Tozo miamala ya simu: Serikali haijafikia lengo, wadau watoa suluhu

January 22, 2023 9:39 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ilipanga kukusanya Sh1.23 trilioni lakini imekuwanya Sh447.5 bilioni ndani ya miezi 15.
  • Punguzo la tozo na ukali wa maisha wachangia lengo kutofikiwa.
  • Wadau washauri Serikali kubuni vyanzo vya uhakika vya mapato.

Dar es Salaam. Wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hawatakuwa na hofu ya kukosa sehemu ya kusomea, baada ya halmashauri hiyo kuwajengea madarasa yatakayokidhi mahitaji yao. 

Manspaa hiyo iliyopo mkoani Mwanza imefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa 110 vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya wanafunzi hao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Mhandisi Modest Apolinary anasema walipokea Sh2.2 bilioni kutoka Serikali Kuu kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo, ofisi tatu za walimu na ununuzi wa viti na meza 5,500. 

“Lengo ni kuwawezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023, kupata nafasi na kuanza masomo kwa wakati pamoja na kuwa na mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia,” anasema Alponary baada ya kukabidhi vyumba hivyo hivi karibuni. 

Miongoni mwa fedha zilizotumika kujenga madarasa hayo zimetokana na tozo ya miamala ya simu ambayo imeibua mjadala mpana katika jamii tangu ianzishwe mwaka 2021. 

Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya mwaka 2021 ndiyo ilianzisha tozo kwenye miamala ya pesa kwa simu kuanzia Julai mwaka jana.

Serikali ingeweza kujenga madarasa mengi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini  na kuboresha miundombinu mingine ya kutolea huduma za kijamii kwa kutumia mapato ya tozo kama ingepata muitikio chanya kutoka wananchi. 

Kutokana na maoni tofauti ya wananchi, Serikali imeshindwa kufikia kiwango cha makusanyo ya mapato ya tozo iliyojiwekea tangu kuanzishwa kwake mwaka jana. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha na Mipango, kati ya Julai 2021 hadi Septemba 2022, Serikali iliweka lengo la kukusanya tozo za Sh1.23 trilioni lakini imefanikiwa kukusanya Sh447.5 bilioni.

Hiyo ni sawa na asilimia 36.3 ya lengo la makusanyo yote katika kipindi hicho cha miezi 15 tangu kuanzishwa kwa tozo hiyo. 

Wakati Serikali inaanzisha tozo hiyo,  ilijiwekea lengo la kukusanya Sh228.1 bilioni kati ya Julai hadi Septemba 2021 (robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2021/2022) lakini iliishia kukusanya Sh64.4 bilioni tu.

Hata miezi iliyofuata katika kipindi hicho, matarajio hayakufikiwa. Mathalan, Julai hadi Septemba 2022 (robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2022/23), lengo lilikuwa ni kukusanya Sh215.1 bilioni lakini Sh89 bilioni ndiyo zilikusanywa sawa na asilimia 41.4 ya lengo.

Licha ya kuwa Serikali haijawahi kufikia lengo la makusanyo ya tozo, makusanyo hayo yaliyokusanywa hayajawahi kuvuka asilimia 50 au nusu ya lengo kwa kila robo mwaka, jambo ambalo linaloweza kutoa tafsiri kuwa tozo haikupata muitikio mzuri kwenye jamii. 

Sababu za zilizochangia kutofikia malengo

Tangu kuanzishwa kwa tozo, kumekuwa na maoni tofauti huku baadhi ya watu wakipinga kuwa inambebesha mzigo na kumuongezea ukali wa maisha mwananchi wa kawaida ambaye analipa kodi.

Septemba 2022, Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), kilifungua shauri la kupinga tozo za miamala ya kielektroniki katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

LHRC iliiomba mahakama iruhusi kituo kiwasilisha maombi ya kufanya mapitio ya kimahakama ili kutengua kanuni za tozo kwa muda kwa sababu hazikufuata kufuata utaratibu ulioainishwa ndani ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977. 

Kutokana na maoni ya watu wakiwemo wachumi na watetezi wa haki za binadamu, Serikali ilifanya mabadiliko kadhaa ya kanuni za kodi ili kupunguza viwango vya tozo ikiwa na lengo la kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha uliosababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa na vita kati ya Urusi na Ukraine. 

Tangu kuanzishwa kwake, kiwango cha tozo kilipunguzwa kwa asilimia 30 Septemba 2021 na kikapunguzwa tena Julai mwaka huu na hivyo kufanya punguzo la jumla la asilimia 60 ya kiwango cha kilichowekwa awali.

Septemba 20, 2022, Serikali ilipunguza tena tozo ya miamala ya simu na benki kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kwa kuzingatia makundi na gharama za miamala husika.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Nchemba aliyekuwa akitoa tangazo hilo bungeni jijini Dodoma alisema fedha zilizopungua katika tozo hizo zitafidiwa kwa kubana matumizi ya Serikali  ikiwemo mafungu ya chai, vitafunwa, misafara kwenye safari/ziara, mafunzo, semina, warsha na matamasha.

Kupunguzwa kwa tozo kwa viwango tofauti katika kipindi hicho cha miezi 15 kwa kiasi kikubwa kumechangia Serikali kutofikia lengo lake la makusanyo ya tozo.


Soma zaidi:


Ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza kati ya Juni na Julai 2022 uliolenga kukusanya  maoni ya wananchi kuhusu hali ya uchumi wa Taifa, na tozo za miamala ya fedha kupitia simu za mkononi inaeleza kuwa zaidi ya nusu au asilimia 57 ya wananchi hawakubaliani na tozo hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka jana. 

“Wananchi walio wengi hawakubaliani (asilimia 23) au hawakubaliani kabisa (asilimia 34) na tozo tangu ilipoanzishwa mara ya kwanza,” imeeleza ripoti hiyo ya Twaweza iliyotolewa Agosti 25, 2022.

Hata hivyo, wananchi walipoulizwa katika utafiti huo uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi Awamu ya Saba’, maoni yao kuhusu kupunguzwa kwa kiwango cha tozo, bado wananchi wengi zaidi hawakubaliani (asilimia 32) kuliko kukubaliana kwa asilimia 18 na mabadiliko hayo.

Utafiti huo ulikusanya maoni ya watu 3,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo kati yao watu 960 walipinga mabadiliko ya tozo hizo licha ya kupunguzwa huku watu 540 ambao ni sawa na asilimia 18 walikubaliana na mabadiliko ya tozo hizo.

“Miongoni mwa wale wanaokubali kwamba tozo hiyo ni njia muhimu ya kuongeza mapato kwa Serikali asilimia 26 kati yao wanasema viwango vya kodi hiyo ni kubwa” inaeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa tozo za miamala ina manufaa makubwa katika maendeleo ya nchi ikiwemo kuchagiza ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji.

“Serikali ilitumia jumla ya Sh147.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo kati ya fedha hizo, Sh117 bilioni sawa na asilimia 81.4 zilitokana na tozo ya miamala,” alisema Mwigulu bungeni Septemba 20 mwaka huu. 

Moja ya darasa lililozinduliwa hivi karibuni ambalo litatumika na wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemelea mkoani Mwanza. Baadhi ya pesa za ujenzi wa madarasa hayo zimetokana na tozo. Picha | Mariam John.

Tozo yaibua mjadala

Nayo makampuni yanayotoa huduma za simu hayakubaki salama na tozo baada ya kuripoti kupata hasara katika shughuli zao.

Mathalan, kampuni ya Vodacom Tanzania katika ripoti yake ya mwaka unaoishia Machi 31, 2022 inaonyesha kuwa ilipanga kukusanya Sh1.06 trilioni katika mwaka ulioisha Machi mwaka huu lakini kutokana na athari za tozo imepoteza 9.8% ya mapato na kukusanya Sh956 bilioni ambayo ni pungufu ya matarajio.

Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Jaji Mstaafu Thomas Mihayo katika ripoti hiyo amesema tozo hizo ziliongeza gharama za wateja kufanya miamala kwa kutumia simu za mkononi, hivyo kusababisha zaidi ya wateja milioni 1.3 kuacha kutumia huduma za M-Pesa.

Tuangalie vyanzo vingine vya mapato

Mchambuzi wa masuala ya elimu na jamii, Richard Mabala anasema ni wakati sasa kwa Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika shughuli zake ili kodi inayokusanywa ielekezwe katika miradi ya maendeleo kuliko kuendelea kutoza tozo za simu.

“Naamini tungepata nyingi zaidi (fedha za tozo) kwa kupunguza matumizi ya miungu na wateule.  Bilioni 447 ni sawa na Mavi-Eti (magari) mangapi?,” amehoji Mabala ambaye amekuwa akijihusisha na tafiti mbalimbali za masuala ya kijamii huku akisisitiza uwajibikaji kwa rasilimali za umma. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire imeiomba Serikali kuangalia upya suala la tozo katika bajeti inayokuja (2023/24) ili kuwasogeza zaidi watumiaji katika mfumo wa kidijitali utakaosaidia kupata mapato mengi.

Wadau wengine wa masuala ya uchumi wanapendekeza kuwa Serikali kutanua wigo wa kupata mapato hasa kubuni vyanzo vipya vya kodi ambavyo ni endelevu na visivyomuumiza mwananchi wa kipato cha chini.

“Serikali inapaswa kulitazama suala hili kwa kina na kubuni vyanzo vipya vya kodi ili ipate fedha nyingi kwa sababu walipa kodi ni wachache,” anasema Mchambuzi wa masuala ya uchumi Walter Nguma na kusisitiza kuwa tozo inaweza isilete matokeo makubwa katika uchumi.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV