Shule 1,342 zanufaika na mradi wa vyoo wa Benki ya Dunia

June 11, 2024 2:42 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni shule za msingi za umma zilizopo Tanzania ambazo zimejengewa vyoo na miundombinu ya kunawia.
  • Umesaidia kuimarisha ufaulu kwa watoto wa kike nchini.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imesema imefanikisha ujenzi wa vyoo na miundombinu ya kunawia kwa shule za msingi 1,342 nchini hatua itakayosaidia kuimarisha afya za wanafunzi na walimu kuchochea ufaulu wa masomo.

Shule hizo kutoka mikoa 25 nchini Tanzania zimenufaika na huduma hiyo kupitia mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira (WASH) unaotekelezwa na Wizara ya Maji Tanzania chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kuanzia mwaka 2019 hadi 2025.

Benki hiyo imesema sehemu ya wanufaika wa mradi huo ni shule zilizopo vivijini ambazo hazina miundombinu hiyo.

Mhandisi Mashaka Sitta, Mratibu Miradi kutoka Wizara ya Maji aliyekuwa akiwasilisha matokeo ya mradi huo leo Juni 11, 2024 jijini Dar es Salaam amesema mradi huo utafikia shule 1,853 kufikia mwaka 2025.

“Lengo la mradi huo ni kusaidia wanafunzi kuepukana na magonjwa pamoja na utoro kwa watoto wa kike uliotokana na kukosekana kwa mazingira mazuri ya kujistiri wakiwa katika siku zao (hedhi),” amesema Mhandisi Sitta.

Utekelezaji wa mradi huo unawapa ahueni wanafunzi na walimu wao ambao awali walilazimika kujisitiri katika mazingira yasiyofaa huku watoto wa kike wakiathirika zaidi wakiwa wakati wa hedhi. 


Soma zaidi:Ripoti: Afya ya akili chanzo cha watu kujiua, kuua Tanzania


Evelina Saul, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule yaMsingi Katete B mkoani Kigoma anasema yeye na wasichana wenzake wanaweza kuhudhuria shuleni katika siku tano za wiki hatua inayoweza kuongeza ufaulu wa masomo.

“Tulikuwa tunakosa masomo ambayo yangeweza kutusaidia hata katika mitihani lakini tulikuwa tunayakosa tunakaa nyumbani mpaka siku zetu zitakapoisha tunarudi shuleni,” amesema Evelina katika video ya wanufaika wa mradi wa WASH.

Naye Sekani Mwampashi, Mwalimu wa Shule ya Msingi Ifunda iliyopo Mkoani Iringa anasema baada ya mradi huo sasa wanaweza kuwasaidia wanafunzi hao kujistiri kwa kuwapa taulo za kike pamoja na kuwafundisha kujisafisha kupitia maji safi na salama yanayopatikana shuleni hapo.

Wanafunzi katika shule ya  Shule yaMsingi Katete B mkoani Kigoma wakinawa mikono katika mabomba yaliyowekwa shuleni hapo chini ya mradi wa .Maji safi na Usafi wa Mazingira (WASH). Picha|WB/X(Twitter)

Afya za wanafunzi zimeimarika

Mwalimu Mwampashi anaeleza kuwa mbali na mradi huo kunufaisha watoto wa kike kujistiri wakati wa hedhi pia umeimarisha afya za wanafunzi hao ambao awali walikuwa wakishambuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo ya mfumo wa mkojo (UTI) na homa za matumbo.

Magonjwa hayo yalisababishwa na kukosekana kwa maji ya kunawa mikono kabla ya baada ya kutoka chooni pamoja na miundombinu mibovu ya choo iliyowalazimisha wanafunzi wengi kutumia tundu moja la choo. 

Kwa mujibu Benki ya Dunia hali hiyo inakadiriwa kusababisha wanafunzi hao kukosa shule kwa siku milioni 33 kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa miundombinu bora ya maji safi na salama.

Enable Notifications OK No thanks