Wanawake wa shoka waliogoma kuwa ‘mkia wa kondoo’
- Wakataa kuwa nyuma nyuma kama mkia wa kondoo.
- Wakamatia kila fursa ya kuwatoa kimaendeleo.
- Wachochea mabadiliko wilayani Mbogwe.
Mbogwe. Katika shughuli za kijamii na maendeleo zinazofanyika katika wilaya ya Mbogwe mkoani Geita huwezi kukosa kusikia jina lake. Ni moja ya wanawake wachache mashuhuri anayefahamika karibu kila kata za wilaya hiyo iliyopo kanda ya Ziwa.
Rebeka Makenza, Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Waraghibishi Wilaya ya Mbogwe (MBODANET), amekuwa chachu ya mabadiliko miongoni mwa wanawake wa wilaya hiyo yenye kata 17.
Licha ya kuwa kihistoria wanawake walikuwa nyuma katika eneo hilo, mama huyo amewafanya wanawake wajionee fahari kushiriki katika mikutano na shughuli za maendeleo ya vijiji vyao.
“Tamaduni za watu huku Kanda ya Ziwa zilikuwa zinawanyima fursa wanawake kushiriki katika mikutano ya maendeleo hata katika maamuzi muhimu yanayohusu maisha yao,” anasema Rebeka.
Mwanamke wa mstari wa mbele
Miongoni mwa masuala anayohamasisha zaidi wanawake kushiriki ni katika masuala ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, elimu, maji ambazo zimesaidia kuboresha maisha yao na familia zao.
Mwanamke huyo anayeishi kata ya Nyasato wilayani humo amekuwa mstari wa mbele kubadilisha fikra na mtazamo hasi kwa jamii kuhusu nafasi ya mwanamke hasa katika kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo katika ngazi ya familia na jamii.
Yeye pamoja na wanawake wachache hawakufurahishwa na jinsi wanawake walivyokuwa wanaachwa nyuma kimaendeleo ndipo walipoamka na kuanza kutoa elimu kwa viongozi kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika vikao vya maamuzi.
“Haikuwa rahisi wakati huo tunaanza miaka ya 2016, tulipingwa sana na hata kutengwa lakini hatukuchoka kupigania maslahi ya wanawake. Tulitoa elimu, jamii imetuelewa sasa si ajabu kuona wanawake wakiwa mstari wa mbele kwenye shughuli za maendeleo,” anasema Rebeka.
Ushiriki wa wanawake katika mikutano ya vijiji umeongezeka wilayani Mbogwe baada ya kujengewa uwezo kuhusu mchango wao katika shughuli za maendeleo na waraghabishi. Picha| Gift Mijoe.
Safari ya mapambano ilivyoanza
Nguvu hiyo ya kudai mabadiliko waliipata baada ya kupata maarifa na ujuzi kuhusu uraghibishi kutoka Shirika la Tamasha kwa kushirikiana na shirika la Twaweza.
Mraghabishi kutoka kata ya Nyasato, Lucy Mganga anasema moja ya masomo waliyojifunza ilikuwa umuhimu wa kujenga jamii yenye usawa kwa makundi yote wakiwemo wanawake kushirikishwa kwenye masuala yanayohusu maendeleo ya vijiji.
Kwa mujibu wa Mganga ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Mbogwe, baada ya mafunzo hayo waliwakusanya wanawake wenzao kutoka maeneo mbalimbali na kuwapa mwanga kuhusu ushiriki wao kwenye maendeleo na namna wanavyotakiwa kuboresha maisha yao.
“Walikuwa wagumu kubadilika lakini tulipozidisha elimu na mwamko wa wanawake kudai haki zao ulipoongezeka walikubali na sasa wanawake wana nafasi kubwa sana katika maamuzi ya vikao vya maendeleo,” anasema mama huyo.
Elimu waliyoipata kutoka Tamasha iliwajenga kuwa wajasiri, wanaojitambua na kusimamia haki zao za msingi kwenye jamii ili kuepuka ukatili wa kijinsia.
“Tulikaa na wanawake tukawasikiliza, tukawapa nafasi yao wao kuzungumza katika mikutano ya hadhara na wanaume wakaanza kuelewa umuhimu kuwa wanawake wanapaswa kushiriki vyema katika mikutano waweze kutoa hoja zao na ziweze kusikilizwa,” anasema Mwenyekiti wa MBODANET, Petro Hyera.
Rehema Gervas, mkazi wa kijiji cha Isebya wilayani Mbogwe aliyenufaika na mafunzo ya uraghabishi yaliyomsaidia kujiajiri katika kazi ya ushonaji nguo. Picha| Gift Mijoe.
