Chanjo ya Uviko-19 kuanza kutolewa kwa waliotimiza miaka 18
Wananchi wakipatiwa chanjo ya Uviko-19 kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa huo mkoani Mwanza hivi karibuni. Picha | Mariam John.
- Hatua hiyo itasaidia kuwafikia vijana wengi na kuwakinga na ugonjwa huo.
- Pia Serikali iko mbioni kuanza kutoa chanjo za kusisimua (booster) za Uviko-19.
Mwanza. Serikali imesema itaanza kuwafikia vijana ambao hawakuwa wamefikisha umri wa kupata chanjo ya Uviko-19 tangu zoezi hilo lianze miaka mitatu iliyopita ambao kwa sasa watakuwa wametimiza miaka 18.
Pia iko mbioni kuanza kutoa chanjo za kusisimua (booster) za Uviko-19 kwa watu wote waliochanja chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.
Mratibu wa chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kitereja akizungumza na waandishi wa habari Januari 13 jijini Mwanza amesema lengo ni kuhakikisha wote waliopata chanjo mbalimbali na ambao hawakupata wanapatiwa kwa pamoja.
Kitereja pia amesema katika mpango huo wataweka msisitizo kwa wilaya ambazo zipo chini kwenye suala la uchanjaji ili ziweze kufikia lengo la kuchanja.
“Lengo tunatamani kuwapatia chanjo wote ambao hawajapatiwa chanjo na hasa wale ambao walikuwa chini ya miaka 18 wakati zoezi linaanza ambapo kwa sasa watakuwa wamefikisha umri wa kuchanja,” amesema Kitereja.
Kwa mujibu wa Kitereja amesema Mkoa wa Mwanza unakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 4 na kati ya hao watu milioni 1.8 ni vijana wenye umri wa miaka 18.
“Tunataka sasa kuwahamasisha hao vijana nao waweze kupatiwa chanjo ya Uviko-19 hivyo ni jukumu la kila mmoja vikiwemo vyombo vya habari kuhakikisha vinatoa elimu ya kuhamasisha watu kwenda kuchanja,” amesema Kitereja.
Amesema mpaka sasa mkoa umefanikiwa kuchanja kwa asilimia 100 ambapo waliochanja chanjo zaidi ya moja ni asilimia 102 huku waliochanja chanjo moja wakiwa ni asilimia 125.
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Silas Wambura amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba mwaka huu, mkoa huo ulikusudia kuchanja watu watu 1.2 milioni.
Amesema hadi zoezi linakamilika walikuwa wamefanikiwa kuchanja kwa asilimia 100.
Soma zaidi:
- Tanzania na Uviko-19: Maambukizi yaongezeka kwa asilimia 62
- Watanzania wahimizwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya mfumo wa hewa
Kihunzi cha kuvuka
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Clement Mwarabu ameeleza changamoto zinazokwamisha zoezi hilo kuwa ni imani potofu juu ya chanjo hizo ambapo wengi wanaamini ukichanja wanatokwa na damu nyingi.
“Changamoto iliyopo ni mapokeo hasi ya chanjo hizo kwa jamii ambapo wengi wanakuwa na imani zisizo sahihi, hivyo kwa sasa tunaendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo hiyo,” amesema Mwarabu.
Dk Mwarabu amesema zipo baadhi ya kata ambazo hazijawahi kuchanja kutokana na imani hasi hivyo wanatarajia kutumia mashirika mbalimbali ya afya ambayo yatatoa elimu nyumba kwa nyumba na kwenye mikusanyiko ya hadhara ili waweze kutimiza lengo la kuchanja watu 219, 000 katika wilaya hiyo ifikapo Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia kufikia Januari 11, 2022, Tanzania imeripoti visa 42,467 vya Uviko-19 huku watu 846 wakifariki kwa ugonjwa huo.