Kwaheri “Jeshi”: Mamia wajitokeza Mwanza kumuaga hayati Rais John Magufuli

March 24, 2021 5:49 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mchakamchaka wa wananchi walioamua kusindikiza mwili wa Hayati Rais Magufuli ni mkubwa kiasi cha kutokuweza kuona mwisho wake.
  • Kanga, vitenge, mitandio vyatandikwa barabarani kuonyesha kuguswa na msiba huo wa kitaifa.
  • Wengi waimba “Magufuli jeshi”, “Magufuli jeshi”

Dar es Salaam. Kuanzia kutoka katika uwanja wa ndege wa Mwanza hadi katika uwanja wa michezo wa CCM Kirumba ni sauti mchanganyiko za simanzi zikiwemo zinazomsifu aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Magufuli kuwa alikuwa “Jeshi”. 

“Magufuli Jeshi, Magufuli Jeshi, Magufuli Jeshi…” watu wengi wamesikika wakiimba asubuhi ya Machi 24 baada ya kupokea mwili wa kiongozi huyo uliokuwa ukiwasili jijini hapo kutokea visiwani Zanzibar baada ya kuagwa jana. 

Sanjari na nyimbo hizo, vilio vya akina mama, vilivyojaa uchungu, vimekuwa mbadala wa kelele za magari, muziki na za watu masokoni zilizozoeleka katika jiji hilo lilipo kandokando mwa Ziwa Victoria. 

Wenye Khanga wamezitandika barabarani huku wale wenye nguvu wakikimbia sanjari na msafara uliobeba mwili wa kiongozi huyo aliyefariki Machi 17 wakati akipatiwa matibabu ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. 

Wananchi wa jijini Mwanza wakiusubiri mwili wa Hayati Rais Magufuli katika viwanja vya CCM Kirumba. Picha| Full Shangwe Blog.

Walioshindwa kuusindikiza msafara huo wamejipanga barabarani  wakilia, wakifanya maombi na kupeperusha majani ya miti na wengine wakiwa wamenyanyua mabango mbalimbali yakiwemo yenye ujumbe wa maneno ya “Hatutokusahau”.

Kundi kubwa la watu wanaosindikiza msafara huo limekuwa kubwa kiasi fulani kuwapa shida maafisa usalama kutengeneza njia kwa ajili magari yaliyopo katika msafara huo kupita.

Ndani ya uwanja wa CCM Kirumba watu wamejaa kiasi cha wengine kushindwa kuingia ndani. Tayari mwili wa Hayati Magufuli (61) umeshaingia katika uwanja huo kwa ajili ya kuagwa na wakazi hao. 

Baada ya kuagwa jijini Mwanza mwili wa Hayati Magufuli unatarajiwa tena kuagwa mkoani Geita kabla ya kupumzishwa kwenye nyumba ya milele hapo Machi 26 katika kijiji cha nyumbani cha Chato wilayani Chato. 

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV