2024 yaanza na neema kwa watumiaji vyombo vya moto, bei ya mafuta yashuka kiduchu
- Petroli yashuka kwa Sh54 na dizeli kwa Sh148.
- Ewura waeleza sababu za kushuka kwa bei ya mafuta.
- Bei ya mafuta ya taa yaendelea kung’ata.
Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania wanaendelea kupata ahueni kidogo mara baada ya bei ya petroli na dizeli kushuka kiduchu, ikichangiwa na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Kwa miezi mitatu mfululizo sasa bei ya mafuta imekuwa ikipungua tangu ilipopanda mfululizo kwa miezi mitano kuanzia Julai 2023 hadi Oktoba 2023 jambo lililoacha maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto.
Ahueni ya bei ya mafuta ilianza kuonekana Novemba 2023, ambapo bei yake ilishuka kiduchu ikifuatiwa na mwezi Disemba 2023.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo Januari 3, 2024, lita moja ya petroli Jijini Dar es Salaam inauzwa Sh 3,084 ukilinganisha na Sh3,138 Â iliyokuwa ikitumika mwezi Disemba mwaka jana.
Soma zaidi :Â Umemejua wapunguza maumivu kwa wafanyabiashara Morogoro
Ahueni hiyo katika bei ya mafuta ya petroli ni ya Sh54 tu ambayo ni kwa mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Bei ya mafuta ya dizeli yanayopita bandari ya Dar es Salaam nayo imeshuka kwa Sh148 kutoka Sh3,226 iliyokuwa ikitumika mwezi Disemba hadi Sh3,078 inayoanza kutumika leo.
Bei imeshuka katika bandari nyingine pia, ambapo kwa mafuta yanayopita Bandari ya Mtwara lita moja ya dizeli inauzwa Sh3,456 na petroli Sh3,201 huku yale yamayopita Bandari ya Tanga ni Sh3,064 kwa lita ya petroli na Sh 3,219 kwa lita moja ya dizeli.
Mafuta ya taa bei juu
Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa bei ya dizeli na petroli, bei ya mafuta ya taa imeendelea kuwa juu jambo litakalowaumiza watumiaji wake ambapo kwa Bandari ya Dar es Salaam, bei imepaa kutoka Sh3,423 mwezi Disemba hadi Sh 3,510 ikiwa ni ongezeko la Sh87.
Maumivu ya bei ya mafuta ya taa yanaendelea katika bandari nyingine ikiwemo ya Tanga ambako huko lita moja inauzwa Sh3,556 huku Mtwara ikiuzwa Sh3,582 ambayo ndio ya juu zaidi.
Mafuta ya taa ni bidhaa inayotumiwa zaidi na watu kutoka wenye kipato kidogo hususan waishio maeneo ya vijijini kama chanzo cha nishati ya mwanga, ambapo hutumika kuwashia taa, karabai au majiko.
Sababu za kushuka kwa bei ya mafuta zatajwa
Soma zaidi : Umemejua unavyowakwamua wanawake kiuchumi Tanzania
Ewura imebainisha kuwa, kushuka kwa bei ya mafuta kwa mwezi Januari kumechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la duniaÂ
“Kupungua kwa bei za mafuta kwa mwezi Januari 2024 ni kwa sababu ya kushuka kwa bei za mafuta (FOB) katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia 6.03 kwa petroli na asilimia 7.13 kwa dizeli,” imesema Ewura.
Aidha, Ewura wameongeza kuwa, kupungua kwa bei za mafuta kumetokana na kushuka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 3.72 kwa petroli na asilimia 17.52 kwa dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam na kwa wastani wa asilimia 22.71 kwa petroli na asilimia 22.12 kwa dizeli kwa Bandari ya Mtwara.