Mfumuko wa bei waendelea kushuka Tanzania
- Umeshuka kwa asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.6 iliyorekodiwa Juni 2023
- Bidhaa za vyakula zachangia kushuka kwa mfumuko wa bei.
- Ahueni hadi katika Nchi za Kenya na Uganda.
Dar es Salaam. Kasi ya bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2023 ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za chakula.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai, 2023 umepungua kutoka wa asilimia 3.6 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Juni hadi asilimia 3.3 iliyorekodiwa mwaka unaoshia mwezi Julai, 2023.
Kuendelea kushuka kwa kasi ya mfumuko wa bei kunaenda kutoa ahueni kwa walaji ambao walikuwa wakilazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kumudu gharama za msingi za bidhaa na huduma kama chakula.
“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma
kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2023 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023,” imesema taarifa ya NBS iliyotolewa leo Agosti 9, 2023.
Kiwango cha chini ndani ya mwaka mmoja
Uchambuzi wa takwimu hizo za NBS uliofanywa na Nukta Habari unabainisha kuwa kiwango hicho kilichorekodiwa Julai mwaka huu ndio kiwango kidogo zaidi kilichowahi kurekodiwa ndani ya mwaka mmoja.
Mara ya mwisho kasi ya mfumuko wa bei wa taifa wa asilimia 3.3 iliripotiwa katika mwaka ulioishia April na Mei, 2021 na tangu wakati huo mfumuko wa bei ulikuwa ukipanda na kushuka lakini haukuwahi kushuka zaidi ya kiwango hicho.
Baadhi ya bidhaa zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei Julai mwaka huu ni pamoja na ngano, mchele, mahindi, unga wa mahindi unga wa ngano, samaki, dagaa wabichi, viazi mviringo, dagaa wakavu mkate na bidhaa za kuoka pamoja na bidhaa za mafuta ya kupikia.
Soma zaidi
- Rais Samia apiga marufuku uuzwaji holela wa mazao, azitaka Wizara kuandaa mfumo maalum
-
Bajeti ya Wizara ya Kilimo yaongezeka kwa asilimia 29
NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2023 nao umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka ulioishia Juni, 2023.
Kwa upande wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai, 2023 umeongezeka hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023.
Ahueni hadi nchi jirani
Wakati Watanzania wakipata ahueni ya mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma mbalimbali, nchi jirani ikiwemo Kenya na Uganda nazo zimepata ahuenibaada ya mfumuko huo kushuka katika nchi zao.
Nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Ju;ai, 2023 umepungua hadi asilimia 7.3 kutoka asilimia 7.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023.
Kupanda kwa bei za bidhaa na huduma nchini Kenya ni miongoni mwa masuala yaliyochochea maandamano yaliyoongozwa na upinza wa Umoja wa Azimio siku za hivi karibuni kushinikiza serikali ya Rais William Ruto kuondoa baadhi ya kodi zitakazopunguza maumivu hasa kwa watu wenye kipato cha chini.
Kwa mujibu wa NBS nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2023 umepungua hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023.