Kasi ya mfumuko wa bei yang’ang’ania kiwango cha Agosti
- Mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba, 2023 umesalia kuwa asilimia 3.3.
- Kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula kwatajwa kama sababu.
- Kasi ya mfumuko wa bei yapungua Uganda na na kupaa nchini Kenya.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia Septemba 2023 imebaki asilimia 3.3 sawa na kiwango kilichorekodiwa mwaka unaoishia Agosti mwaka huu.
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Oktoba 9, 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inasema hali hiyo imechangiwa zaidi na kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula.
“Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2023 kuwa sawa na mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2023 umechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula,” imesema taarifa ya NBS.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa kasi ya mfumuko wa bei kusalia kiwango kimoja hali inayotoa ahueni kwa walaji ambao walikuwa wakilazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kumudu gharama za mahitaji ya msingi ikiwemo bidhaa za chakula.
Itakumbukwa kuwa kiwango cha kasi ya mfumuko wa bei kilichoripotiwa kwa mwezi Julai, Agosti na Septemba ndio kiwango kidogo zaidi kilichowahi kurekodiwa ndani ya mwaka mmoja.
Mara ya mwisho kasi ya mfumuko wa bei wa taifa wa asilimia 3.3 iliripotiwa katika mwaka ulioishia Aprili na Mei, 2021 na tangu wakati huo mfumuko wa bei ulikuwa ukipanda na kushuka lakini haukuwahi kushuka zaidi ya kiwango hicho.
Soma zaidi:Upotevu wa chakula unavyochangia baa la njaa duniani
Bidhaa zilizochangia mfumuko wa bei kusalia pale pale
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023 ni pamoja na ngano, mkate, nyama, mayai,samaki wabichi, dagaa, ndizi za kupika, mafuta ya kupikia, na njegere.
Hata hivyo, mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za chakula umepungua ikilinganishwa na mwaka ulioishia Agosti, 2023 zikiwemo nguo za wanaume, vinywaji vikali na tumbaku, nguo za watoto, viatu vya wanawake, viatu vya watoto, nishati ya gesi, nishati ya mkaa,nishati ya kuni, na samani za nyumbani.
Aidha, NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Septemba, 2023 umesalia kuwa asilimia 5.6 ikiwa ni sawa na ule uliorekodiwa mwaka ulioishia Agosti, 2023.
Kwa upande wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Septemba, 2023 umesalia kuwa asilimia 2.4 ikiwa ni kiwango sana na mwaka unaoishia Agosti, 2023.
Soma zaidi:Afrika inavyoweza kukabiliana na baa la njaa
Vilio, ahueni nchi jirani
Wakati mfumuko wa bei ukisalia kiwango kile kile nchini, nchi jirani nazo zimepata ahueni na vilio mara baada ya viwango vya mfumuko wa bei kupanda na kushuka.
Nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Septemba, 2023 umeongezeka hadi asilimia 6.8 kutoka asilimia 6.7.kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023.
Wakati Kenya ikipata maumivu, walaji nchini Uganda wamepata ahueni mara baada ya mfumuko wa bei kushuka hadi asilimia 2.7 kutoka asilimia 3.5 mwaka ulioishia Agosti, 2023.