Ulaji milo mitatu ya chakula bado kitendawili Tanzania
- Idadi ya wanaokula milo mitatu yashuka kwa asilimia 8.2.
- Mtanzania mmoja kati ya 10, anakula mlo mmoja wa chakula.
- Uviko -19, uhaba wa chakula baadhi ya maeneo vyatajwa kama sababu.
Dar es Salaam. Wakati wataalamu wa afya wakihimiza kula milo mitatu ya chakula kwa siku au zaidi ili kuwa na afya bora, hali ni tofauti nchini Tanzania kwani idadi ya watu wanaokula milo mitatu kwa siku imeshuka kwa asilimia 8.2.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kufuatilia Hali ya Kaya Tanzania (NPS) ya mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya Watanzania wanaokula milo mitatu imeshuka kutoka asilimia 71.2 mwaka 2014/15 mpaka asilimia 63 mwaka 2020/21.
Hii ni kumaanisha kuwa kati ya Watanzania kumi ni sita ndio wanaokula milo mitatu ya chakula au zaidi kwa siku.
Wakati idadi ya wanaokula milo mitatu au zaidi ikishuka, idadi ya wanaokula milo miwili hadi mmoja imeongezeka. Mathalani wanaokula mlo mmoja wameongezeka kutoka asilimia 0.6 mpaka 1.6 huku wanaokula milo miwili wakiongezeka kutoka 28.2 mpaka 35.4.
Uchambuzi wa takwimu uliofanywa na Nukta habari umebaini kuwa kwa mujjbu wa ripoti hiyo katika kila Watanzania kumi basi mmoja hula mlo mmoja tu wa chakula huku watatu kati ya 10 wakila milo miwili ya chakula.
Hata hivyo, hali ya ulaji wa chakula imeonekana mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini kuliko mjini kwani, Watanzania waishio mjini wana wastani mzuri zaidi wa kula milo mitatu kwa asilimia 74.8 huku vijijini wakiwa na asilimia 57.3.
Vivyo hivyo, idadi ya wanaokula mlo mmoja vijijini ni kubwa zaidi ambao ni asilimia 1.8 wakati mjini ni 1.2 huku asilimia ya wanaokula milo miwili vijijini ikiwa ni mara mbili zaidi ya wale waishio mjini.
Huenda hali hiyo imechangiwa na kuwepo kwa upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini hali iliyosababishwa na mtawanyiko wa mvua pamoja na visumbufu.
Soma zaidi
- Vyakula vinavyoimarisha kumbukumbu, uelewa wa kimasomo kwa watoto
- Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Chakula nchini ya mwaka 2020/21 imeeleeza kuwa pamoja na kuwa na ziada ya chakula halmashauri 17 kutoka mikoa nane nchini ilitarajiwa kukutana na uhaba wa chakula mwaka juzi.
“Upungufu huo umechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mtawanyiko mbaya wa mvua, visumbufu vya mimea kama vile wanyamapori, ndege aina ya kwelea kwelea na viwavijeshi vamizi, ” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha uwepo wa ugonjwa wa Uviko-19 uliathiri shughuli za kilimo kwani ulisababisha changamoto katika upatikanaji wa pembejeo muhimu za kilimo kama vile mbegu, mbolea, viuatilifu na zana za kilimo.
Janga hilo lilichangia watu kupoteza ajira na biashara, na hivyo kukosa kipato kwa ajili ya kukidhi ya mahitaji ya kila siku ya chakula.
Tangazo: