Utoaji chanjo ya Uviko-19 wasuasua Mwanza, Serikali yaja na muarobaini
- Idadi ndogo ya watu wajitokeza kuchanjwa.
- Kampeni ya kata kwa kata yaanza kuhamasisha watu.
- Serikali yatoa wiki mbili chanjo ziwe zimeisha.
Mwanza. Baada ya Mkoa wa Mwanza kuwa na idadi dogo ya watu waliochanjwa chanjo ya Uviko-19, Serikali mkoani humo imekusudia kuanza kampeni ya kata kwa kata kuhamasisha watu kujitokeza kwenda kupata chanjo hiyo.
Tangu zoezi hilo lilipozinduliwa mkoani humu Agosti 3 mwaka huu ni asilimia 20 ya watu tu ndiyo wamejitokeza kupata chanjo hiyo ambayo ilitanguliwa na makundi maalum yawatoa huduma za afya, watu wenye umri zaidi ya miaka 50 na wenye magonjwa sugu.
Kampeni hiyo inaanza leo katika Kata za Buhongwa na Mkuyuni kwa wilaya ya Nyamagana na Butuja kwa Wilaya ya Ilemela inalenga kuongeza maeneo ya kutolea huduma hiyo ili kuwafikia watu wengi ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kuifuata.
Awali mkoa huo ulikuwa na vituo 26 vya kuchanja watu chanjo na ilipokea chanjo ya Uviko-19 dozi 90,000 lakini bado hazijaisha mpaka sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ametaja wilaya ya Ukerewe kuwa moja ya wilaya ambayo watu wake wanalazimika kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma hiyo.
“Kwa hiyo tumeona ni vema tupanue wigo wa kupeleka huduma hiyo kwenye maeneo ambayo watu wanalazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo, hivyo niombe watoa huduma waliopangwa kutumia fursa hiyo kuhakikisha wanafikisha huduma hiyo,” amesema Gabriel.
Japokuwa chanjo hiyo inatolewa kwa hiari lakini Mkuu wa Mkoa huyo amesema ni vema hamasa iongezwe ili kuwakinga watu dhidi ya maradhi hayo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa amesema utafiti uliofanywa hivi karibuni umebaini watu wanaopata chanjo wapo kwenye hatari ndogo ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo tofauti na wale ambao hawajachanja.
“Kupitia kampeni hii wanafunzi wote na wananchi wengine wajitokeze kwenda kuchanja kwenye vituo vitakavyotengwa ili waweze kuendelea na masomo yao kuliko huko mbele wakipata shida washindwe kuendelea na masomo yao,” amesema Gabriel.
huenda kampeni ya mkoa wa Mwanza ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Tanzania kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa chanjo dhidi ya Uviko-19 ili kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili chanjo za ugonjwa huo ziwe zimekwisha.
Dozi za chanjo zilizoingizwa nchini kutoka nchini Marekani ni milioni 1.058 ambapo hadi kufikia Septemba 15 zaidi ya nusu ya chanjo hizo bado zilikuwa hazijatumika.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuchanja ni hiari.
Latest
