Bajeti Wizara ya Maendeleo yaongezeka kwa asilimia 11.9 

May 27, 2025 2:06 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaongezeka kwa Sh8.1 bilioni kulinganisha na ile ya mwaka 2024/25.
  • Wizara imejipanga kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza vitendo vya ukatili.

Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 imeongezeka kwa asilimia 11.9 hadi kufikia Sh76 bilioni huku sehemu kubwa ya bajeti hiyo ikielekezwa katika matumizi ya kawaida.

Bajeti hiyo imeongeza kwa Sh8.1 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita ya Sh67.9 bilioni.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha ujao leo Mei 27, 2025 bungeni Dodoma amesema kuwa kati ya fedha inayoombwa, Sh49.1bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

“Kati ya fedha hizo matumizi mengineyo ni Sh26.46 bilioni na Sh22.6 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi,” amesema Dk Gwajima.

Fedha za miradi ya maendeleo ni Sh26.94 bilioni sawa na asilimia 35.4 ya bajeti yote ya mwaka ujao. Kati ya fedha hizo za maendeleo, fedha za ndani ni Sh15.4 bilioni na fedha za nje ni Sh 11.5 bilioni.

Viongozi watendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakiongozwa na Katibu Mkuu Dk John Jingu wakati wa utambulisho bungeni leo Mei 27, 2025. Picha/Maendeleo jamii.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26 wizara hiyo imepanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo kukuza hali ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa ngazi ya msingi.

Pia itaratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi na maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza vitendo vya ukatili, uwezeshaji wanawake kiuchumi na upatikanaji wa malezi bora katika familia.

Vipaumbele vingine ni kutambua, kuratibu maendeleo na ustawi wa makundi maalum wakiwemo watoto, wazee na wafanyabiashara ndogo ndogo. 

Wizara itaelekeza juhudi zake katika boresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi na vyuo vya ustawi na maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa mashirika yasio ya Serikali katika maendeleo ya Taifa. 

Licha ya wizara hiyo kuimarisha hatua za kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini kwa kushirikiana wadau mbalimbali, vitendo hivyo bado vinashamiri.

Kwa mujibu wa Dk Gwajima kwa mwaka 2024/25,  jumla ya manusura wa ukatili 19,717 walilipotiwa wakiwemo watoto 7,278 walihudumiwa katika madawati ya kijinsia.

Kamati yatoa mapendekezo yake

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq amesema ucheleweshwaji wa upatikanaji wa fedha umeendelea kuwa changamoto inayoathiri utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

“Kutokana na majukumu ya wizara hii kuwa mtambuka na kugusa maeneo nyeti ya jamii, hasa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na ustawi wa makundi maalum, ipo haja ya dharura ya kuiongezea bajeti ili iweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo.” amesema Toufiq. 

Amesema kamati yake inaendelea kuishauri Serikali kuipa kipaumbele wizara hiyo kwa kuzingatia nafasi yake katika kujenga jamii jumuishi na yenye maendeleo endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks