Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Agosti 2024 

October 8, 2024 6:39 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  •  Wasalia asilimia 3.1 kiwango kilichokuwepo mwaka unaoishia mwezi Agosti 2024.

Arusha. Kasi ya mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2024 imebakia kuwa asilimia 3.1 sawa na kiwango kilichorekodiwa mwaka unaoishia Agosti mwaka huu.

Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Oktoba 10, 2024 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa hali hiyo imechangiwa na kupungua na kuongezeka kwa kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa.

“Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2024 kuwa sawa na kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula,” imesema taarifa ya NBS.

Kwa mujibu wa NBS, hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2024 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024.

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 ni pamoja na mchele kutoka asilimia 5.3 hadi asilimia 2.5, mtama kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 4.1 na mikate na bidhaa nyingine za kuoka kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 1.4.

Aidha, bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024 ni pamoja na pikipiki mpya kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 11.1, spea za vyombo vya usafiri kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 4.5.

Bidhaa nyingine ni zile za usafi wa mwili ambazo zimeongezeka kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 5.6 na mabegi ya shule kutoka asilimia 6.2 hadi asilimia 9.8.

Ahueni Kenya, Uganda

Wakati kasi ya mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma nchini Tanzania uking’ang’ania kiwango cha awali, nchini Kenya na Uganda ni ahueni kiduchu baada ya kiwango hicho kushuka.

Katika mwaka unaoishia mwezi Septemba 2024 mfumuko wa bei nchini humo umepungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.5 iliyorekodiwa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024, huku nchini Kenya mfumuko huo ukipungua hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 4.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2024. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks