Hayati Rais John Magufuli azikwa nyumbani kwao Chato, Tanzania

March 26, 2021 3:40 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kiongozi huyo alifariki Machi 17 mwaka huu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.
  • Rais Samia Suluhu Hassan awataka Watanzania kushikamana na kuonyesha upendo katika kipindi hiki kigumu.
  •  Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya pili, amwelezea Hayati Magufuli kama mchapakazi aliyeiletea Tanzania maendeleo ndani ya muda mfupi.

Dar es Salaam. Hatimaye mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk John Magufuli umezikwa katika makaburi ya familia katika mji wa Chato mkoani Geita ikiwa ni wiki moja baaada ya Watanzania kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyefariki Machi 17 mwaka huu.

Mwili wa Hayati Magufuli uliingizwa kaburini Saa 11 kasoro jioni Machi 26 huku sala ya maziko yake yakifanywa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge -Ngara, Severine Niwemugizi.

Kuzikwa kwa mwili huo wa Hayati Magufuli kunahitimisha safari ya maisha ya miaka 61 ya kiongozi huyo ambaye kwa miaka mitano na nusu aliongoza kama Rais wa tano wa Tanzania hadi alipofikwa na umauti katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Kabla ya maziko hayo, ilifanyika misa ya maalum ya maziko katika uwanja wa Magufuli mjini Chato iliyoongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Gervas Nyaisonga ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliwasihi Watanzania kuwa na ushirikiano na upendo. 

“Nachotaka kuwaambia Watanzania Dk John Magufuli ameitwa na Mungu na ameitika na leo tunakwenda kumstiri. Tunachokwenda kukistiri ni kiwiliwili chake tu lakini maono, mikakati na falsafa yake ya ‘Hapa ni kazi tu’ itaendelea kuwepo na tutaendelea kuifanyia kazi,” amesema Rais Samia. 

Kiongozi huyo wa juu wa nchi amewataka wote wanaotoa huduma kwa wananchi serikalini, sekta binafsi na viongozi wa dini kuonyesha mshikamano, ushirikiano na upendo kwa Taifa.

“Kama muda tunaotakiwa kuonyesha upendo kwa taifa letu ni muda huu ambapo tumeondokewa na mpendwa wetu, jemedari wetu. Basi tusiyumbe na tusiliyumbishe Taifa. Twendeni tukaoneshe upendo, tukaoneshe mshikamano, twendeni tukaliendeleze Taifa la Tanzania,” amesema Rais Samia aliyeapishwa Machi 19 baada ya kifo cha hayati Magufuli. 



Katika salamu za rambirambi, viongozi mbalimbali walimwelezea hayati Magufuli kuwa alikuwa ni mchapakazi aliyefanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ndani ya muda mfupi na kuishangaza dunia. 

Mmoja ya waliotoa salamu za rambirambi katika shughuli hiyo ni Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (95) aliyefanya umati uliokuwepo kiwanjani hapa kufurahi kutokana na kusahau baadhi ya majina au maneno huku akimsihi Rais Samia na waombolezaji kumvumia katika hotuba yake kwa kuwa ni mzee. 

“Kwa muda mfupi wa miaka mitano amejenga barabara za lami nyingi, alikuwa hodari sana kwa statistics angetuambia hapa. Barabara nyingi zimejengwa katika nchi hii kwa muda mfupi sana. Amestawisha uwekezaji na biashara nchini kwa kurahisisha mawasiliano. Hata masoko makubwa ya kisasa yuamenza kuchipuka kama uyoga katika nchi yetu,” amesema Mzee Mwinyi.

Mwinyi amesema hayati Magufuli amewaondolea wamachinga fedheha ya kuwindwa katika kando za barabara badala yake akawapa ruhusa ya muda kufanya biashara zao huku akiwatafutia maeneo yatakayowafanya waendeshe biashara zao kwa utulivu. 

Hata wakati baadhi wakimwagia sifa kedekede kwa ujenzi wa miundombinu baadhi ya watu wamemsifu na kumkosoa katika baadhi ya mambo ambao wanaona hayakuwa sawa. 

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo katika makala yake ya rambirambi amesema hayati Magufuli amewafunza mengi ikiwepo kuhakikisha kiongozi ajaye kama yeye haruhusiwi “kufanya atakalo.” 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW