Mikoa inayoongoza maambukizi ya VVU Tanzania
Dar es Salaam. Licha ya jitihada za kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU), bado kuna baadhi ya mikoa nchini ina kiwango kikubwa cha maambuzi ya VVU, mara 2 zaidi ya wastani wa kitaifa wa 4.4% kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi 2022-23 wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ( NBS).
Maambukizi ya VVU Tanzania yamepungua ndani ya miaka 19 kutoka 7% mwaka 2003/04 hadi 4.4% mwaka 2022-23.
Hali ya maambukizi ya VVU kwa watu wenye miaka 15 au zaidi mwaka 2022/23 kitaifa ni asilimia 4.4% wanawake wakiwa na asilimia 5.6 na wanaume asilimia 3.0. Hii ina maana kuwa kitaifa watu 44 kati ya 1,000 wenye miaka 15 au zaidi wana maambukizi ya maradhi hayo. Kwa jinsia, hii ina maana kuwa wanawake 56 kati ya 1,000 wana VVU wenye umri huo ikilinganisha na wanaume 30 kwa kila 1,000.
Vijana ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa maradhi hayo ammbapo miongoni mwa mipango ya Serikali ya Tanzania kwa sasa ni kupunguza maambukizi mapya hususan kwa vijana balehe pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Unafikiri ni kwa nini mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Kagera ina viwango vikubwa vya maambukizi ya VVU Tanzania?