Jua lachomoza sekta ya utalii: Tanzania yaripoti ongezeko la watalii zaidi ya 90,000

May 26, 2022 9:10 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kupungua kwa maambukizi ya Corona ulimwenguni
  • Kati ya Januari na Aprili, wataliii 367,632 waliingia Tanzania.
  • Filamu ya “Royal Tour” kuvuta zaidi watalii.

Dar es Salaam. Hatimaye matumaini yameanza kuonekana katika sekta ya utalii Tanzania mara baada ya kuongezeka kwa idadi ya watalii kwa asilimia 33.6 katika kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na kupungua kwa janga la Corona (Uviko-19), huku idadi hiyo ikitegemewa kuongezeka zaidi.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika taarifa yake kuhusu watalii wanaotembelea Tanzania iliyotolewa Mei 19, 2022 imeeleza kuwa kati ya Januari na Aprili wataliii 367,632 waliingia Tanzania.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la watalii 92,535 kutoka watalii 275,097 waliotembelea vivutio vya Tanzania katika kipindi kama hicho mwaka jana. 

Kati ya watalii walioingia nchini, 124,212 waliingia kupitia Zanzibar sawa na zaidi kidogo ya theluthi moja ya watalii wote walioingia Tanzania.

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, Februari ndiyo ulirekodi kiwango cha juu cha watalii ambapo waliiingia watalii 100,936 huku Aprili wakiingia wachache zaidi kuliko miezi mingine. 

NBC imeeleza kuwa kuongezeka kwa watalii hao ni matokeo ya kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Uviko-19 na Tanzania kujitangaza zaidi duniani.

“Ongezeko la idadi ya watalii limetokana na kuondolewa kwa marufuku ya kusafiri kufuatia kupungua kwa maambukizi ya Uviko-19 katika nchi nyingi duniani na juhudi zinazoendelea za Serikali kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi,” imeeleza NBS katika taarifa yake.


Zinazohusiana: 


Sekta ya utalii nchini ilipitia kipindi kigumu cha ukata wa watalii tangu ulipotokea mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 mwishoni mwa mwaka 2019 na kusababisha mataifa mengi kuweka sheria kali ikiwemo zuio la safari za kimataifa.

Mwaka 2019, kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania ilipokea watalii milioni 1.5 ambapo idadi ilishuka zaidi mwaka uliofuata hadi watalii 620,867. 

Hata hivyo, mwaka 2021 idadi ya watalii iliongezeka hadi 922,692 baada ya kulegezwa kwa masharti ya safari za kimataifa.

Matumaini zaidi

Pamoja na ongezeko hilo la watalii, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi siku zijazo kutokana na jitihada za Serikali kutangaza vivutio vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama.

Filamu ya Tanzania ya “Royal Tour” inayoonyesha vivutio vya utalii vilivyopo nchini itasaidia kuongeza watalii.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,  sekta utalii huchangia wastani wa  asilimia 17 ya pato la Taifa na  asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Huzalisha ajira takriban milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka na huchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda, biashara, kilimo, mifugo na usafirishaji


Tangazo:


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW