Jinsi ya kujikinga na Corona unapotumia lifti
- Vaa barakoa yako pale unapoingia kwenye lifti.
- Nawa mikono yako na maji tiririka na sabuni kabla na baada ya kuingia kwenye lifti au tumia vitakasa mikono.
- Usipande kwenye lifti ambayo ina watu wengi.
Dar es Salaam.Licha ya kuwa ugonjwa wa Corona amepungua kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania, bado wananchi wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo aina ya COVID-19.
Ugonjwa huo hauchagui umri, rangi wala eneo utakalokupata.
Eneo mojawapo unalotakiwa kuchukua tahadhari ni wakati ukitumia lifti (elevators) zilizopo katika majengo marefu ya ofisi na biashara.
Licha ya kuwa lifti hurahisisha kazi ya kuwapandisha na kuwashusha watu kwenye majengo marefu, zisipotumika vizuri zinaweza kuwa chanzo cha kuambukizana COVID-19.
Kila unapoingia kwenye lifti itakulazimu kubonyeza kutufe cha ghorofa unayoenda. Picha| Forbes.
Ni tahadhari zipi unapaswa kuzingatia wakati unatumia lifti?
Nawa au takasa mikono yako baada na kabla ya kuingia kwenye lifti
Kila unapoingia kwenye lifti itakulazimu kushika sehemu mbalimbali ikiwemo vitufe vinavyokusaidia kufika ghorofa unaloenda.
Hali hiyo inaweza kukuweka katika hatari ya kupata maambukizi kwa sababu vitufe hivyo hushikwa na watu wengi.
Pia usiguse sehemu zingine za lifti kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo.
Ni muhimu kunawa mikono yako kwa maji safi na tiririka pamoja na sabuni au kutumia vitakasa mikono vilivyokidhi vigezo vya ubora.
Hata baada ya kunawa mikono epuka kugusa pua, mdomo na macho yako.
Tumia barakoa yako
Vaa barakoa unapokuwa kwenye lifti ili kuzuia maambukizi kwa sababu ugonjwa huo huenezwa kwa maji maji yanayotoka kwa mgonjwa anayepiga chafya, kukohoa au kuongea.
Barakoa itakusaidia kuzuia maji maji kukufikia na hivyo kukuweka salama dhidi ya virusi hivyo.
Zinazohusiana
- Usidanganyike nzi hawaenezi ugonjwa wa Corona
- Ni uzushi: Huwezi kupata maambukizi ya Corona kwa kuchangia damu
- Ukweli kuhusu maiti kuambukiza Corona
Zingatia umbali wa mita moja
Kanuni ya kukaa umbali wa mita moja na mwenzako bado inafanya kazi hata kwenye lifti. Unashauriwa usipande lifti yenye watu wengi ili muachiane nafasi kati ya mtu na mtu.
Kama lifti imejaa, tumia mbadala wa kutembea kwa miguu ili kupanda ngazi za jengo.
Hii siyo tu itakuepusha na msongamano wa watu kwenye lifti bali itaimarisha afya yako kwa sababu ni sehemu ya mazoezi.
Usiende sehemu zenye mikusanyiko
Kama unaweza kutulia nyumbani au ukifika ofisini ni jambo jema kwa sababu unajiweka katika nafasi nzuri ya kujikinga na Corona.
Epuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwa sababu unakutana na watu wengi na uwezekano wa kukaa umbali wa mita moja unakuwa mdogo ikilinganishwa na nyumbani au ofisini.
Unaambiwa Corona bado ipo, chukua tahadhari jikinge na wengike na wengine.
Umepata ujumbe, video au picha uliyo na mashaka nayo kuhusu Corona? Tutumie kupitia mitandao yetu ya kijamii. Facebook na Twitter, @NuktaFakti, Instagram @nuktafakti
Latest
