Wanasayansi kuja na chanjo ya Uviko-19 ya kunywa

January 25, 2023 8:40 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Matokeo ya utafiti wa awali yaonyesha mwitikio chanya. 
  • Inatarajiwa itachochea ongezeko la watu wanaopata chanjo.

Dar es Salaam. Huenda idadi ya watu wanaopata chanjo ya Uviko-19 ikaongezeka siku za usoni pale wanasayansi watakapokamilisha utafiti wao kuhusu chanjo ya ugonjwa huo ambayo mtu anaweza kuipata kwa kunywa.

Mpaka sasa katika aina zote za chanjo zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), huingizwa katika mwili wa binadamu kwa kutumia njia ya sindano jambo ambalo limekuwa kigezo kwa baadhi ya watu kutochanja kwa kuogopa maumivu ya sindano.

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya teknolojia ya nchini Marekani ya Cnet watafiti na wanasayansi wameongeza nguvu katika ugunduzi wa chanjo mpya kupitia mfumo wa upumuaji au kinywa.

Chanjo hiyo itakayofahamika kama QYNDR (kinder),  imeshakamilisha sehemu ya kwanza ya majaribio yake na sasa inasubiri fedha kwa ajili ya majaribio zaidi na kisha iingizwe sokoni.

Kwa mujibu wa Kyle Flanigan ambaye ni mtengenezaji wa chanjo hiyo, ‘kinder’ itatumia njia rafiki kuingia kwenye mwili wa binadamu.

Flanigan anasema matokeo ya utafiti wa chanjo hiyo yaliyofanyika nchini New Zealand yana mwitikio chanya ingawa bado hayajakaguliwa na mamlaka za kiafya za kimataifa.

“Si rahisi kutengeneza na kuifanya  na chanjo iweze kufanya kazi kupitia mfumo wa mmeng’enyo, tuligundua njia itakayoifanya chanjo ipite tumboni na kutoa matokeo yanayofaa, “ anasema Flanigan.

Habari za uwepo wa majaribio ya chanjo za Uviko-19 kwa njia ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula zinakuja kipindi ambacho mzalishaji wa chanjo za Pfizer anakabiliwa na ukosoaji mkubwa nchini Marekani kuhusiana na ufanisi wa chanjo zake.

Hata hivyo mpaka sasa WHO hawajatoa taarifa yoyote ya kuthibitisha shutuma hizo dhidi ya Pfizer zaidi ya kuendelea kusisitiza matumizi ya chanjo kwani zimesaidia kuokoa mamilioni ya maisha ya watu.

Wataalamu wa afya wanaendelea kusisitiza kuwa ugonjwa wa Uviko-19 bado upo na unaua  ingawa kwa kasi ndogo ambapo kwa mujibu wa WHO Januari 23 mwaka huu watu 1,017 walipoteza maisha siku hiyo huku jumla ya watu milioni 6.7 wakipoteza maisha tangu kuanza kwa janga hilo mwaka 2019.

Enable Notifications OK No thanks