto zinazowakabili.
  • Wataalamu wasema mbinu hiyo inasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji.
  • Baadhi wamkwepa kwa kuwa anawafuatilia kiasi cha kumuona mnoko.

Pangani, Tanga. Licha ya kuwa na majukumu lukuki ya kijasiriamali, Asia Clement (23) hulazimika kutenga angalau siku moja kwa ajili ya masuala ya kijamii. 

Binti huyo, anayeishi kijiji cha Msaraza wilayani Pangani, Tanga na baadhi ya wakazi wengine ni miongoni mwa wanaotoa elimu kwa wananchi wenzao kushiriki shughuli za kimaendeleo kwa kuibua na kutatua matatizo yanayowakabili. 

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa amekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya wananchi inayohamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo katika wilaya ya hii ya kaskazini mwa Tanzania. 

Mafanikio ya jasho

“Najivunia kutoa elimu kwa wanajamii kushiriki katika masuala yanahusu kijiji chao. Hadi sasa najivunia kuchangia kutatua mgogoro wa wananchi na viongozi na kuhamasisha wazazi kuchangia chakula cha shule,” anasema huku akionyesha kuridhishwa na jitihada anazofanya. 

Katika kundi la waraghbishi waliokuwa wamekutana Pangani kutathmini kazi zao, Asia ni mmoja ya mabinti wachache hapa anayeonekana kuwa na ushawishi zaidi. 

Wazee katika mkutano huo na watu wa makamu wanamsikiliza huku baadhi wakitikisa vichwa juu na chini anapokuwa anatoa maoni yake na mrejesho wa kazi ambazo walikuwa wakifanya katika kijiji chao. 

Asia aliyeva gauni nyekundu akiwa katika moja ya mikutano ya kijiji. Binti huyo amekuwa ni hamasa kubwa kwa vijana kushiriki katika mikutano ya vijiji ili kuchagiza ajenda za maendeleo. Picha| Benezeth Kahwa.

Kazi ya bure

Kazi anayofanya Asia haina malipo. Anahitaji kutumia fedha zake wakati mwingine kugharamia shughuli za kuelimisha wanakijiji wenzie. 

Mbali na kutumia fedha zake pale inapohitajika, binti huyo hulazimika wakati mwingine kuahirisha kazi zake za ushonaji nguo ili aweze kuhudhuria vikao vya dharura vinavyotokea. 

Kamati yao ya wananchi yenye takriban mwaka mmoja sasa inafanya kazi kwa karibu na uongozi wa kijiji chao kwa kuwa inawasaidia viongozi hao kuwafikia wanakijiji kirahisi kuibua, kujadili na kutatua matatizo yao. 

‘Hakuna kijana anayetaka kufanya kazi isiyolipa’

Si rahisi kwa vijana wengi kupoteza muda wao kwa ajili kazi za kijamii ambazo huenda zisimuingizie kipato siku za mbeleni. 

“Kazi hii inahitaji imani na uvumilivu zaidi kwa sababu ni suala la kujitolea,” anasema Asia. 

“Unatumia muda wako mwingi kutafuta changamoto ya mtu na unatumia muda mwingi kwenye vikao. Ile yote ni utayari kwa kuwa umeliona lile tatizo kama lako ndiyo maana utatafuta suluhu,” anaongeza huku akitabasamu. 


Soma zaidi: 


Kinachompa nguvu kuendelea kujitolea, Asia anasema ni imani yake kuwa ukisaidia wengine kupiga hatua kimaendeleo unakuwa umejisaidia nawe pia. 

‘Lazima uwe tayari’

“Lazima uwe tayari kuwa chachu ya mabadiliko,” anasema. 

Ni adimu kuona vijana kama Asia akiambatana na wazee kuitisha vikao vya kujadili changamoto za vijiji vyao. 