Faida zilizopatikana kwa wanawake
Iwapo mwenendo wa wanawake kushiriki katika maendeleo ya vijiji na mitaa ya Mbogwe utaendelea, itakuwa ni moja ya halmashauri nchini zitakazokuwa zikitekeleza ipasavyo Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG’s) ya mwaka 2030 yanayotaka kujenga jamii yenye usawa na shirikishi.
Uhamasishaji huo umesaidia kuongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki katika vikao vya maendeleo ya vijiji, jambo lililofanya wapewe nafasi zaidi ya kusikilizwa na hoja zao kutekelezwa ipasavyo na viongozi.
Mkazi wa kata ya Nyasato, Kabelela Augustine anasema ushiriki wa wanawake kwenye mikutano umeongezeka na kufanya sauti zao ziwe na nguvu hasa wanapotoa hoja zinazolenga kuboresha huduma za kijamii kama ujenzi wa zahanati na uchimbaji wa visima vya maji.
“Wakina mama wamekuwa ni wahamasishaji wakubwa wa maendeleo hususani uchangiaji wa huduma za afya. Kata ya Nyasato kabla ya uraghibishi ilikuwa na zahanati moja tu, sasa tunazo zahanati tatu zinazofanya kazi na maboma matatu ambayo yanasubiri kupauliwa,” anasema Augustine.
Imeongeza ujasiri na kujiamini kwa wanawake
Tofauti na miaka ya nyuma, kwa sasa siyo jambo geni kuona wanawake wilayani hapa wakiongea mbele ya viongozi kwenye mikutano na wakasikilizwa.
“Waraghibishi walituambia tunatakiwa kujiamini, uwe shupavu sehemu yoyote kuongea hata kama kwenye kikao usiogope maana hoja yako itatekelezwa,” anasema Catherine Edward, mkazi wa Nyasato kuwa hayo ni mabadiliko makubwa kwa sababu awali wanawake walikuwa hawashiriki kabisa mikutano ya vijiji.
Ushiriki huo umewafanya wanawake kuheshimika jambo lililosaidia hata kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwemo vipigo na udhalilishaji wa kingono.
“Mabinti wanaenda shuleni vizuri, kusumbuliwa na kupewa mimba kumepungua sana maana jamii inampa heshima mwanamke kutimiza ndoto zake,” anasema Annastazia Fungameza, mkazi wa kata ya Nyakafuru wilayani humo.
Sehemu kubwa ya wanawake wameunda vikundi vya kuinuana kiuchumi kwa kukopeshana ili kuendesha biashara ndogo ndogo na kilimo kujipatia kipato ambacho kinatumika katika familia na kusomesha watoto.
Wachochea maendeleo
Diwani wa kata ya Ushirika katika Halmashauri ya Mbogwe, Deogratious Shayo anasema kwa sasa wanawake wanashiriki kwa wingi kuliko wanaume kwenye shughuli za maendeleo na wanajitoa kujenga shule, zahanati na barabara.
“Sisi kama viongozi tunaona tumerahisishiwa kazi,” anasema Shayo ambaye kwa nguvu za wananchi wamefanikiwa kujenga shule ya sekondari na zahanati ambayo imekuwa msaada kwa wanawake wajawazito wa kata yake.
Zahanati ya Nyakafuru iliyopo kata ya Nyakafuru wilayani Mbogwe iliyojengwa kwa nguvu za wananchi baada ya kupewa elimu ya uraghabishi. Imekuwa mkombozi kwa wanawake na watoto waliokuwa wanasafiri umbali mrefu kusaka huduma za afya. Picha| Gift Mijoe.
Wapo kila kona
Katika miaka ya hivi karibuni wanawake wamepata nafasi za uongozi ndani ya vyama vya siasa, Serikali za vijiji na kamati za maendeleo na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mapato na rasimali za umma.
“Kamati za maendeleo za vijiji kwa sasa lazima ziwe na mchanganyiko wa wanawake na wanaume. Kukuta kamati haina mwanamke ni vigumu na wanafuatilia sana matumizi ya fedha za wananchi, wizi umepungua sana,” anaeleza mkazi wa kijiji cha Nyakafuru, Edward Sakay ambaye pia ni mraghibishi.
Serikali yakubali ‘muziki’ wa wanawake
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mbogwe, Martha Mkupasi anasema wanawake wengi kuliko wanaume hukushiriki zaidi katika miradi ya maendeleo.
“Hii inarahisisha kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Mkupasi kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Chato.
Anasema Mbogwe itaendelea kutoa ushirikiano kwa wanawake ili kuhakikisha wanakua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Latest
