Bajeti ya Wizara ya Ardhi yapungua kwa Sh7.2 bilioni 2025/26
- Yapungua kwa asilimia 4.22 kulinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025
Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imepungua kwa Sh7.2 bilioni, sawa na asilimia 4.13 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 licha ya kuwa na vipaumbele saba vya kutekeleza.
Katika hotuba ya bajeti iliyosomwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi, Bunge limeidhinisha jumla ya Sh164.146 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha.
Kiasi hicho kinajumuisha fedha za matumizi ya kawaida na za maendeleo kwa Wizara ya Ardhi na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
“Fedha hiyo imepungua kwa Sh7.2 bilioni sawa na punguzo la asilimia 4.22 kutoka Sh171.372 zilizoombwa katika mwaka wa fedha 2024/2025,” amesema Ndejembi.
Kwa upande wa Wizara ya Ardhi pekee, bajeti kwa mwaka 2025/2026 imefikia Sh153.437 bilioni, punguzo la asilimia 2.55 kutoka Sh157.445 bilioni iliyoombwa mwaka jana.

Hata hivyo, bajeti ya matumizi ya kawaida ya wizara hiyo imeongezeka kwa Sh4.5 bilioni kutoka Sh86.7 hadi Sh91.3 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 5.28.
Wakati huo huo, bajeti ya miradi ya maendeleo imepungua kutoka Sh70.6 hadi Sh62.05 bilioni, ambapo ni upungufu wa Sh8.5 bilioni sawa na asilimia 12.17.
Aidha, Bunge limeidhinisha bajeti ya Sh10.7 bilioni kwa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, kiwango ambacho kimepungua kwa Sh1.46 bilioni sawa na asilimia 12.04 kutoka bajeti iliyoombwa mwaka uliopita.
Kwa upande wa matumizi ya kawaida ya tume hiyo, bajeti imeongezeka hadi Sh8.187 bilioni kutoka Sh7.132 bilioni, ongezeko la asilimia 14.79 sawa na Sh1.055 bilioni.
Hata hivyo, kiasi kilichotengwa kwa matumizi ya maendeleo kimepungua kwa asilimia 50.01 kutoka Sh5.041 bilioni hadi Sh2.520 bilioni, hali inayozua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya matumizi bora ya ardhi nchini.
Vipaumbele vya wizara
Katika bajeti hiyo Wizara imeweka vipaumbele saba ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na usajili wa ardhi mjini, vijijini na maendeo ya kimkakati, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya Wilaya na kuimarisha mipaka ya kimataifa na nkuendeleza miji ya mipakani.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha mifumi ya TEHAMA, kuweka nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na makazi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele pamoja na kuimarisha upatikanaji wa ramani kuwezesha mipango mbalimbali ya kitaifa na matumizi mengine.
Maoni ya Kamati ya Bunge
Kamati ya Bunge kupitia mwenyekiti wake Najma Giga, imeeleza kutoridhishwa na kiwango cha ukusanyaji wa madeni katika wizara hiyo ambapo kamati imeeleza kuwa udhaifu huo unachangia kupunguza mapato ambayo wizara ingeweza kuyakusanya.
Aidha, Kamati imeishauri wizara kuongeza bajeti ya matumizi ya maendeleo ili kuboresha utekelezaji wa miradi na kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za ardhi nchini.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa licha ya ongezeko la matumizi ya kawaida katika baadhi ya maeneo, kupungua kwa fedha za maendeleo hasa kwenye Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kunaashiria changamoto katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya matumizi bora ya ardhi jambo linaloweza kuathiri kasi ya upimaji, upangaji na utoaji wa hatimiliki nchini.
Latest



