Labda kesho: Wanafunzi wanavyosotea kumpata mwalimu wa kike Maswa
- Hawajawahi kuwa na mwalimu wa kike kwa miaka mitano sasa.
- Wakiwa katika hedhi hulazimika kusitisha masomo kwenda nyumbani kujisitiri.
- Wazazi wasema Serikali inachelewa kupeleka walimu wa kike.
- Serikali yasema itatua tatizo hilo ndani ya mwaka huu wa fedha.
Maswa, Simiyu. Joyce Ngassa amebakiza takriban miezi sita tu ahitimu elimu ya msingi. Hata hivyo, binti huyo wa miaka 15 huenda akamaliza elimu yake katika Shule ya Msingi Mwamihanza bila ya kumuona wala kufundishwa na mwalimu wa kike.
Hali hiyo si kwa siku za hivi karibuni tu, la hasha! Joyce na wanafunzi wenzie wa shule hiyo iliyopo wilayani Maswa mkoani Simiyu hawajawahi ‘kubahatika’ kuwa na mwalimu wa kike kwa miaka mitano sasa.
Hali hiyo huenda hali hiyo si tatizo kwa watoto wa kiume lakini kwa Joyce na wenzie wa kike ni kikwazo katika safari yao ya kujifunza na afya ya mwili na akili.
Siku wasichana wakiwa hedhi ni shida tupu
“Tunatamani tungekuwa na mwalimu wa kike hapa shuleni, tunawahitaji sana kwa sababu kuna wasichana wengine wamefikia umri wa kupata hedhi lakini kwa sababu hakuna walimu wanawake, wanapata tabu, wanaogopa kuwaambia walimu wa kiume,” anasema Joyce kwa aibu.
Joyce anasema wakiwa katika hali hiyo hulazimika kusitisha masomo kwa muda na kwenda nyumbani ili wakasaidiwe na wazazi au walezi wao, jambo ambalo lingezuilika iwapo kungekuwa na mwalimu wa kike.
Ukosefu wa walimu wa kike katika shule hii ni moja ya vikwazo vinavyowakumba watoto wa kike katika kusaka elimu kutokana na maumbile yao ukiachana na vikwazo vingine vya kimila na kijamii vinavyowakumba wanawake.
Kwa kawaida wasichana waliotoka kuvunja ungo au kupevuka huhitaji msaada wa karibu ikiwemo mafunzo ya usafi binafsi na usafi wa mazingira, namna ya kutumia visodo na kutunza mazingira ya vyoo na bafu au chumba maalum cha kujisitiri.
Tofauti na wenzao ambao hawana vyoo vya kutosha na maji safi na salama, wanafunzi wa kike wa Mwamihanza wao wana miundombinu hiyo lakini ukosefu wa walimu wa kike ni kikwazo kikuu.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwamihanza wilayani Maswa wakimsikiliza mwalimu wao (hayupo pichani). Hata hivyo, wanafunzi kwa muda mrefu hawajawahi kuwa na mwalimu wa kike. Picha| Nuzulack Dausen.
Mwalimu wa afya huokoa jahazi
Ili kuwasaidia wanafunzi hawa, mwalimu aliyefundishwa masuala ya afya na usafi huwapatia elimu ya kujisitiri japo baadhi ya watoto hawa wanaona aibu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wa Watoto (UNICEF) linasema uwepo wa walimu wa afya na usafi waliopewa mafunzo stahiki ni muhimu katika kuwasaidia watoto wa kike wakue kitaaluma, kimwili, kiafya na kiakili.
Hata hivyo, si shule zote Tanzania zina walimu hao waliofunzwa kama huyo wa Mwamihanza jambo linalowaacha wengi bila huduma hususan wale wasiokuwa na walimu wa kike.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwamihanza, Christian Machobo anasema mwalimu wao wa afya alishapewa mafunzo kuwafundisha wanafunzi waliopevuka kama sehemu ya somo la sayansi ili waweze kujisitiri pale wanapokuwa wameingia kipindi cha hedhi.
Ripoti ya Tathmini ya Huduma za Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni ya mwaka 2018 (2018 School Water, Sanitation and Hygiene Assessment) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa ni asilimia 44 tu za shule Tanzania zina walimu waliofundishwa kuhamasisha usafi na afya kwa watoto.
Hii ni sawa na kusema walimu wanne kati ya 10 pekee ndiyo wamepewa mafunzo ya kuhamasisha usafi binafsi na usafi wa mazingira shuleni.
Ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano na UNICEF mwaka 2020 inaeleza kuwa walimu wa shule za msingi walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufundishwa uhamasishaji wa masuala ya usafi binafsi na afya ya mazingira shuleni kwa asilimia 49.2 kuliko wale wanaofanya kazi katika shule za sekondari kwa asilimia 33.3.
Soma zaidi:
- Binti wa miaka 22 anayepambana kuung’oa umaskini Kanda ya Ziwa
- Zaidi ya nusu ya wakazi Maswa hawafamu hata mkutano mmoja wa kijiji uliofanyika 2021
Wake wa walimu, kamati hugeuka ‘walimu wa kike’
“Tunapata wakati mgumu…pale tatizo kama hilo linapotokea labda la muda mrefu huwa tunawasiliana na wanakamati wanawake lakini kama ni la ghafla wake wa walimu huwa wanatusaidia,” anasema mwalimu Machobo.
Machobo, ambaye amekuwepo shuleni hapo kwa miaka mitano, anasema ameshawasilisha tatizo hilo kwa uongozi wa halmashauri na kwamba ameahidiwa kuwa watatua tatizo lake.
Miaka ya nyuma, anasema, kulikuwa na walimu wa kike lakini walihamishwa kwa mujibu wa sheria japo yeye hajamkuta mwalimu wa kike shuleni hapo.
Wakazi wa kijiji hiki wanaona kama kasi ya Serikali kutatua tatizo hilo ni ndogo. Wazazi na walezi wameiambia Nukta kuwa Serikali ina uwezo wa kutatua tatizo ndani ya muda mfupi ikiwemo kuboresha mazingira ili walimu wa kike waweze kuishi kijijini hapo.
Baadhi ya wananchi wameanza jitihada za kuishinikiza Serikali kuharakisha upatikanaji wa mwalimu angalau mmoja wa kike kuwanusuru wasichana na usumbufu wa kurejea nyumbani na kukosa masomo pale wanapokuwa katika hedhi.

Kwa nini Mwamihanza?
“Pale shuleni hamna walimu wa kike tofauti na miaka ya nyuma, tunawahitaji walimu hawa haraka. Walimu wa kike ni muhimu kuna baadhi ya mambo wanatakiwa kuwafundisha watoto wetu lakini hawapo, si sawa,” anasema Agness Mussa, mkazi wa kijiji cha Mwamihanza na kuongeza kuwa,
“Wakiwa kwenye siku zao walipaswa kusaidiwa hasa wanafunzi wadogo waliotoka kupevuka.”
Wahamasishaji wa maendeleo katika kijiji hiki wanasema kuwa si jambo jema shule kuwa na walimu sita halafu wote wakawa wa kiume.
Dominick Richard (24), Mraghbishi katika Kijiji cha Mwamihanza anasema mwalimu wa kike mbali na kusaidia katika masuala ya hedhi na ugonjwa, ni rahisi kuwafundisha wanafunzi wao namna ya kuepuka vishawishi vya wanaume wakware kwa kuwa wana uzoefu mwingi wa kuwahudumia watoto wa kike.
Kwa mujibu wa uongozi wa shule hiyo walimu sita waliopo wanafundisha wanafunzi 441 ambao zaidi ya nusu au 235 ni wasichana.
Idadi hiyo ya walimu inafanya wastani wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 73, juu ya kiwango kinachopendekezwa na Serikali cha mwalimu mmoja wanafunzi 45.
Mwalimu Christian Machobo akimhudumia mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwamihanza wilayani Maswa. Watoto wa kike hawana walimu wa kike ambao wangeweza kuwakimbilia kupata huduma za faragha kama wenzao wa kiume. Picha| Nuzulack Dausen.
Serikali yaahidi kupeleka walimu wa kike
Serikali inasema inafahamu tatizo la ukosefu wa walimu katika shule hiyo hasa la ukosefu wa walimu wa kike na kwamba wameanza kutafutia suluhu ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/23.
“Hivi punde tutapata fedha za kusawazisha ikama walau tupeleke mwalimu wa kike kule (Mwamihanza) wa kukaa na wanafunzi wa kike,” anasema Vivian Christian, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
“Tutalifanyia kazi hilo kwa sababu ni lazima kwenye jamii yenye watoto wa kike kuwe na mwalimu wa kike kwa sababu kuna mambo wanafunzi hao watakuwa wanaongea na mwalimu wa kike ambayo hawawezi kuongea na wa kiume,” anasema Christian.
Christian anasema hatua hiyo ni ya awali kutatua uhaba wa walimu wa kike wakati wakisubiria Serikali iwaongezee idadi ya walimu kwa kuwa kwa sasa wana upungufu wa walimu 800 kwa shule za msingi na walimu zaidi ya 200 kwa shule za sekondari.
Latest