Binti huyo na wanakamati wenzao kuna wakati huzunguka kaya hadi kaya kuhamasisha watu kuhudhuria mikutano ya kijiji na kuibua hoja au kushiriki katika shughuli fulani za kimaendeleo katika eneo lao. 

Katika harakati hizo, ni vijana wachache hujitokeza hususan wanawake. 

Miongoni mwa sababu zinawakwamisha vijana ni uelewa duni wa umuhimu wa kushiriki mikutano, kuhoji au kuibua suluhu za matatizo yanayowakabili katika jamii yao. 

“Vijana wengi tumekuwa wavivu wa kufuatilia maendeleo ya kijiji au maendeleo kwa ujumla, iwapo unajua lengo lako ni nini utaweza kujitolea bila kutegemea kulipwa,” anasema Asia. 

Kazi, kujitolea, kazi

Katika utekelezaji wa shughuli za uraghbishi, Asia hulazimika kupanga muda wake kwa ajili ya kazi zake za ushonaji na za kutoa elimu. 

“Hili ni suala la kujitolea muda, unapanga muda gani ufanye kazi za kujiingizia kipato na muda gani uende kwenye masuala ya kijamii, wasitafute sababu,” anasema Asia akieleza vijana wengi wa kiume wanajishughulisha zaidi na bodaboda kiasi cha kutopatikana mara kwa mara kijijini kwao. 

Wadau wa maendeleo wanasema jamii ya sasa hususan maeneo ya vijijini inahitaji wananchi kama Asia wanaoweza kuwaelimisha wengine ili kuhamisha maarifa chanya kwa wengine.

                       

Uraghbishi utaiinua Tanzania

Mkufunzi wa Uraghbishi, Rukia Masanyika anasema mbinu ya uraghbishi ni njia muhimu ya kukuza ushiriki, uwazi na uwajibikaji nchini Tanzania kwa kuwa inambadilisha mtu tabia na mwenendo wake unaohitajika kwenye jamii. 

“Tunaiwezesha jamii kuibua masuala yao na mraghbishi anavyoenda kwenye jamii anakuwa hana ajenda bali anaichokoza iweze kuibua, kuchambua na watafute ufumbuzi…wanashriki kwa hiari na si kwa kulazimishwa,” anasema Masanyika.  

Mtaalamu huyo anasema uraghbishi na ushiriki ni pande mbili za sarafu bila mmoja wapo hakuna kinachotokea na watu wanavyosisitizwa kushiriki na watu kama Asia haimaanishi watatakiwa kutoa michango kila mara. 

Uongozi wa kata anayoishi Asia na wenzie unafurahia matunda ya kazi ya binti huyu kwa kuwa inawarahisishia kufikia malengo hasa ya kuhamasisha ushiriki katika shughuli za maendeleo.


Tangazo:


‘Viongozi waingia mitini’

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bushiri, Mwinyimkuu Sultan ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa tangu wajitokeze wakazi wa kijiji chake wenye hamasa ya kuhamasisha wengine kushiriki maendeleo kuna mafanikio makubwa.

“Kamati za wananchi tunafanya nao kazi vizuri lakini kuna baadhi ya viongozi huwa inawawia vigumu kufanya nao kazi… wanafuatilia jambo kujua viongozi ambao wapo kwenye nafasi wamechukua hatua gani kutatua hilo jambo,” anasema Sultan. 

Kiongozi huyo wa Serikali anasema wajumbe wa kamati ya jamii hususan waraghbishi kama Asia wamepewa mafunzo stahiki, ni wadadisi na wanafuatilia masuala ya maendeleo kwa karibu. 

Kama hujachukua hatua, anasema wanakufuata mara kwa mara jambo linalofanya baadhi ya viongozi waone kero na kuwaona waraghbishi ni wanoko. 

“Mimi kwangu nafurahia kwa sababu wananikumbusha kwa hiyo na kuwa na mtu wa karibu kunikumbusha mara kwa mara. Mimi napenda namna wanavyofanya kazi na kunikumbusha,” anasema Sultan. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV