Mamia wajitokeza kupata chanjo ya Corona Mwanza
- Zaidi ya watu 300 walijitokeza na kupata chanjo ya Uviko-19 ya Johnson & Johnson katika hospitali ya Sekou Toure pekee.
- Baadhi walalamikia kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kutolea chanjo licha ya kuwahi asubuhi.
Mwanza. Zaidi ya watu 300 wamejitokeza siku ya kwanza ya utoaji chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Korona (Uviko-19) katika kituo cha hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, ikiwa ni dalili kuwa wengi wapo tayari kupata kinga hiyo licha ya kuwepo kwa kiwango kikubwa cha upotoshaji.
Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo Uyanjo Nkumbi ameiambia Nukta Habari leo (Agosti 4, 2021) kuwa mwitikio ni mkubwa na hakuna malalamiko ya madhara yoyote yaliyowasilishwa kutoka kwa wananchi hao waliopatiwa chanjo hiyo.
Mkoa wa Mwanza ulianza rasmi utoaji wa chanjo ya Uviko-19 aina ya Johnson & Johnson au mashuhuri kama Janssen Agosti 3 ikiwa ni takriban wiki moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi mpango wa kuchanja nchini.
“Leo tunaweza kupata zaidi ya watu hao waliojitokeza jana kutoka kwenye makundi ainishi yanayotarajiwa kupata chanjo hiyo, mwitikio ni mkubwa na watu wamekuwa na ushirikiano na kutii kila maelekezo wanayopewa,” amesema Nkumbi.
Mmoja ya wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza kupata chanjo katika kituo cha hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure Agosti 4, 2021.
Nkumbi amesema zoezi hilo lilipofunguliwa jana watoa huduma za afya wamefanya kazi siku nzima bila kusimama na hii ni baada ya vyombo vya habari kuwafahamisha wakazi wa jiji hilo kuwa chanjo hiyo imewasili na ipo tayari kutolewa.
Mkoa wa Mwanza una vituo 26 vya kutolea chanjo ya Uviko-19 kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa.
Nkumbi amesema watu wanaofika hapo lazima wachukuliwe taarifa zao mahususi sanjari na kupimwa magonjwa kama presha, kisukari na homa ili watakapobaini waweze kumpatia mgonjwa ushauri wa kitaalam.
Amewatoa hofu kuwa dawa au chanjo yoyote inayoingia kwenye mwili wa binadamu huwa na maudhi madogo madogo hivyo watakapochoma sindano hizo wakipata maudhi hayo wasianze kutilia shaka.
“Dawa yoyote unayomeza iwe Panadol huwa ina maudhi madogo madogo kwa hiyo hata hii inaweza ikasababisha hivyo wasiwaze kuwa zina madhara hayo ni ya kawaida,”amesema Nkumbi.
Kumekuwapo na upotoshaji mkubwa katika mitandao ya kijamii kuwa chanjo hiyo si salama jambo ambalo si kweli na limelenga kutisha baadhi ya watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kuhusu kinga hiyo.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wakisubiria kupata chanjo ya Uviko-19 katika viwanja vya hospitali ya rufaa Sekou Toure Agosti 4, 2021 hadi sasa kituo hicho kimehudumia watu 300. Picha zote|Mariam John/Nukta.
Tanzania ilipokea dozi zaidi ya milioni moja za Johnson & Johnson kutoka kwa Serikali ya Marekani mwezi uliopita ikiwa ni msaada kupitia mpango wa kusaidia chanjo nchi zenye kipato cha chini ujulikanao kama Covax.
Katika kituo hicho cha Sekou Toure, Nkumbi amesema wanategemea kupata watu wengi zaidi kwa kuwa kipo katikati ya mji na tayari wameshafunga vipaza sauti kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi kuchanja dhidi ya ugonjwa huo.
Baadhi ya wakazi waliofika kupata chanjo hiyo wamesema hawajapata madhara yoyote isipokuwa wanaomba utaratibu ubadilishwe kwa kuwa huduma inaanza kwa kuchelewa.
“Nimefika hapa toka saa 12.30 alfajiri na kuna wananchi wengine wamefika kwa wakati lakini chanjo inaanza kutolewa kuanzia saa 3 asubuhi na hakuna taarifa yoyote ambayo wananchi wamepewa,” amesema Nurath Hussein mkazi wa Isamilo Mwanza.
Katika kituo hicho kulikuwa watu wamepanga foleni huku wengine wakiwa wanapimwa afya kabla ya kuchoma cha chanjo kwenye maeneo mbalimbali yaliyotengwa.
Sarafina Lusibamahila amesema alikuwa na shauku ya kupata chanjo hiyo ili kujikinga na ugonjwa huo kwa kuwa wataalam wa afya wanatoa elimu kuwa aliyechanjwa ana uwezekano mdogo wa kupata maambukizi hayo kuliko yule ambaye hajachanjwa.
Habari hii ni sehemu ya mfululizo wa habari na makala kukabiliana na Uviko kwa hisani ya Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest