Wasiowapeleka watoto kidato cha kwanza kusakwa nyumba kwa nyumba
- Serikali kuwakamata na kuwachukulia hatua wazazi ambao watoto hawajaripoti shule.
- Mkoa wa Mwanza wasema wanafunzi walipoti shule hata kama hawana sare.
Mwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imetoa wiki mbili kwa wanafunzi 1,515 wa kidato cha kwanza ambao bado hawajaripoti kufanya hivyo, kabla hatua kali hazijachukuliwa kwa wazazi wao.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Masala akizungumza leo Februari 2, 2023 kwenye kikao kazi ametoa agizo hilo huku akitaka shule ambazo zina idadi kubwa za wanafunzi ambao hawajaripoti kuhakikisha wanaripoti.
Amesema wilaya ilifaulisha wanafunzi 12,500 lakini mpaka sasa wanafunzi 1,515 wa kidato cha kwanza hawajaripoti.
“Hadi kufikia Februari 1, jumla ya wanafunzi 11,458 walikuwaa wameripoti shule ambayo ni sawa na asilimia 90.46 kati ya hao wavulana ni 5, 585 na wasichana ni 5,873,” amesema Masala.
Akizungumzia uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali, mkuu huyo wa wilaya amesema mpaka kufikia Februar 1, jumla ya wanafunzi 7,706 wa darasa la awali walikuwa wameandikishwa sawa na asilimia 103 na wanafunzi wa darasa la kwanza 11,221.
Hata hivyo, Afisa elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi amesema mkakati uliopo ni kuwakamata wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shule na kuwachukuliwa hatua za kisheria.
Ametoa agizo hilo kwa watendaji wa kata kuhakikisha wanawakamata wazazi ambao hawajapeleka watoto wao shule na wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ya maotea ya elimu.
“Tumetangaza kuanzisha msako kwa wazazi wote ambao wameshindwa kuwapeleka watoto wao shule wakamatwe na wachukuliwe hatua,” amesema Nkwabi.
Alipoulizwa iwapo suala la sare za shule kuwa ndiyo kikwazo cha watoto kutoendelea na masomo amesema hiyo sio sababu kama mtoto hana sare aende hivyo hivyo wakati mzazi akijipanga kumnunulia.
“Suala la sare lisiwe kikwazo japokuwa tunasisitiza kwa kuwa sare ndio mlinzi wa mtoto hasa kwenye wakati huu ambao kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia hivyo mbakaji hawezi kwenda na mtoto chumba cha kulala wageni akiwa na sare za shule atakamatwa,” amesema Nkwabi.
Latest