Utafiti ulivyowaumbua viongozi wakwepa uwajibikaji Maswa

April 6, 2022 5:38 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mkazi mmoja tu kati ya 10 wilayani Maswa huwasiliana na kukutana na diwani wake.
  • Baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wanatuhumiwa kufanya upendeleo kwa baadhi ya watu.
  • Serikali yawataka viongozi wa serikali za mitaa kushughulikia matatizo ya wananchi.
  • Wadau washauri wanawake kupewa kipaumbele kwenye mikutano.

Maswa. Stephen Dwese, Diwani wa Kata ya Ng’wigwa wilayani Maswa bado haamini kuwa kuna viongozi wengi hasa madiwani katika eneo lao ambao hawawasiliani ipasavyo na wananchi wao. 

“Kwa ninachoona isingeweza kusomeka kuwa mtu mmoja kati ya 10 ndiye anawasiliana na viongozi (madiwani) angalau basi iwe katikati au hiyo tisa iwe mawasiliano halafu moja iwe ambao hawawasiliani na diwani,” anasema diwani huyo.  

Sintofahamu ya diwani huyo inakuja baada ya matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Twaweza Afrika Mashariki kwa kushirikiana na asasi ya kiraia ya Kasodefo kati ya Machi na Aprili 2021 kubainisha kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu hawapati fursa ya kuwasiliana na kukutana na viongozi wao. 

Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa Februari 22, 2022 yanabainisha kuwa wananchi wa Maswa wana uwezekano mkubwa wa kukutana au kuwasiliana na viongozi wa vijiji kuliko wabunge au watendaji wa kata. 

Utafiti huo unaeleza kuwa asilimia 87 au wakazi tisa kati ya 10 wanasema hawajawahi kukutana na kuzungumza na diwani wao ambaye ni moja ya watu muhimu katika kufanya uamuzi na kuleta maendeleo katika serikali za mitaa.  

“Kuna sehemu unaweza kukuta kuna uzembe fulani wa kiongozi ‘especially’ (hasa) kwa diwani hiyo inaweza kutokea lakini kwa jinsi ninavyofahamu si kweli kwa ujumla kwa sababu sisi waheshimiwa madiwani kazi yetu ni kufanya mawasiliano kwenye kata zetu,” anasema Dwese. 

Diwani huyo anasema kuwa madiwani hufanya mawasiliano na wapiga kura wao kwa njia mbalimbali vikiwemo vikao vya ndani na vya nje, mikutano mikuu na ile ya kawaida.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa utafiti wa “Wasemavyo Wanamaswa: Ushiriki wa wananchi, utoaji wa huduma za jamii na uwezo wa serikali za mitaa” wilayani Maswa, Mkoa wa Simiyu Februari 22, 2022. Picha| Twaweza.

Hata hivyo, hali ni mbaya zaidi katika fursa ya wananchi kukutana na kuzungumza na mbunge wao baada ya matokeo ya utafiti huo kuonyesha kuwa asilimia 94 hawajawahi kufanya hivyo. 

Ni wakazi sita tu kati ya 100 ndiyo angalau waliwahi kukutana na kuzungumza na mwakilishi wao bungeni. 

Pamoja na kubainisha viongozi kutowajibika ipasavyo, matokeo ya utafiti huo yanaonyesha pia wananchi wapo nyuma katika masuala ya mikutano jambo linalorudisha ushiriki wao katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao. 

Utafiti huo unabainisha kuwa takriban wakazi saba kati ya 10 au asilimia 65 wilayani Maswa hawafahamu kuwa hata mkutano mmoja wa kijiji ulifanyika mwaka uliopita.

Hata hivyo, kati ya wakazi 10 wanaojua mikutano hiyo ni wanane tu ambao walihudhuria huku Mkurugenzi wa Utafiti na Kujifunza wa Twaweza Baruani Mshale akisema mahojiano ya kina yalibainisha kuwa uhudhuriaji wa mikutano hiyo ulikuwa chini zaidi ya kiwango hicho. 

Mshale anasema miongoni mwa sababu zinazofanya ushiriki mdogo kwenye mikutano kwa mujibu wa utafiti huo ni pamoja na viongozi kutumia lugha za kuudhi na mashinikizo kutetea ajenda zao. 

Sababu nyingine zilizoainishwa na utafiti huo unaoitwa “Wasemavyo Wanamaswa: Ushiriki wa wananchi, utoaji wa huduma za jamii na uwezo wa serikali za mitaa” ni kuwa viongozi wa serikali za mitaa hupendelea ndugu au marafiki na watu wengine. 


Soma zaidi:


Utafiti huo wa awali wa ngazi ya kaya ulifanywa wilayani Maswa kwa wakuu wa kaya 602 na ulihusisha mahojiano ya vikundi na watu mashuhuri. 

Katika upande mwingine wa maafisa wa serikali za mitaa, Mshale anasema utafiti huo unaonyesha kuwa viongozi hao wanakumbana na changamoto lukuki zikiwemo kukosa fedha za kutosha kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila uchwao kiasi cha kutegemea zaidi michango ya wananchi. 

Dwese anakiri kuwa ni kweli wananchi wengi hawahudhurii mikutano kutokana na mwamko mdogo miongoni mwa wakazi wa maeneo mengi wilayani Maswa.

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza anasema ili maendeleo yaweze kutokea, yapaswa kuwepo ushirikishaji wa wananchi na kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wao. 

“Wananchi na viongozi wanapoaminiana na kumuona mwingine kama mshirika, taarifa zinapotolewa kwa uwazi na kwa wakati, na wote wakiwa na hamasa, ari, uwezo na fursa za kufanya kazi pamoja, matokeo yake ni mafanikio ya wazi na ya haraka,” anasema Eyakuze. 

Pamoja na kuwa wanasiasa wengi walionekana kutokubaliana na baadhi ya matokeo ya utafiti huo uliobainisha mapungufu yao, Serikali inawashauri kuwa viongozi wote wanapaswa kuwajibika na kuwasikiliza wananchi. 

Agnes Alex, Afisa Tawala wa Wilaya ya Maswa anasema kuwa takwimu zilizotolewa ni sahihi ni vema viongozi wa serikali za mitaa wafanyie kazi mapungufu yaliyoanishwa kweye utafiti huo. 

 “Kupitia hizi tafiti sisi Serikali tuna kitu cha kufanya kuhakikisha matakwa ya wananchi wetu ndani ya wilaya yetu yanatekelezwa kwa wakati na ufasaha,” anasema kiongozi huyo na kuongeza;

“Sisi tunaweza kuwa na matazamio yetu lakini na wananchi kwenye mazingira yao wanamatarajio yao wanayohitaji Serikali iwafanyie lakini sisi tunakuja tu na mambo yetu tunayaweka pale, hatuweza kupata mafanikio tunayohitaji.” 

Ili kutatua baadhi ya changamoto za mwamko mdogo katika kuhudhuria mikutano, Eliud Kabengo kutoka Shirika la Jema Action for Community Development la mkoani Simiyu anashauri kuwepo na mkakati wa kuwapa kipaumbele wanawake na kuongeza uwajibikaji katika serikali za mitaa. 

“Kwa sisi Wasukuma kutokana na utamaduni wetu wanawake hawako ‘comfortable’ (hawajisikii huru) kuongea mbele ya wanaume. Hivyo, tunapaswa kuwapa kipaumbele kuongeza ushiriki wao,” anasema. 

Enable Notifications OK No thanks