Mfumuko wa bei washuka baada ya kung’ang’ania kiwango kimoja miezi miwili
- Wapungua na kufikia asilimia 3 kutoka asilimia 3.2.
- Kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula kwatajwa kama sababu.
- Kasi ya mfumuko wa bei yapungua Kenya na huku Uganda ikibaki pale pale.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia Disemba 2023 imepungua hadi asilimia 3 kutoka asilimia 3.2 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Novemba 2023.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Kasi hiyo ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Disemba 2023 imepungua baada ya kung’ang’ania kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo yaani asilimia 3.2
Soma zaidi : Maumivu vifaa vya shule vyapanda bei Mwanza
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Disemba 8, 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inasema hali hiyo imechangiwa zaidi na kupungua kwa bei ya bidhaa za chakula.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2023 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Disemba, 2023 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2023,” imebainisha taarifa ya NBS.
Bidhaa zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Disemba 2023, ni pamoja na ngano, mchele, nyama, mayai, samaki wabichi, dagaa, ndizi za kupika, mafuta ya kupikia, na njegere.
Bidhaa zisizo za vyakula ambazo mfumuko wake wa bei umepungua ni huduma ya chakula na vinywaji kwenye mahoteli na migahawa na kuni.
Soma zaidi : Umemejua unavyowaokoa wafugaji na ukame Dodoma
NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Disemba, 2023 nao umepungua hadi asilimia 2.3 kutoka asilimia 3.7 uliorekodiwa mwaka ulioishia Novemba, 2023.
Kwa upande wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Disemba, 2023 umeongezeka kidogo na kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3 iliyorekodiwa mwaka ulioishia Novemba, 2023.
Ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mfumuko wa bei, Januari Mosi 2024, Serikali ilitangaza kutoa kibali cha kuagiza tani 50,000 za sukari kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yake ambapo bei ya bidhaa hiyo ilipanda hususan katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha.
Ahueni nchi jirani
Wakati mfumuko wa bei ukipungua kidogo nchini, pia ahueni imeshuhudiwa katika nchi jirani za Africa Mashariki.
Nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Disemba, 2023 umepungua hadi asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.8 kwa mwaka ulioishia Novemba, 2023.
Mfumuko wa bei nchini Uganda umesalia katika kiwango cha mwezi uliopita cha asilimia 2.6.