Siku ya mwisho Rais Magufuli kuzungumza hadharani

Mwandishi Wetu 0131Hrs   Machi 18, 2021 Habari
  • Iliongea hadharani Februari 26, 2021 wakati wa uzinduzi wa majengo ya Chuo Cha Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
  • Alitoa maagizo makuu mawili kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Wizara ya Mambo ya Ndani.
  • Rais John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam. 

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiomboleza kifo cha Rais John Magufuli, atakumbukwa kwa maagizo makuu mawili aliyoyatoa alipozungumza hadharani kwa mara ya mwisho katika ziara yake mkoani Dar es Salaam Februari 26, mwaka huu. 

Februari 26, wakati wa uzinduzi wa majengo ya Chuo Cha Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mkopo wa Sh19 bilioni uliotolewa na benki ya CRDB kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Dk Magufuli alisema uchunguzi wa kina ufanyike juu ya matumizi ya fedha za mkopo huo maana kuna harufu ya ufisadi.

“Hakuna hela itakayotolewa na Serikali, sana sana itachunguza hizo fedha zilikwenda wapi na kamanda wa Takakukuru naomba ufuatilie hilo wamenisaidia kujieleza hapa ili tujue hiyo hela nani alikwenda kufanya majadiliano na CRDB? Je maeneo hayo yalikuwa ya nani? Je hizo fedha zilizokuwa zinalipwa ndiyo zilikuwa zinastahili?,” alihoji Rais wakati akitoa maagizo ya kufanyika kwa uchunguzi.  

Hatua hiyo ilikuja baada ya Mbunge wa Temeke, Doroth Kilave kumuomba Dk Magufuli aisaidie manispaa hiyo kulipa kiasi Sh12.9 bilioni kilichobaki kati ya Sh19 bilioni ilizokopa katika benki hiyo ya biashara.


Soma zaidi: 


Rais magufuli aliyeonekana akishangiliwa na maaskari waliohudhuria uzinduzi huo, pia aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kushughulikia changamoto za wastaafu wa Jeshi la Polisi kucheleweshewa mafao yao licha ya kulitumika Taifa kwa uzalendo. 

“Kuna suala limezungumzwa hapa la wastaafu wa Jeshi la Polisi kutokulipwa mafao yao, msema kweli mpenzi wa Mungu, mimi nawashangaa Wizara ya Mambo ya Ndani na nina uhakika hata raia wengine wanawashangaa yule mstaafu wako amefanya kazi nzuri katika miaka yake yote.

“Amemaliza Jeshi la Polisi bila tatizo lolote, anatakiwa kulipwa mafao yake na mafao yake yapo, Waziri utakaa ofisini bila kwenda kuwaombea kwa nini? Katibu Mkuu umekaa ofisini tu, Naibu Katibu Mkuu umekaa ofisini tu, kwanini usichukue haya majina ukatembea ukaenda Wizara ya Fedha ukasema nina wastaafu hapa nataka fedha zao ziende,” alihoji Rais Magufuli.

Baada ya ziara hiyo ya mkoani Dar es Salaam, Rais Magufuli ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 61 alionekana hadharani wakati wa kuapishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi mpya Dk Bashiru Ally Ikulu mkoani humo. 

Hata hivyo, Rais hakuzungumza katika hafla hiyo na tangu hapo hajaonekana tena hadharani mpaka umauti unamkuta. 

Rais John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu kwa maradhi ya moyo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema jana wakati akitangaza kifo chake kupitia Shirika la Habari la Tanzania (TBC).

                     

Related Post