Chanjo ya Corona yapokelewa kwa hisia tofauti Mwanza
- Yazinduliwa jijini hapa huku wengi wakijitokeza kuchanja.
- Wengine waendelea kushirikilia kumtegemea Mungu.
- Serikali yawataka walio tayari kujitokeza kwa wingi kuchanja.
Mwanza. Mkoa wa Mwanza leo umezindua rasmi zoezi la utoaji chanjo huku wakazi wa jiji hilo la kibiashara wakiipokea kwa hisia tofauti kwa baadhi kusema watachanja chanjo hiyo kwa sababu wameshuhudia marafiki zao wakipoteza maisha.
Chanzo inayotolewa kwa sasa nchini ni aina ya Johnson & Johnson ambapo kipaumbele kimewekwa kwa watumishi wa afya, watu wenye umri zaidi ya mika 50 na wagonjwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel leo Agosti 3 amezindua rasmi utoaji wa chanjo mkoani hapa kwa yey kuchanjwa pamoja na viongozi na wananchi katika Hospital ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure.
Viongozi wengine waliochanjwa mapema leo Agosti 3 ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilinga na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Antony Diallo.
“Ninaomba tusiogope sindano lakini mambo mengine madaktari watawasaidia namna ya kufanya, na zaidi tuzidi kumwomba Mungu tusiogope Mungu wetu yupo, “amesema Gabriel muda mfupi kabla ya kupata chanjo hiyo ambapo Mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya dozi 90, 000.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel akipatiwa chanjo ya kujikinga na Uviko-19 leo Agosti 3 katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure ambapo jumla ya dozi 90, 000 zimwasili. Picha| Mariam John.
Wananchi walivyoipokea chanjo hiyo
Baada ya uzinduzi huo, kumekuwa na hisia tofauti kwa wakazi wa jiji hili lililoko Kanda ya Ziwa kuhusu utayari wa kuchanja chanjo hiyo ili kujikinga na ugonjwa huo.
Walio tayari na ambao baadhi yao wamepata chanjo hiyo leo, wameeleza kuwa msukumo uliowafanya wapate chanjo hiyo ni tahadhari na namna wanavyoshudia wenzao wakipoteza maisha kwa ugonjwa huo.
“Nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe kuchanja, kwa kuwa nimeshuhudia marafiki zangu wakipoteza maisha na wengine kulazwa kwenye hospitali na kuwekewa mitungi ya kupumulia imenihamasisha sana ili niendelee kuchukua tahadhari,” amesema Mkazi wa mtaa wa Isamilo, Kulwa Msekwa.
Amesema baadhi ya Watanzania wameingia kwenye mkumbo wa kupotosha jamii hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa huu kutokana na watu kupuuzia kutokana na upotoshaji uliopo.
“Watu wasipoteze matumaini wengine, waache upotoshaji na watambue hili suala ni la hiari si la lazima, chanjo hii si ya kwanza kutolewa zipo chanjo nyingi zilipita huko nyuma miaka ya 1960 ikiwemo ya ndui, pepopunda, surua, polio ambazo zilikuwa zinatolewa hadi mashuleni na zilisaidia,” amesema Mzee Msekwa.
Mzee huyo ameeleza kuwa “watu wajue kuwa wakishachanjwa wanajikinga wao na ndugu zao lakini pia waendelee kuchukua tahadhari ikiwemo ya kuvaa barakoa.”
Hadi kufikia Julai 22 mwaka huu, Tanzania imeripoti wagonjwa 858 wa Uviko-19 tangu ugonjwa huo ulipoingia nchini Machi 2020.
Mkazi mwingine jijini hapa, David Francis, hajapoteza ndugu na hajawai kuugua ugonjwa huo isipokuwa amemua kuchukua tahadhari ya kuchanja ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na ugonjwa huo.
Charles Maburuki amesema amejitokeza kuchanja kwa ajili ya usalama wa afya na familia yake na kuikubusha jamii kuungana pamoja kwenye hili suala la chanjo kwa ajili ya usalama wao.
Baadhi ya Wakazi jijini Mwanza wakiwa wamepanga foleni kwa ajili ya kupata fomu ya kuapatiwa chanjo ya Uviko-19 katika viwanja vya hospital ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure. Picha| Mariam John.
Wakati mwitikio ukionekana kuwa mkubwa watu wazima ambao wamejitokeza kupata chanjo hiyo leo, wapo ambao bado hawajapata hamasa hiyo.
“Rais Hayati John Magufuli alituambia tusiwe na hofu tuzidi kumwomba Mungu kwa kuwa yeye ndiye anaweza kuiponya hiyo Corona na kutuweka huru kutoka kwenye hili janga,” amesema mkazi wa Kiloleli jijini hapa, Meshack Ilunda.
Ilunda anasema hawezi kuchanja na ataendelea kusimamia imani yake ya kusali na kumwomba Mungu akiamini atamkinga na ugonjwa huo.
Mkazi mwingine wa mtaa wa Isamilo, Raphael Maira amesema yeye amechukua fomu kwa ajili ya kupata chanjo lakini ataenda kumwomba Mungu ili apate jibu la moja kwa moja kama atachanja au hatachanja.
“Bado natafakari na nitaendelea kumwomba Mungu ili kupata njia ya kufanya kwa sasa bado ni fumbo,” amesema Maira.
Changamkieni chanjo
Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Thomas Rutachunzibwa amewataka wananchi wenye sifa ya kupata chanjo kwa sasa, kuchangamkia fursa hiyo kwa sababu chanjo iliyopo ni chache.
Amesema kwa sasa chanjo hizi zinatolewa bure huenda huko mbele mambo yakabadilika zikawa zinapatikana kwa shida na gharama kubwa.
“Kwa sasa tunapokea chanjo bure hatuwezi kujua huko mbeleni huenda zikapatikana kwa shida na kwa gharama kubwa hivyo ni vyema tukajitokeza kuchanja wakati huu zikiwa zinapatikana,” amesema Dk Rutachizibwa.
Latest
