Majuta: Picha ya Hayati Magufuli iendelee kubaki ofisini

April 6, 2021 11:49 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wanachama wa Mujuta ambao wamesema wanaamini ndiyo sahihi ya kumkumbuka.
  • Utaratibu wa Serikali ni kuwa Rais akifariki au akistaafu, picha yake inaondolewa katika ofisi za umma na binafsi. 

Mwanza. Ikiwa ni leo ni siku ya mwisho ya maombolezo ya kifo cha Rais wa Tanzania Hayati Dk John Magufuli, Shirika la Mfumo na Muundo  wa Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata) limeiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoziondoa picha za viongozi wakuu wa nchi waliostaafu au kufariki  kwenye maofisi ili kutopoteza  kumbukumbu kwa waliyotenda hapa nchini.

Hayati Dk Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu na kuzikwa Chato mkoani Geita. Kutuatia kifo hicho, Serikali ilitangaza siku 21 za maombolezo ya kitaifa na kuagiza bendera kupepea nusu mlingoti.  

Mratibu wa mafunzo wa Mujata, John Malagira amesema Serikali iliweka utaratibu wa kiongozi anayemaliza muda wake madarakani au kifo kinapotokea basi picha yake iondolewe ofisi lakini kuna haja ya kutazama upya utaratibu huo.

“Hii inadhihirisha wazi kuwa kumbukumbu za viongozi hao zinapotea au anapofariki kiongozi huyo anazikwa na picha zake, hivyo ni vema ukawepo utaratibu wa picha hizo kuendeleza kubaki kama kumbukumbu kwa taifa,” amesema Malagira.

Kiongozi huyo ametoa pendekezo hilo leo Aprili 6, 2021 katika wanachama wa Mujata walipokutana pamoja kufanya maombi ya kumshukru Mungu kwa ajili ya maisha ya Hayati Magufuli hapa duniani. 

Amesema pamoja na kwamba hayati Magufuli  amelala kaburini, lakini Tanzania haijabaki yatima kwa kuwa tayari kwa mujibu wa Katiba, Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza pale alipoishia kiongozi huyo.

“Tunaimani na Rais Samia tunajua Taifa ataliongoza vema na sisi kama Mujata tupo nyuma yake kuhakikisha tunamsaidia kutatua changamoto zinazoikumba jamii,” amesema.


Soma zaidi:


Mujata wamesema wataendelea kumkumbuka Hayati Magufuli hasa kwa kutunga sheria mbalimbali zilizosaidia kulinda rasimali za Taifa na kuondoa mikataba mibovu hususan ya madini.

Pia wataendelea kumuenzi kwa kuhakikisha elimu ya msingi inatolewa bure, kusimamia maendeleo ya Taifa na kurudisha hadhi ya taasisi za umma.

Kiongozi wa wanawake kutoka Mujata, Juliana Mushi ametumia maombi hayo kuwataka akina mama kuendelea kuungana pamoja kumsaidia Rais Samia ili aweze kutatua changamoto zinazowakumba wanawake.

Amesema zipo changamoto za ukatili wa kijinsia, masuala ya ndoa na talaka mahakamani ambazo kila kukicha zinaongezeka, mirathi na suala la mimba katika umri mdogo.

Mushi amesema ipo haja ya sheria kubadilishwa ili watoto wanaopata mimba katika umri mdogo waendelezwe kielimu  na suala hilo pia lipewe kipaumbele hata kwa wanawake ambao hawajui kusoma na kuandika.

“Ikiwezekana wapate muda angalau wa kufundishwa hata wanapokuwa nyumbani lengo ni kuhakikisha wanapunguza ongezeko la wanawake wasiojua kusoma na kuandika nchini,” amesema.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW