Rais Magufuli afariki dunia kwa maradhi ya moyo Tanzania

Mwandishi Wetu 1623Hrs   Machi 17, 2021 Habari
  • Alikuwa amelazwa katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha Rais John Magufuli aliyefariki wa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mama Samia amelitangazia taifa kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Jumatano ya Machi 17, 2021 kuwa Rais Magufuli alifariki Saa 12 jioni baada ya kulazwa hospitali hapo tangu Machi 14 mwaka huu.  

“Ndugu Watanzania kwa masikitiko makubwa nawajulisha kuwa leo 17 machi 2021 majira ya saa 12 jioni tumempoteza kiongozi wetu shupavu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Mheshimiwa Rais Magufuli alilazwa 6 Machi mwaka huu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete  kwa tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo kitaalumu linajulikana kama  Chronic Atrial Fibrillation ambalo alikuwa nalo kwa miaka 10,” amesema Mama Samia kwa machungu.

Mama Samia amelieleza taifa kuwa baada ya kupatiwa matibabu JKCI, Rais Magufuli aliruhusiwa Machi 7, mwaka na kuendelea na majukumu yake.

“Tarehe 14 Machi 2021 alijisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Mzena ambapo aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa JKCI hadi umauti ulipomkuta,” ameeleza.

Kiongozi huyo amesema mipango ya mazishi ya kiongozi huyo inafanywa na wananchi watajulishwa.  

“Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti,” amesema.

Related Post