Gharama ya uhai: Ukosefu wa zanahati unavyohatarisha maisha Maswa
- Wakazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa waanza jitihada za ujenzi wa zahanati kuokoa maisha.
- Ukosefu wa zahanati umeongeza gharama za maisha kwa Watanzania wengi.
Maswa, Simiyu. Maria Daudi mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa bado anakumbuka mkasa uliomkuta mwaka 2019 baada ya kushikwa na uchungu usiku wa manane.
Kwa kuwa anapoishi hapana huduma ya afya, Maria (40) alilazimika usiku huo huo kusaka usafiri wa kumpeleka katika kituo cha afya cha jirani aende kujifungua mwanaye wa tano. Mambo hayakuwa kama alivyotarajia.
Akiwa njiani kuelekea Kituo cha Afya cha Isanga kwenye bodaboda uchungu ulizidi na kujifungulia njiani, shukran kwa mkunga wa jadi aliyekuwa ameongozana naye katika safari hiyo kuokoa maisha yake na mtoto.
Maisha ni yale yale
Miaka miwili baadaye Maria haoni ahueni. Akiwa na ujauzito wake wa sita mambo ya kawa yale yale lakini safari hii aliwahi kidogo.
“Uchungu ulianza Saa nane za usiku ilinichukua muda mrefu kupata pikipiki ya kunipeleka huko Isanga…nilitumia Sh15,000 kufika hospitali,” anasema Maria ambaye hadi tunakutana naye Februari 24, 2022 alikuwa ana siku nne tu tangu atoke kujifungua mtoto wa sita.
Kati ya wato hao sita, Maria anasema mtoto mmoja alijifungulia nyumbani na mmoja njiani.
Ukosefu wa huduma za uhakika za afya zinaangamiza maisha ya mama na mtoto katika nchi nyingi zinazoendelea duniani ikiwemo Tanzania.
Licha ya Serikali kuendelea kupeleka huduma za afya vijijini bado baadhi ya vijiji nchini vikiwemo Mwamihanza, Buhungukira, Bushitara na Zabazaba wilayani Maswa katika mkoa wa Simiyu havina huduma hiyo.
Wanavijiji wa maeneo haya, ambao husafiri umbali mrefu kupata huduma za afya, sasa wameweka ujenzi wa zahanati katika mipango kazi yao badala ya kusubiria Serikali kuwaanzishia safari hiyo.
Baada ya kutaabika kwa muda mrefu, wakazi wa Kijiji cha Mwamihanza wameweka ujenzi wa Zahanati kama moja ya vipaumbele vyao vikuu. Tayari wameshashusha mawe kwa ajili ya kuanza kujenga boma. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Ni maumivu juu ya maumivu
Ukosefu wa zahanati katika vijiji hivyo vinaongeza gharama za maisha za wajawazito na akina mama wenye watoto kwenda kupata huduma za kliniki katika vijiji vya jirani.
“Bodaboda kukuchukua kwenda kliniki Isanga anakuchaji Sh15,000 hivyo kwenda na kurudi inakuwa ni Sh30,000,” anasema Maria ambaye anasema kipato chake hakiendani na gharama hizo.
Bodaboda katika kijiji hiki hupandisha bei za usafiri kuwabeba wajawazito kwa kuwa huona ni fursa ambayo mgonjwa hawezi kubishia kwa mujibu wa Maria Laurent, Mkazi wa Mwamihanza.
“Wakishaona mjamzito huwa wanajua huyo siyo mgonjwa wa kawaida lazima fedha itapatikana tu…huwa tunatumia fedha nyingi sana kwenda hospitali ikiwa ni usiku huwa inatugharimu hadi Sh30,000 kwa safari moja kwa bodaboda tu,” anasema.
Laurent anasema kutokana na kijiji chao kutokuwa na wenye bodaboda wengi, huduma hiyo ya usafiri huwa inachukuliwa kijiji jirani cha Isulilo kilichopo kama kilomita tano kutoka Mwamihanza.
Baadhi ya wanakijiji wa Mwamihanza wasio na uwezo wa kifedha hutembea kwa miguu kutoka kijijini kwao hadi Kijiji cha Isulilo ili kupata usafiri wa umma ambao si ghali sana kuliko bodaboda. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Masharti ya huduma ya afya vs kipato
Kwa kwa kawaida, Wizara ya Afya inashauri mama mjamzito kuhudhuria kituo cha afya mara nne na zaidi ili madaktari waweze kumpatia huduma stahiki na siku za mwisho anatakiwa kwenda haraka iwezekanavyo ili ajifungulie mikononi mwa watalaamu.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania mwaka 2015/16 inabainisha kuwa idadi ya wanaojifungulia vituo vya afya na kwa msaada wa watu wenye ujuzi inazidi kuongezeka Tanzania mwaka hadi mwaka.
Ripoti ya utafiti huo iliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar (OCGS) inaonyesha kuwa mwaka 2015/16 asilimia 63 au watoto sita kati ya 10 walizaliwa kwenye vituo vya afya ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 50 au nusu ya watoto waliofanyiwa utafiti mwaka 2010.
“Ingawaje huduma ya mama mjamzito inapatikana kwa kiwango cha juu, ni asilimia 24 tu (takriban robo) ya wanawake ndio walikuwa wamehudhuria kliniki katika mwezi wa nne wa ujauzito wao kama inavyoshauriwa na nusu (asilimia 51) ya wanawake wajawazito walitembelea sehemu za kutolea huduma ya afya mara nne au zaidi katika kipindi chao cha ujauzito,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, mapema Aprili 2022 wakati wa uzinduzi wa huduma ya M-Mama jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alieleza kuwa idadi ya wanawake wajawazito wanaohudhuria mara nne na zaidi imeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2015/16 hadi asilimia 93.
Hii ina maana kuwa idadi ya wanauhudhuria kliniki wakati wa ujazito imepanda kutoka watano kati ya 10 mwaka 2015/16 hadi tisa kati ya 10 mwaka huu.
Safari hii ya kufuata huduma ya mama mjamzito mara kwa mara ni maumivu kwa wasio na kipato hasa wanaoishi vijijini ambapo huduma za afya zinapatikana umbali mrefu.
Ukosefu wa huduma za afya waongeza umaskini
Maria anasema kipato chake ni wastani wa Sh50,000 kwa mwezi wakati wa masika na wakati wa kiangazi akiuza mazao huwa kidogo angalau anapata Sh100,000 kwa mwezi kwa miezi michache tu ya mwanzo ya mavuno.
Hii ina maana iwapo mjamzito mwenye kipato kama cha Maria cha wastani wa Sh100,000 kwa mwezi atafuata masharti ya kwenda kliniki kutoka kijijini kwao angalau mara moja kwa mwezi, atatumia wastani wa takriban theluthi ya kipato chake kupata huduma ya mama na mtoto jambo linalowarudisha katika vita ya kuung’oa umaskini.
Kituo cha Afya cha Isanga kipo takriban kilomita 17 kutoka Kijiji cha Mwamihanza.
Safari ya kutoka katika Kijiji cha Mwamihanza kwenda kupata huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Isanga wilayani Maswa huwagharimu wakazi wa kijiji hiki kiasi cha fedha kisichopungua Sh20,000 kwa pikipiki kwenda na kurudi. Picha|Google.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa wanawake ambao hawana elimu, wanawake waishio maeneo ya vijijini na wanaotoka kaya maskini sana kama Maria wana uwezekano mkubwa wa kujifungulia nyumbani.
“Tunaomba tu Serikali ituletee zahanati ili na sisi tusiwe tunazalia njiani na tusipate shida tena,” anasema Maria.
Gharama hizo na shuruba nyingine zimewafanya wanakijiji wa Mwamihanza kuweka ujenzi wa zahanati kijijini kwao kama moja ya vipaumbele vikubwa.
Tayari kijiji hicho kimefanikiwa kupata eneo karibu na Shule ya Msingi Mwamihanza ambapo wanajamii watachangia nguvukazi, kokoto, mawe, mchanga na maji pale ujenzi wa boma la zahanati utakapoanza.
“Wanakijiji cha Mwamihanza waliona ujenzi za zahanati ni kipaumbele namba moja,” anasema Dominic Richard, Mraghbishi kutoka kijiji hicho cha Mwamihanza.
Serikali yaahidi kutatua tatizo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa Vivian Christian anasema Serikali itamalizia miradi yote iliyoanzishwa na wananchi zikiwemo zahanati na madarasa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Ukosefu wa huduma madhubuti za afya ni moja ya changamoto zinazoikumbuka Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inayokabiliwa na uhaba wa rasilimali fedha.
Soma zaidi:
- Manahodha wakwepa mamba wanaoipiga jeki elimu Tanzania
- Haina kusubiri: Wanavijiji walivyoamua kupunguza wanafunzi 100 darasa moja
“Niwaahidi Watanzania kujenga kwa kasi mfumo wa huduma bora za afya…tumeanza na ujenzi wa miundombinu ambapo vituo kadhaa katika ngazi ya vijiji, kata, wilaya, mkoa na zile hospitali za rufaa na kazi ya ujenzi inaendelea,” alisema Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua huduma ya mfumo wa M-Mama unaolenga kuboresha huduma za mama na mtoto nchini.
Rais Samia anasema Serikali inaendelea kuajiri watumishi katika sekta ya afya baada ya mwaka jana kuajiri watumishi 3,600 na wanatarajia kuongeza wengine kati ya ajira 32,000 zitakazotolewa mwaka 2022.
Kiongozi huyo wa juu wa nchi anasema licha ya kuboresha huduma za afya bado kuna kina mama wajawazito wanafariki wakati wa kujifungua kwa sababu ya kutokuwepo kwa taarifa za haraka ili kutoa usafiri wa kumfikisha mapema kwenye kituo cha afya kupata huduma.
“Serikali inajitahidi kuhakikisha kila kata angalau ambulance moja. Tumeagiza ambulance 233 za kawaida ambazo zitamwagwa Tanzania nzima na ambulance 25 za ngazi ya juu zenye huduma sawa na kituo cha afya,” anasema Rais Samia.
Latest
