Mdogo mdogo: Mwanza yatafuna mfupa uhaba wa madawati shuleni
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala (katikati) akiwa na wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Buswelu baada ya kukabidhi madawati katika shule hiyo. Picha |Mariam John.
- Halmashauri ya Ilemela yakabidhi madawati 1,525 shule za msingi.
- Hatua hiyo itasaidia kupunguza uhaba wa madawati katika wilaya hiyo.
- Wilaya hiyo ina mpango wa kumaliza tatizo la madawati fikapo Septemba mwaka huu.
Mwanza. Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala amekabidhi madawati 1,525 ambayo yatatumiwa na wanafunzi 4,575 katika shule za msingi wilayani humo ikiwa ni jitihada za uongozi wa wilaya na wadau mbalimbali katika kuhakikisha watoto wanasoma kwenye mazingira bora.
Madawati hayo yalipatika kwenye hafla fupi iliyokuwa imeandaliwa na mkuu huyo wa wilaya iliyofanyika Mei 31 mwaka huu ambapo wadau wa sekta ya elimu waliahidi kuchangia madawati 2,000 pamoja na fedha taslimu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Massala amesema wilaya ya Ilemela inakabiliwa na upungufu wa madawati 5,838.
“Tumeona ipo haja ya kupunguza changamoto hiyo ya upungufu wa madawati kwa kufanya kampeni za uchangiaji ili kupunguza upungufu wa madawati ambao unaikabili halmashauri hiyo,” amesema Massala
Madawati hayo 1,525 yametengenezwa kwa Sh100 milioni, fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Amesema kupatikana kwa madawati hayo kutapunguza uhaba wa madawati 4,000 na kwamba hadi kufikia Juni wamelenga kumaliza changamoto hiyo.
Moja ya mikakati ya kupunguza changamoto hizo ni kuanzisha mbio za “Dawati Marathon” Septemba mwaka huu kwa ajili ya uchangiaji wa madawati hayo.
“Kama unaona elimu ni gharama kubwa sana jaribu ujinga,sisi tumeona tusijaribu ujinga lazima tuwekeze katika elimu, megawanyika katika maeneo mengi tuna elimu msingi, sekondari mpaka chuo,” ameeleza Massala.
Hata hivyo, wanafunzi waliozungumza na Nukta habari wamesema uwepo wa madawati utasaidia kusoma vizuri na kutimiza malengo yao.
“Tunaishukru Serikali kwa kutuletea madawati ambayo yatatusaidia kujifunza kwa bidii,” amesema Juliana Antony mwanafunzi shule ya msingi Buswelu.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Fatuma Karoli ametumia fursa hiyo kuwapongeza wadau wote ambao wamejitolea fedha zao katika utengenezaji wa madawati hayo.
Meneja wa Benki ya Stanbic tawi la Mwanza, Geofrey Makondo amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa maono na usimamizi wake ambao umefanikisha watoto kupata madawati.
“Nakushukuru kwa sababu unayoyafanya ni kwa ajili ya Taifa naamini watoto hawa kwa kupata madawati watasoma vizuri na uelewa utaimarika,” ameeleza Makondo.
Latest