Ni uzushi: Kupiga mbizi kwenye maji hakusababishi Corona
- Bado haijathibitishwa kisayansi kwamba maeneo ya kuogelea ni njia ya mtu kupata Corona.
- Unashauriwa kuendelea kuchukua tahari ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara.
Dar es Salaam. Licha ya kuwa kuogelea (kupiga mbizi) kwenye mabwawa au baharini ni moja ya burudani inayoweza kumfanya mtu ajisikie vizuri, baadhi ya watu wameacha kuogelea kwa kuogopa kupata maambukizi ya COVID-19.
Hata hivyo, dhana hiyo ambayo inalenga kuleta taharuki kwa watu, haina ukweli wowote kwa sababu bado haijathibitishwa kisayansi.
Maeneo ya kuogelea siyo njia ya moja kwa moja kumsababishia mtu kupata COVID-19 ikizingitiwa kuwa ugonjwa huo unaenezwa kwa njia ya kugusana au kugusa maji maji yanayotokana na kikohozi au chafya ya mtu mwenye virusi hivyo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limewatoa hofu watu wanoapenda kuogelea na kuwataka kuendelea kupata burudani hiyo huku wakichukua tahadhari zinazohitajika kujikinga na ugonjwa huo.
Soma zaidi:
- ‘Famba’: Matunda, mboga mboga havisababishi Corona
- Ni uzushi: Huwezi kupata maambukizi ya Corona kwa kuchangia damu
Tahadhari ambazo zinapendekezwa ni kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja na mwingine, jambo ambalo linaweza kuzingatiwa na waogeleaji.
Nyingine ni kuvaa barakoa, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara.
“Virusi vya Corona havisambazwi kwa maji unapoogelea. Hata hivyo virusi husambaa mtu anaposegea karibu na mtu mwenye Corona,” WHO inaeleza katika moja ya miongozo ya kudhibiti ugonjwa huo.